Tafuta

Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote ndiyo kauli mbiu ya Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2018 Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote ndiyo kauli mbiu ya Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2018 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Kimisionari Duniani kwa mwaka 2018

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimisionari Duniani kwa mwaka 2018, inayoongozwa na kauli mbiu “Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote”, anawaalika waamini wote kushikamana na vijana katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kwa kipindi cha mwaka 2018, katika mikakati yake ya kichungaji ametoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya familia pamoja na vijana kama inavyojionesha wakati huu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Kwa kutambua umuhumi wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimisionari Duniani kwa mwaka 2018, inayoongozwa na kauli mbiu “Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote”, anawaalika waamini wote kushikamana na vijana katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wote.

Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2018 inaadhimishwa Jumapili tarehe 21 Oktoba 2018. Ushuhuda wa Injili ni changamoto endelevu kwa Wakristo wote! Lakini, umisionari unawataka Wakristo kuwa na moyo na ari ya ujana, ili kuthubutu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimisionari Duniani, anakazia umuhimu wa maisha kuwa ni sehemu ya utume wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anawakumbusha watoto wa Mungu kwamba imani ya Kikristo daima itaendelea kufumbatwa katika ujana, kwani utume wa Kanisa unapyaisha imani, kama alivyozoea kusema Mtakatifu Yohane Paulo II aliyewapenda vijana katika maisha na utume wake. Mama Kanisa katika mwezi huu wa Oktoba, anaadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, fursa ya pekee kwa Kristo Yesu kuzungumza na vijana na kwa njia ya vijana, Habari Njema ya Wokovu iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Vijana ambao bado wana ari, moyo na upendo mkuu, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kutambua kwamba, hii ni changamoto kubwa katika maisha na utume wao; kuna mwanga na giza, lakini matumaini ni makubwa zaidi kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kila mwamini anahamasishwa kutafakari kwamba, yeye ni sehemu muhimu ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kanisa linatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya uhuru wa ndani unaowasukuma kugundua na hatimaye, kutangaza ujumbe huu kwa ari na moyo mkuu.

Vijana kamwe wasiomwogope Kristo na Kanisa lake, kwani Yeye ni chemchemi ya furaha ya maisha ya uzima wa milele, msingi wa ndoto wanazoweza kuzitekeleza katika maisha yao. Vijana wanakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha kama vile: mateso, umaskini na upendo wa dhati; kuna umati wa vijana ambao umejisadaka bila ya kujibakiza, kiasi hata cha kuthubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya upendo kwa Injili na huduma kwa jirani, mfano na kielelezo makini kutoka kwa Kristo Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu na Injili ni kwa ajili ya uzima wa milele.

Upendo wa Kristo unawabidisha na kuwajengea ari na moyo mkuu; unawaangaza na kuwatia shime kukua na kukomaa katika upendo. Shule ya watakatifu, inawafungulia mwelekeo mpana zaidi wa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kujiuliza, katika nafasi zao, Yesu angafenya kitu gani? Hii ni changamoto ya kutangaza na kushuhudia imani hadi miisho ya dunia, changamoto kwa vijana ambao bado wanafurahia ujana wa imani unaobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na kuwaambata wote, kiasi hata cha kuwatia shime na kuwahamasisha kuwa ni mashuhuda amini, wenye matumaini kwa siku za usoni.

Ujana ni chemchemi ya matumaini kwa wale ambao bado wako safarini. Lakini, ikumbukwe kwamba, utume wa Kanisa unawafumbata watu wa marika yote katika jamii na kwa mantiki hii, Kanisa linakuwa ni daraja na kiungo muhimu kati ya vizazi kwa njia ya imani. Urithishaji wa imani, kiini cha utume wa Kanisa unatekelezwa kwa njia ya ushuhuda wa upendo na furaha ya Injili, kielelezo cha utimilifu wa maisha. Upendo hauna mipaka kwani unaibua fursa za waamini kukutana, kushuhudia, kutangaza na hatimaye, kushirikishana upendo hata na wale ambao wako mbali na imani ya Kanisa. Bado kuna watu na mazingira ambayo hayajaguswa na Injili ya Kristo, uwepo wa Kanisa Kisakramenti; maeneo ambayo, Kristo Mfufuka anapenda kuwatuma waja wake kutangaza na kushuhudia Injili, daima wakitambua kwamba, yuko pamoja nao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ndio Uinjilishaji wa awali kwa watu wa Mungu. Watu wanaotengwa, wasiokuwa na mvuto katika imani, wanaoogea katika dhuluma na magumu ya maisha, kwa maneno machache, watu wanaoishi pembezoni mwa ubinadamu, hao ndio wenye kiu ya kutaka kuonja uwepo wa Kristo katika maisha yao. Umaskini wa maisha ya kiroho, hali na kipato, ubaguzi wa watu daima imekuwa ni alama ya kumkana Mungu na upendo wake! Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, leo hii umbali umefupishwa sana na kuta za mipaka kuvunjiliwa mbali, kiasi kwamba, ulimwengu umekuwa kama kijiji.

Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu ni watu kujenga umoja na mshikamano unaofumbatwa katika maisha. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema unahitaji sadaka na majitoleo. Kwa kijana anayetaka kumfuasa Kristo Yesu hana budi kujibidisha kutamfuta na hatimaye, kuchuchumilia maisha ya wito wake. Baba Mtakatifu anawashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya kimisionari sehemu mbali mbali za dunia, kwa kudumisha utu na heshima ya binadamu; pamoja na kushuhudia furaha ya kupenda na kuwa Mkristo.

Hii ni shule inayowaandaa watu wa Mungu kutoa huduma makini kwa jirani. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka katika huduma ya kimisionari, kwa kuwasaidia vijana kufanya mang’amuzi ya miito yao, ili siku moja waweze kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama wamisionari. Mashirika ya kimisionari ya kipapa ni matunda ya moyo wa ujana, yanayoendelea kusaidia kukuza utu na utamaduni wa watu mbali mbali, wenye kiu ya ukweli. Mchango wa hali na mali kutoka katika Mashirika haya, unaliwezesha Kanisa kutoa ushuhuda wenye mvuto.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, hakuna mtu anayeweza kudai kwamba ni maskini kiasi kwamba hana hata kitu kidogo cha kutoa, au tajiri kiasi kwamba, haitaji msaada wowote kutoka kwa wengine. Watu watambue kwamba, wanapaswa kusaidiana na kwa njia hii wanakamilishana. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yawasaidie kujenga na kudumisha ari na moyo wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

ujumbe wa Papa 2018
18 October 2018, 14:43