Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Mdahalo kati ya vijana na wazee: tunu msingi, shuhuda, ndoto na matumaini ya vijana! Papa Francisko: Mdahalo kati ya vijana na wazee: tunu msingi, shuhuda, ndoto na matumaini ya vijana!  (Vatican Media)

Papa Francisko: mdahalo kati ya vijana na wazee: shuhuda, tunu, ndoto na matumaini!

Baba Mtakatifu amejibu maswali kutoka kwa wazee na vijana; akasikiliza shuhuda; ndoto na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya; na wazeee wakashirikisha amana na utajiri unaobubujika kutoka katika uzoefu na mang’amuzi ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Majadiliano ya kina kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya sanjari na mshikamano wa upendo ni kati ya changamoto kubwa zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” itakayohitimishwa hapo tarehe 28 Oktoba 218. Tarehe 23 Oktoba 2018 kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi, Baba Mtakatifu ameongoza mdahalo kati ya vijana na wazee, uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Augustinianum kilichoko mjini Roma.

Katika tukio hili, Baba Mtakatifu amezindua kitabu cha mkusanyo wa mahojiano 250 yaliyofanywa kutoka katika nchini zaidi ya 30. Kitabu hiki kinajulikana kama “Sharing the wisdom of time” yaani “Kushirikishana busara ya nyakati” ni msaada mkubwa wa majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya na kimehaririwa na Padre Antonio Spadaro, mkurugenzi mkuu wa Jalida la “Civiltà Cattolica”. Baba Mtakatifu amejibu maswali kutoka kwa wazee na vijana; akasikiliza shuhuda; ndoto na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya; na wazeee wakashirikisha amana na utajiri unaobubujika kutoka katika uzoefu na mang’amuzi ya maisha!

Vijana wanasema, utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani ni chanzo cha ubinafsi, mashindano yasiyokuwa na tija, kiasi cha kuwavuruga vijana na kuanza kujisikia si mali kitu na matokeo yake ni kutumbukia katika upweke hasi unaowachimbia shimo la kifo! Baba Mtakatifu anasema, furaha ya kweli inafumbatwa katika kanuni maadili na utu wema. Hii ni safari inayomwezesha kijana kusimama na kutafakari vipaumbele katika maisha, kwa kutambua kwamba, kuna heri na furaha kubwa kutoa kuliko kupokea, kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma makini, kiasi hata cha kuthubutu kutenda, tayari kuambata mambo makuu zaidi yanayoimarisha: umoja, udugu na mapendo! Huu ndio utamaduni wa huduma, chimbuko la furaha ya kweli.

Familia ya Tony na Grace Naudi kutoka Malta, ambayo imedumu katika ndoa yake kwa miaka 43, inasema, imejitahidi kuwalea na kuwafunda watoto wao katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu; wakawa makatekista wa kwanza wa Neno la Mungu pamoja na kujitahidi kuwarithisha imani! Wanandoa hawa wanasema, wanasikitishwa sana wanapowaona vijana hawana tena ari na mwamko katika imani, maadili na utu wema, kiasi cha kuogelea na kutopea katika malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wazazi na walezi kukuza na kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na watoto wao, ili kurithisha imani, mchakato unaoanza ndani ya familia, katika hali ya urafiki na ujirani mwema, kiasi kwamba, katekesi inakuwa ni sehemu ya ushuhuda wa uhalisia wa maisha. Katika shida, mahangaiko na madhulumu ya Kanisa, wazazi na walezi ndio waliojitwika dhamana ya kuwarithisha watoto wao imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Wazazi na walezi wahakikishe kwamba, wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa malezi na makuzi! Vijana wanawajibika katika maamuzi yao, kumbe, wanapaswa kutenda kwa kuzingatia dhamiri nyofu. Hakuna sababu ya wongofu wa shuruti, imani inarithishwa kwa njia ya ushuhuda unaomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji.

Wazazi na walezi, wajifunze utamaduni wa kusikiliza, kuwapokea na kuwasindikiza watoto wao katika hija ya maisha, kwa kutambua kwamba, wanaweza kuanguka na kutumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, pamoja na ulevi wa kupindukia mambo yanayowapelekea kukosa hata fursa za ajira. Mbegu ya imani, maadili na utu wema, iliyopandwa katika uhalisia wa maisha, iko siku, itazaa matunda ya toba na wongofu wa ndani.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kuna sababu lukuki zinazopelekea vijana kutopea katika malimwengu: kwanza kabisa ni kashfa na makwazo kutoka kwa viongozi wa Kanisa; ukosefu wa mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama Kristo mwenyewe aliyewaonea huruma waja wake akawaondolea dhambi, akawaponya magonjwa yao na kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama watoto wapendwa wa Mungu. Mtakatifu Monica, Mama yake Mtakatifu Augostini, Askofu na mwalimu wa Kanisa, awe ni mfano wa udumifu katika sala na malezi kwa watoto wao na kamwe wasikate tamaa, kwani iko siku, machozi yao, yatawapatia ushindi wa toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha! Ushuhuda makini unalipa, wazazi jaribuni, mtaona siri ya mafanikio anasema Baba Mtakatifu.

Rosemary Lane, kutoka USA, anasema, amebahatika kwa kipindi cha mwaka mzima, kukusanya na kuhariri busara za wazee kutoka sehemu mbali mbali za dunia na matokeo yake ni Kitabu cha “Sharing the wisdom of time” yaani “Kushirikishana busara ya nyakati”. Anasema, amekutana na wazee wanaopambana na hali ya maisha yao, ili kuendelea kuwa na matumaini, lakini kwa bahati mbaya, vijana wengi hawana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Ni watu wanaonekana kana kwamba, wanaelemewa na taabu pamoja na changamoto za maisha, kiasi cha kujikatia tamaa.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na ndoto inayomwilishwa katika vipaumbele na mitazamo ya maisha; kwa kuwajibika kikamilifu ili kujenga mafungamano ya kijamii kati ya vijana na wazee; ili kuwa na mwelekeo mpya wa maisha na hatimaye, kukua na kukomaa. Wazee wamepitia furaha na machungu ya maisha; wanayo mang’amuzi na uelewa mpana!

Mama Fiorella Bacherini kutoka Italia, mwenye umri wa miaka 83 mwalimu wa lugha ya Kiitalia kwa wakimbizi na wahamiaji anasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mipasuko, chuki, uhasama na ukatili mkubwa dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! Hapa mkazo si mambo ya siasa bali utu na heshima ya binadamu! Madhara ya vita, kinzani za kijamii, mabadiliko ya tabianchi, umaskini, njaa na ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya mambo yanayochangia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi wengi wanapoingia madarakani wanakuwa na ndoto ya maendeleo endelevu na fungamani kwa raia zao, lakini wanapoanza kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama matokeo yake ndiyo hayo ya Vita Kuu ya Dunia. Katika mwelekeo kama huu, chuki za kisiasa zinajiingiza na kupenya hata katika maisha ya kiroho, kama ilivyotokea kwa Wakatoliki na Waluteri; miaka hamsini imepita, Wakristo wanataka sasa kujenga umoja, upendo na mshikamano kwa kuzika tofauti zao msingi na hivyo, kuendelea kujikita katika mambo yanayowaunganisha zaidi.

Papa Francisko anasema, haya ndiyo mambo yanayofumbatwa katika: Mauaji ya kikabila; kwa kuwachafulia wengine utu na heshima yao; kwa kuwanyima watu hifadhi na usalama wa maisha, kiasi kwamba, leo hii, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi kwa wakimbizi na wahamiaji wengi. Ubabe, ushindani wa silaha, chuki na uhasama wa kitaifa na kimataifa, ni mambo yanayoendelea kupandikiza hofu ya kuzuka Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, ambayo kwa sasa inapiganwa vipande vipande! Wahamiaji na wakimbizi ni sehemu ya historia ya mwanadamu, ustawi na maendeleo ya wengi: kitamaduni na hata katika maisha ya kiroho!

Historia ya Ulaya anasema Baba Mtakatifu inafumbatwa katika shuhuda za wakimbizi na wahamiaji, jambo la msingi ni kuwapokea, kuwalinda, kuwahifadhi na kuwashirikisha katika uhalisia wa maisha, vinginevyo, wanaweza kuwa ni wahanga wa vitendo vya kigaidi kama inavyoshuhudiwa huko nchini Ubelgiji! Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inapaswa kuonesha mshikamano katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, ili Bahari ya Mediterrania isiwe tena kaburi lisilo na alama! Huu ni ushuhuda wa kiutu na wala si uragibishaji wa kisiasa!

Yennifer Tatiana Valencia Morales, kutoka Colombia anasema, Kitabu cha “Sharing the wisdom of time” yaani “Kushirikishana busara ya nyakati” kimesheheni utajiri mkubwa wa: uzoefu, mang’amuzi, shida, mahangaiko na matumaini ya wazee, lakini kwa bahati mbaya ni kundi ambalo halina nafasi tena ya kusikilizwa. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuihamasisha familia ya Mungu kujenga majadiliano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya na kuboresha ujuzi, maarifa na mang’amuzi ya maisha, mambo ambayo pengine si rahisi sana kupatikana kwenye vitabu! Familia iwe ni jukwaa la majadiliano, shule ya upendo na upyaisho wa maisha. Wazee wenye busara ni hazina na utajiri mkubwa wa malezi na makuzi ya vijana. Wazee ni utambulisho na asili ya jamii, ni wimbo wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kama walivyokuwa akina Simeoni na Ana! Ni mwaliko wa kujikita katika majadiliano kati ya vijana na wazee.

Bwana Martin Scorsese, mtunzi na mcheza filamu mashuhuri duniani, aliyejitahidi katika ujuzi wake kuwaonesha walimwengu athari za umaskini na vita, changamoto kwa waamini ni kumwilisha upendo wao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, kashfa na makwazo ni changamoto pevu kwa waamini kulitakatifuza Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto! Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasimame kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Ukatili wa mwanadamu, uwasukume waamini kumwomba Mungu zawadi ya kulia, ili kulainisha akili na nyoyo na kwamba, kilio ni sehemu ya ubinadamu! Ni muda wa kuoneshana huruma na upendo; kusamehe na kusahau; kwa kujikita katika upole na unyenyekevu; ili kuwaendea maskini na wale wote wanaoteseka. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwabariki wote, huku akiomba waendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao!

Papa na Vijana
24 October 2018, 10:33