Tafuta

Vatican News
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018 wametoa hati ambayo imeridhiwa na Papa Francisko. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018 wametoa hati ambayo imeridhiwa na Papa Francisko.  (Vatican Media)

HATI YA MABABA WA SINODI YA MAASKOFU KWA VIJANA 2018

Mababa wa Sinodi wamesafiri pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakafanya kazi kwa umoja, huku wakizingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha kujisikia kuwa ni fumbo la mwili mmoja, unaoteseka na kufurahia, ili kwa njia ya neema ya Mungu, Kanisa liweze kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kipindi cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, 2018, Kanisa limejenga na kuimarisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya, tayari kujibu matamanio yao halali, yatakayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wamejitahidi kutembea kwa pamoja huku wakisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu aliyeendelea kuwashangaza kwa karama na mapaji mbali mbali pamoja na nguvu ya kuwapatia walimwengu matumaini!

Mababa wa Sinodi wamesafiri pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakafanya kazi kwa umoja, huku wakizingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha kujisikia kuwa ni fumbo la mwili mmoja, unaoteseka na kufurahia, ili kwa njia ya neema ya Mungu, Kanisa liweze kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Vijana wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Kanisa limeonekana kuwa ni jukwaa la majadiliano na shuhuda wa udugu. Hali hii ni sehemu ya mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Kumekuwepo na utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi, maswali na majibu dodoso kutoka kwa vijana kwa njia ya mitandao ya kijamii, hati ya kutendea kazi na sasa Mababa wa Sinodi wametoa Hati ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Mapendekezo yote yamepigiwa kura na hatimaye kupitishwa na Baba Mtakatifu Francisko kukabidhiwa naye ameamuru kwamba, hati hii ichapwe, ili iweze kuwa ni dira na mwongozo wa Kanisa kwa sasa na kwa miaka ijayo! Huu ni muhtasari wa kile ambacho Mababa wa Sinodi wamekitambua, wakakitafsiri na kuamua kukichagua kwa mwanga wa Neno la Mungu. Haya ni matunda ya tofauti msingi zinazofumbatwa katika umoja unaokamilishana, baada ya kujadiliana na kusikilizana kwa muda wa miaka miwili.

Hati hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo  zimejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka. Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanayataka Makanisa mahalia kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa, daima yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

SEHEMU YA KWANZAYesu alikua akiandamana nao! Hapa Mababa wa Sinodi wanapenda kujikita kwa kupembua umuhimu wa Kanisa linalosikiliza kwa makini; mchango wa Sinodi tatu zilizotangulia; utambulisho na umuhimu wa mahusiano na manfungamano na vijana wa kizazi kipya!

Hati inapembua kwa kina na mapana hali na mazingira ya maisha ya vijana, nguvu, udhaifu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao. Kanisa linataka kuwasikiliza kwa makini, katika hali ya unyenyekevu, uvumilivu na uwajibikaji, unaolisukuma kufanya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi pamoja na vijana, ili kujibu kilio na matamanio yao halali pasi na haraka ya kuwa na majibu yaliyotengenezwa kwenye maabara. Kwa hakika, vijana wanataka kusikilizwa, kutambuliwa, kuthaminiwa na hatimaye, kusindikizwa na wanataka sauti yao iweze kusikika na kufanyiwa kazi katika jamii na ndani ya Kanisa.

Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, si nyakati zote, Kanisa limekuwa na mwelekeo kama huu, kwani wakleri na watawa wameonekana kuwa na mambo mengi kiasi cha kukosa muda wa huduma ya kuwasikiliza vijana. Umefika wakati wa kuwaandaa hata waamini walei watakaojisadaka kwa ajili ya kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya. Maendeleo ya sayanasi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanaendelea kuwa ni msaada mkubwa kwa vijana kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao na tasaufi, mambo ambayo yanaweza kutumiwa na Kanisa kama chachu ya kufufua imani miongoni mwa vijana!

Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu pamoja na vituo vya michezo ni mahali muafaka pa malezi na makuzi endelevu na fungamani; ni mahali pa shuhuda za kiinjili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna mwingiliano wa pekee kati ya familia, kazi, ulinzi wa uhai pamoja na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Taasisi za elimu na michezo zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, ziwe ni mahali pa kujenga misingi ya imani, kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; ni mahali pa kukabiliana na changamoto za kisayansi na kiteknolijia kwa mwanga wa Injili na kwamba, mabadiliko ya kijamii yanapaswa kuratibiwa na haki jamii. Kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa kuhusu utume wa Parokia, ili kujenga ari na mwelekeo mpya wa kimisionari kwa kujikita katika katekesi ya awali na endelevu.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto katika ulimwengu mamboleo na wala si suala mtambuka! Kuna idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi watoto wasioandamana na wazazi wala walezi wao! Hawa ni wale wanaokimbia: vita, nyanyaso na dhuluma; maafa asilia na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini na matokeo yake, wanaishia kutumbukia katika mikono dhalimu ya wafanyabiashara haramu ya binadamu; utumwa mamboleo; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na nyanyaso za kisaikolojia na kimwili.

Kanisa linaguswa sana na mahangaiko ya watu hawa, linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki zao msingi; kwa kuwapokea, kuwahifadhi, kuwalinda na kuwashirikisha, pale inapowezekana, waunganishwe na familia zao asilia. Wakimbizi na wahamiaji ni hazina na utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho na kiutu kwa jamii inayowapatia hifadhi, kwani kwa njia ya ukarimu wanaweza pia kutajirishana. Mambo makuu ya kuzingatia ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha kama sehemu ya utamaduni unaofyekelea mbali maamuzi mbele, woga, uchoyo na ubinafsi! Maaskofu wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, haki ya watu kubaki nchini mwao inalindwa. Dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo zimegusiwa pia katika hati hii, mambo yanayopelekea uhamiaji wa nguvu na shuruti!

Dhamana na wajibu wa kupambana na: kashfa za nyanyaso; ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka, kwa kujizatiti katika ukweli na uwazi; kwa kuomba msamaha na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka. Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia inatekelezwa ili kashfa hizi zisijirudie tena ndani ya Kanisa, kwa kuzingatia uteuzi, malezi na majiundo ya majandokasisi pamoja na walezi wanaopewa dhamana na Mama Kanisa katika utume huu.

Mababa wa Sinodi wanawapongeza wale wote waliokuwa na ujasiri wa kusema ukweli kuhusu nyanyaso walizotendewa, hali ambayo imelisaidia Kanisa kuamua na kutenda kwa ujasiri, kwa kuzingatia huruma na haki. Lakini, ikumbukwe kwamba, kuna umati mkubwa wa wakleri na watawa wanaojisadaka bila ya kujibakiza katika kuwahudumia watu wa Mungu, katika: ukweli na uaminifu na  kwamba, hawa wanaweza kuwa ni chachu ya mageuzi na upyaisho wa Kanisa katika mwelekeo huu.

Mababa wa Sinodi wanasema, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali rejea pa vijana na jumuiya ya kwanza ya imani, changamoto na mwaliko kwa wazazi, walezi na wazee kusaidia mchakato wa elimu ya dini na urithishaji wa imani sanjari na kuendeleza dhamana na wajibu wa wanaume katika maisha na utume wa familia, dhana ambayo kwa sasa inakumbana na changamoto nyingi, kutokana na ukweli kwamba, malezi na makuzi ya watoto wengi yanatekelezwa na wanawake kutokana na familia kuwa tenge kwa sababu mbali mbali. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya kurithisha imani kwa vijana wenzao!

Hati ya Sinodi ya Maaskofu imejadili kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa Kanisa na Jamii kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Ukosefu wa fursa za ajira, umaskini; dhuluma na nyanyaso; kutengwa na jamii kutokana na sababu mbali mbali; ubaguzi na ukabila; mambo yanayohitaji wongofu na mshikamano! Vijana waendelee kujisadaka kwa kujitolea, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kujihusisha kikamilifu katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, ili kusimama kidete: kulinda: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kudumisha haki jamii, changamoto ambayo vijana wanataka kuona Kanisa inalivalia njuga pasi na mzaha!

Mababa wa Sinodi wanasema, sanaa, muziki na michezo ni rasilimali kubwa katika sera, mikakati na shughuli za kichungaji kwa vijana, kwani zinasaidia katika mchakato wa: elimu, malezi na mafungamano ya kijamii. Muziki unaweza kusaidia pia katika maboresho ya liturujia ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na mwanadamu kutakatifuzwa. Vijana wanataka kushirikishwa katika liturujia hai inayofumbatwa katika ukweli, furaha, ibada na uchaji wa Mungu, ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jumuiya ya waamini. Alama za liturujia, mahubiri yaliyoandaliwa vyema na ushiriki wa waamini ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Vijana wasaidiwe kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuthamini Liturujia ya Kanisa kwani hii ni kazi ya Kristo na Kanisa. Vijana wapewe nafasi ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa; wawajibike pamoja na kushirikisha vipaji na karama zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa kujenga utamaduni wa: kusikiliza na kujadiliana na vijana.

SEHEMU YA PILI: Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua. Mababa wa Sinodi wanakazia kuhusu Pentekoste mpya, zawadi ya ujana, fumbo la wito, utume wa kuwasindikiza vijana na sanaa ya kung’amua! Mwenyezi Mungu anazungumza na Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, kwa njia ya vijana, “majukwaa ya taalimungu”, mahali ambapo Kristo Yesu anapenda kujifunua kwa waja wake. Kutokana na sababu mbali mbali, vijana wa kizazi kipya wanaweza kuwa wamecharuka katika medani mbali mbali za maisha, kumbe, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwapokea, kuwaheshimu, kuwathamini na kuwasindikiza kama sehemu ya mchakato wa kulipyaisha Kanisa ambalo wakati mwingine, limekuwa likijikongoja. Mababa wa Sinodi wanamwona Kristo Yesu kuwa ni mfano kati pamoja na vijana, wanaosindikizwa pia kwa mifano na ushuhuda wa watakatifu ambao wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa katika ushuhuda wa kinabii unaoleta mageuzi katika maisha ya waamini!

Utume na wito miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni mwaliko kwa vijana kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kushirikisha furaha ya Injili katika ukweli na udumifu, huku Kristo Yesu akiwakirimia uhuru zaidi unaofumbatwa katika ukweli na upendo. Maisha ni wito unaojenga na kukuza mahusiano na Mwenyezi Mungu. Wito wa ubatizo ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Kila mwamini anapaswa kuishi vyema wito wake kadiri ya mazingira yake: kitaaluma, kifamilia, maisha ya kuwekwa wakfu, daraja takatifu na ushemasi wa kudumu ambao ni rasilimali inayopaswa kuendelezwa katika utimilifu wake!

Kuwasindikiza vijana: familia pamoja na wadau mbali mbali wanahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao ili kuwasindikiza vijana kuweza kufanya maamuzi magumu katika maisha. Lakini, wazazi, walezi na viongozi wa maisha ya kiroho wanahitaji “kupigwa msasa” katika malezi, kwa kuwa na nyenzo na vigezo muhimu vinavyowaongoza vijana katika maisha yao. Hawa ni vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya maisha na wito wa kipadre; vijana wanaotaka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia.

Jumuiya ya waamini ni mahali muafaka wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kikanisa. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanaguswa, wanafundwa, wanagangwa na kuponywa na Kristo Yesu. Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha na utume wa Kanisa; upatanisho katika maisha ya kiimani na kwamba, huu ni mwaliko kwa wadau mbali mbali kuwasaidia vijana kwa njia ya Mafundisho Jamii ya Kanisa kuwajibika barabara katika medani mbali mbali za maisha: kitaaluma, kisiasa na kiuchumi; kwa kuzingatia tofauti zinazofumbatwa katika umoja na mkamilishano unaojenga na kudumisha umoja katika udugu.

Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa maisha ya sala na useja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu: kielelezo makini cha uhuru wa ndani, furaha, sadaka na unyenyekevu. Kabla ya vijana kufanya maamuzi magumu ya kujiunga na wito na maisha ya kipadre na kitawa, wanapaswa kusaidiwa na watu wenye sifa na ubora; wanaoweza kuwasikiliza, kuwasindikiza katika imani na sala; kwa kuangalia uwezo na mapungufu yao, ikiwa kama wanastahili kusonga mbele. Wasahihishwe kwa upendo na udugu pale wanapokosea na kuondokana na tabia ya kutaka kuwamiliki vijana, hali ambayo wakati mwingine, imepelekea matumizi mabaya ya madaraka na hatimaye, nyanyaso mbali mbali!

Mababa wa Sinodi wanahimiza umuhimu wa kukuza na kudumisha sanaa ya mang’amuzi katika maisha, inayofumbatwa kwa kukutana na kujenga mahusiano na Kristo Yesu. Ni mahusiano yanayoendelea kwa njia ya majadiliano kati ya kijana na mlezi wa maisha ya kiroho, hali inayopaswa kueleweka kuwa ni mfano wa sala unaohitaji ujasiri na mapambano ya maisha ya kiroho, changamoto katika maisha ya kijumuiya katika udugu na huduma kwa maskini. Vijana wanayo mang’amuzi mapana kuhusu “diakonia” yaani “dhana ya huduma”.

SEHEMU YA TATU: Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kwa wafu! Mababa wa Sinodi wanakazia ujana wa Kanisa, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa katika kukuza na kudumisha ari na mwako wa kimisionari; Sinodi kama hija ya pamoja inayotekelezwa kila siku ya maisha; upyaisho wa ari ya kimisionari pamoja na malezi fungamani!

Mtakatifu Maria Magdalena, mfuasi mmisionari, aliyegangwa na kuponywa madonda yake na shuhuda wa ufufuko ni kielelezo makini cha ujana wa Kanisa. Machungu na madhaifu ya vijana, yanaliwezesha Kanisa kuboreka zaidi kutokana na changamoto zao, “madongo” ambao ni kama sauti ya Kristo inayolitaka Kanisa kutubu, kuongoka na kujipyaisha, kwani vijana wote ni muhimu sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa Kanisa kukumbatia na kuambata dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni ushuhuda wa tofauti zinazofumbatwa katika umoja na mkamilishano, changamoto kwa Mabaraza ya Maaskofu na Makanisa mahalia kuendeleza mchakato wa mang’amuzi, ili kuibua sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ili kukabiliana na matatizo na changamoto kwa Makanisa mahalia.

Dhana ya Sinodi ndiyo mwelekeo sahihi wa kimisionari unaolitaka Kanisa kutoka katika dhana ya ubinafsi na kuanza kujikita katika tunu msingi za maisha ya kijumuiya kwa kutambua changamoto changamani zinazotokana na mang’amuzi ya mahali wanakotoka watu pamoja na tofauti za kitamaduni, zawadi na karama kutoka kwa Roho Mtakatifu ili kusaidia mchakato wa maamuzi ndani ya Kanisa, kwa kuwashirikisha waamini walei katika kukuza na kujenga ari na mwamko wa kimisionari.

Uongozi uangaliwe katika jicho la huduma sanjari na mwendelezo wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha vijana katika utume wa Kanisa. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki hayana budi kuanzisha Kurugenzi ya Utume na Miito kwa Vijana ili kusaidia malezi na  majiundo ya vijana. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa na Kimataifa yamepewa mkazo wa pekee kabisa, bila kusahau umuhimu wa vituo vya malezi na michezo kwa vijana.

Changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa digitali zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu na Mama Kanisa, ili kuwasaidia vijana kuwajibika barabara katika malezi, makuzi na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, mahali ambapo kumegeuka kuwa ni “vijiwe vya vijana”. Mitandao ya kijamii, ina faida na hasara zake, changamoto ni kuwajengea vijana uwezo wa kuwa kweli ni raia wanaowajibika katika ulimwengu wa digitali, ili wasitumbukie katika upweke hasi utakaowapelekea katika kifo; wasinyanyaswe wala kudhalilishwa, bali waimarishwe ili kweli mitandao ya kijamii iweze pia kutumika katika kutangaza na kushuhudia nguvu ya Injili inayookoa!

Ni wakati wa kutamadunisha na kuinjilisha mitandao ya kijamii, kwa kuimarisha tovuti zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, ili kupambana na habari za kughushi “FAKE NEWS”, kielelezo cha utamaduni usiofumbata na kuambata ukweli. Ziwepo sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo katika tovuti. Kanisa liendelee kuwathamini, kuwaheshimu na kuwashirikisha wanawake katika maisha na utume wake, bila kusahau mchango wake katika jamii, kama sehemu ya upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika uongozi wa Kanisa na vikao mbali mbali vya maamuzi, kwa kuheshimu pia dhamana na wajibu wa wakleri waliopewa daraja, kwani hii ni sehemu ya haki inayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu.

Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa kuheshimu maadili na utu wema, kwa kuepuka picha za utupu zinazoendelea kuzagaa katika mitandao ya kijamii, utalii wa ngono pamoja na ukahaba wa kwenye mitandao. Vijana watambue na kuheshimu miili yao kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa liwasaidie vijana kutambua ukweli huu, ili kusaidiana na kukamilishana katika tofauti zao za kijinsia. Kanisa liwe na uwezo wa kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa tendo la ndoa, hali inayohitaji malezi na majiundo makini, kwa kukazia pia useja kama zawadi na sadaka katika maisha inayoweza kuwasaidia watu kufikia ukomavu katika miito mbali mbali.

Sehemu hii inahitaji walezi makini wanaoweza kuwasaidia vijana kutambua uzuri na utakatifu wa miili yao, jambo linaloweza kufafanuliwa: kiutu, kitaalimungu na kichungaji kadiri inavyofaa, ili kupambanua: tofauti na uhusiano wa jinsia ya kiume na kike; umuhimu wa kuondokana na nyanyaso za kijinsia kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa mahusiano ya kijinsia. Watu wenye mielekeo ya mahusiano ya ndoa za watu wa jinsia moja, wasaidiwe kutambua uhuru na wajibu wao.

Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa halina budi kutenga rasilimali fedha na watu kwa ajili ya kuwasindikiza vijana ili waweze kukua na kukomaa na hatimaye, kufanya mang’amuzi sahihi ya miito yao, kwa kuondokana na mazoea katika mazingira! Wanandoa wachanga waendelee kusindikizwa kwa njia ya ushauri na mifano ya familia bora za Kikristo, ambazo zinapaswa pia kushirikishwa kikamilifu katika malezi, majiundo na makuzi ya wanandoa wapya. Talaka na ndoa sugu ni kati ya matatizo makubwa yaliyobainishwa na Mababa wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, kwani kuna baadhi ya waamini ambao kwa makusudi mazima, wanafyekelea mbali sheria, kanuni na taratibu za Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia, tabia ambayo inawafanya waamini kama hawa kushindwa kuwajibika, na hivyo kuwa ni tatizo kubwa kwa jumuiya ya Kikristo!

Mababa wa Sinodi wanahitimisha hati yao kwa kusema kwamba, waamini katika miito yao mbali mbali wanaitwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, ili kuimarisha na kukuza utakatifu wa Kanisa, kwa kuendelea kuwa waaminifu na wadumifu kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kushuhudia furaha ya Injili hata katika madhulumu na nyanyaso, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kitume ndani ya Kanisa!

Hati ya Sinodi ya Vijana
29 October 2018, 09:38