Tafuta

Mababa wa Sinodi wanaandaa: Hati ya Mwisho wa Sinodi na Barua kwa vijana wote duniani. Mababa wa Sinodi wanaandaa: Hati ya Mwisho wa Sinodi na Barua kwa vijana wote duniani. 

Sinodi ya Maaskofu: Hati ya mwisho na Barua ya Mababa wa Sinodi kwa vijana duniani!

Baba Mtakatifu anasema, Muhtasari huu ni nyenzo muhimu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na kwa nguvu na jeuri ya Injili, vijana wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yanayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” yatakayohitimishwa hapo tarehe 28 Oktoba 2018 yanaendelea kushika kasi, kwa Mababa wa Sinodi sasa kuanza kujadili kwa kina na mapana: Hati ya Sinodi na Barua ya Mababa wa Sinodi kwa Vijana Wote Duniani. Hizi ni nyaraka kuu mbili zinazochota utajiri wake kutoka katika “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya kutendea kazi”.

Baba Mtakatifu Francisko amewazawadia vijana wote wanaoshiriki katika maadhimisho ya Sinodi “Docat” yaani “Kitabu cha Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kuyatangaza na kuyashuhudia katika vipaumbele vya maisha na utume wao! Huu ni muhtasari wa mafundisho Jamii ya Kanisa kutoka kwa Papa Leo XIII “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayofumbatwa katika: Haki msingi, utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hadi katika Mafundisho ya Papa Francisko: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” na “Amoris laetitia” yaani “Furaha katika upendo ndani ya familia”.

Baba Mtakatifu anasema, Muhtasari huu ni nyenzo muhimu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na kwa nguvu na jeuri ya Injili, vijana wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo!

Tume iliyopewa dhamana ya kuhariri “Hati ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana” imefanya kazi kubwa, kwa hamasa kubwa na hivyo kuweza kuiwasilisha kwa wakati. Haya ni matunda ya juhudi za Padre Giacomo Costa na Rossano Sala chini ya usimamizi wa Kardinali Sergio da Rocha, Mwezeshaji mkuu wa Sinodi, waliokuwasanya pamoja utajiri wa mawazo yaliyotolewa katika kipindi cha miaka miwili, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, tayari kumkabidhi Baba Mtakatifu mapendekezo atakayoyafanyia kazi na hatimaye, kutoa Wosia wa Kitume, baada ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018.

Katika kipindi cha maadhimisho ya Sinodi, Kanisa limejenga na kuimarisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya, tayari kujibu matamanio yao halali, yatakayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inachota utajiri wake kutoka katika “Hati ya kutendea kazi”, hotuba elekezi zilizotolewa na wawezeshaji wakuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi, bila kusahau mchango uliotolewa na Mababa wa Sinodi kama watu binafsi na katika taarifa za makundi.

Hati hii  imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Kufahamu, Kutafsiri na Kuchagua, kwa kujikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka. Hati hii anasema Kardinali Sergio da Rocha ni matunda ya ushirikiano na mshikamano wa Mababa wa Sinodi chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Papa Francisko ambaye amejitahidi kuhakikisha kwamba, pale alipopata nafasi, aliweza kushiriki kikamilifu na kuchangia pia mawazo yake.

Mababa wa Sinodi wanawashukuru na kuwapongeza vijana waliochangia kwa kiasi kikubwa kwani hii ni Sinodi ya Vijana kwa ajili pamoja na vijana. Baba Mtakatifu akiridhia Mapendekezo haya, basi, Hati itatolewa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na watu wote wenye mapenzi mema. Waraka huu, utakiwa ni kitendea kazi kwa ajili ya utume wa Kanisa kwa vijana na msaada mkubwa kwa ajili ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana pamoja na kuhamasisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa!

Familia ya Mungu ndio walengwa wakuu, wao ni chanzo na hatima ya kazi nzima iliyotekelezwa na Mababa wa Sinodi katika kipindi chote hiki! Katika tofauti za kitamaduni, mahali wanapotoka na kuishi vijana; hali yao ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kikanisa yamezingatiwa, lakini, utekelezaji na umwilishaji wake, utahitaji ushirikiano wa dhati kutoka katika kanda na hatimaye, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuanza utekelezaji wake kwa kusoma alama za nyakati. Barua ya Mababa wa Sinodi inapania kuwahamasisha vijana kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa ari, upendo na moyo mkuu hayo yaliyopembuliwa na Mababa wa Sinodi katika uhalisia wa maisha yao.

Kardinali Sergio da Rocha anakaza kusema, Sinodi imekuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kufanya hija ya toba na wongofu wa kimisionari; kwa kutafakari kwa kina na mapana changamoto zilizojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, hasa kutokana na kashfa mbali mbali! Vijana wanataka kuliona Kanisa linalojikita katika ukweli na uwazi; Kanisa ambalo ni chombo na shuhuda wa huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Hili ni Kanisa ambalo linajikita katika tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Kristo Yesu, ndiye kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa na kamwe haliwezi kuteteleka, licha ya udhaifu na mapungufu ya watoto wake. Kanisa linaendelea kusonga mbele, likiwa limesheheni imani na matumaini na kwamba, linataka kujikita katika huduma kwa vijana wa kizazi kipya kwa kusadaka: rasilimali watu, muda na fedha katika maisha na utume wa Kanisa. Mchakato wa Sinodi ya kweli ya vijana unaanza rasmi tarehe 29 Oktoba 2018!

Hapa Mababa wa Kanisa watapaswa kujizatiti kikamilifu katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho, ili kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa Kanisa kusimama kidete katika sera na mikakati yake bila kuyumbishwa wala kumezwa na malimwengu! Kamwe lisikubali kutekwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii vyenye malengo tofauti, ili kweli Sinodi iweze kuzaa matunda ya toba na wongofu wa kimisionari, tayari kusikiliza na kujibu matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya!

Sinodi Vijana: Hati
25 October 2018, 09:43