Tafuta

Barua ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 Barua ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 

Barua ya Mababa wa Sinodi kwa vijana wote duniani!

Mababa wa Sinodi kabla ya kufunga maadhimisho haya wamewaandikia vijana wote barua ambayo imesheheni: matumaini, imani na faraja kutoka kwao, ambao wamekuwa na fursa ya kusikiliza sauti ya Kristo Yesu, ambaye ni kijana katika umilele wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yaliyozinduliwa tarehe 3 Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” yamefungwa rasmi, Jumapili tarehe 28 Oktoba 2018 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mababa wa Sinodi kabla ya kufunga maadhimisho haya wamewaandikia vijana wote barua ambayo imesheheni: matumaini, imani na faraja kutoka kwao, ambao wamekuwa na fursa ya kusikiliza sauti ya Kristo Yesu, ambaye ni kijana katika umilele wake. Kwa njia ya Kristo, Mababa wa Sinodi wameweza kusikiliza sauti ya vijana, furaha yao, malalamiko na ukimya wao.

Mababa wa Sinodi wanatambua tafakari za maisha yao ya ndani, furaha na matumaini; shida na mahangaiko yanayowakumba katika safari ya maisha yao hapa duniani. Mababa wa Sinodi wanawataka vijana kuwasikiliza, kwani wanapania kuwa ni washiriki wenza katika furaha ili matamanio yao halali yaweze kumwilishwa katika uhalisia wake. Kanisa ni Mama na mwalimu kwa vijana, kumbe, hawezi kuwatelekeza kamwe, hadi pale matumaini yao yatakapotekelezwa. Mababa wa Sinodi wana uhakika kwamba, vijana wako tayari kujisadaka kwa njia ya maisha yao, ili ndoto ya maisha iweze kumwilishwa katika uhalisia na katika historia ya binadamu!

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, udhaifu, mapungufu yao ya kibinadamu na dhambi zisiwe ni kikwazo kinachofifisha imani. Kanisa ni Mama na kamwe hawezi kuwatelekeza, daima yuko tayari kuwasindikiza katika njia mpya, kwa kuwaongoza na kuwaelekeza mahali ambapo nguvu ya Roho Mtakatifu inataka kuwapeleka kwa kuvunjilia mbali mawingu ya kutojali, ya kufanya mambo kwa juu juu tu pasi na kuzama katika undani wake na hatimaye, hali ya kukata tamaa!

Wakati ambapo Mwenyezi Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu, unaendelea kutopea katika: vitu, mafanikio ya haraka haraka, raha na starehe kwa kutumia migongo ya maskini; vijana wausaidie ulimwengu kuweza kusimama tena na kuinua uso wake katika upendo, uzuri, ukweli na haki. Mababa wa Sinodi wanasema, kwa muda wa mwezi mzima, wametembea na baadhi ya vijana wenzao bila kusahau umati mkubwa wa vijana uliowasindikiza kwa njia ya sala.

Mababa wa Sinodi wanatamani kuendeleza safari hii kila sehemu ya ulimwengu, pale ambapo wanatumwa na Kristo Yesu kama wafuasi wamisionari. Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, unahitaji ari na mwamko wa vijana. Wanawaalika vijana kuwa wanandani wa safari kwa vijana wenzao ambao ni dhaifu, maskini na wale ambao wamejeruhiwa katika maisha. Vijana wawe ni mwanga angavu kwa sasa na kwa siku za usoni!

Barua ya Maaskofu kwa Vijana

 

29 October 2018, 10:01