Vatican News
Papa Francisko amewataka Wascabrini kuwa waaminifu kwa karama yao ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa ari na moyo mkuu. Papa Francisko amewataka Wascabrini kuwa waaminifu kwa karama yao ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa ari na moyo mkuu.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Imarisheni huduma kwa wahamiaji dhidi ya chuki na maamuzi mbele!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka wanashirika hawa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, daima wakijikita katika ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika ukarimu kwa wageni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 29 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Wamisionari wa Mtakatifu Carlo, maarufu kama Wascalabrini, waliokuwa wanaadhimisha mkutano mkuu wa Shirika, ambao umemchagua Mheshimiwa Padre Leonor Chiarello, kuwa Mkuu mpya wa Shirika. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka wanashirika hawa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, daima wakijikita katika ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika ukarimu kwa wageni. Wimbi kubwa la wahamiaji kutoka Honduras kuelekea nchini Marekani ni changamoto kubwa inayohitaji mshikamano na mafungamano, ili kuweza kuwasaidia wakimbizi hawa.

Baba Mtakatifu amewashukuru wamisionari hawa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, watambue wao pia ni wakimbizi mbele ya Mwenyezi Mungu, ambao daima wanaendelea kubisha hodi, ili waweze kufunguliwa malango ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Fumbo la Msalaba, ni kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, changamoto kwa waamini kuwa na ujasiri ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Ameitaka jamii kuwatunza na kuwaenzi wazee ambao ni amana na utajiri wa jamii na wala si watu waliopitwa na wakati!

Baba Mtakatifu katika hotuba aliyokuwa ameandika kwa ajili ya wanashirika hawa amekazia umuhimu wa huduma kwa wahamiaji na wakimbizi kama sehemu ya mchakato wa kupambana na maamuzi mbele, chuki na uhasama dhidi ya watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Mkutano mkuu wa Wascalabrini umeongozwa na kauli mbiu “Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Mfufuka alitumia fursa hii kuwafafanulia wafuasi wake wa Emau, Maandiko Matakatifu, akaandamana nao, changamoto ya kuendelea kuinjilisha kwa kushikamana na familia ya Mungu pamoja na kuwa waaminifu kwa Karama ya shirika inayowataka kuwa ni wahudumu wa wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu amewataka wawe ni mashuhuda wa kinabii kama ilivyokuwa kwa Muasisi wa shirika lao Mtakatifu Carlo, kwa kutambua kwamba, utume kwa wakimbizi na wahamiaji kwa sasa unakabiliwa na changamoto kubwa, hasa maamuzi mbele, sera na mikakati ya kufunga mipaka dhidi ya wakimbizi na wahamiaji; watu ambao wanahitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Kristo. Uinjilishaji uimarishe umoja na mshikamano na watu wa Mungu kwa kuwasikiliza kwa makini: historia, changamato, matatizo na matamanio yao halali.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wenye sura, historia, asili na utambulisho makini, hawa ni rasilimali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mchakato wa uinjilishaji unafumbatwa katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambamo waamini wanapata fursa ya kushiriki Liturujia ya Neno la Mungu: chemchemi ya wokovu, matumaini, uhuru, amani na utulivu wa ndani. Liturujia ya Ekaristi Takatifu inawashirikisha waamini fumbo la upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kuandamana na watu wanaoteseka daima wakijitahidi kumwilisha karama ya Mwenyeheri Giovanni Battista Scalabrini, tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, hasa wale ambao wamejeruhiwa, na kifo kiko daima mbele ya maisha yao. Elimu makini, katekesi na utume kwa familia ni mambo msingi kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Wascalabirini, Ili kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu tete, wanapaswa kushikamana na Kristo anayewapyaisha katika imani, matumaini na mapendo.

Yesu anaendelea kuwa hai katika Neno na Sakramenti zake. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu; Tafakari ya Neno la Mungu na kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi inayofumbata huruma ya Mungu kwa binadamu! Yote haya yamwilishwe katika maisha ya kijumuiya, kielelezo makini cha umoja katika tofauti msingi, kama njia ya kukamilishana na ushuhuda wa furaha ya Injili; amana na utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wawe tayari kuwakaribisha waamini walei ili kushiriki katika karama yao, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mamboleo.

Papa: Scalabrini
30 October 2018, 10:21