Cerca

Vatican News
Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake! Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki, Italia SIR linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake!  (ANSA)

Papa Francisko: utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele katika tasnia ya habari!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. Vicenzo Corrado, Mkurugenzi mkuu wa SIR, amemtaka kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapewa kipaumbele cha kwanza katika utume wao wanaopaswa kuutekeleza kwa kuzingatia: weledi, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR, linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake yaani hapo tarehe 25 Oktoba 1988! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. Vicenzo Corrado, Mkurugenzi mkuu wa SIR, amemtaka kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapewa kipaumbele cha kwanza katika utume wao wanaopaswa kuutekeleza kwa kuzingatia: weledi, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji, kwa kusoma alama za nyakati, ili kujibu changamoto mamboleo na mahitaji ya watu wa Mungu kwa nyakati hizi.

Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ni chombo muhimu sana cha mawasiliano ya jamii, kinachounganisha familia ya Mungu nchini Italia; ni chombo cha umoja na mshikamano wa kikanisa, kijamii na kitamaduni. Baba Mtakatifu analishukuru shirika hili kwa kutoa habari za Vatican, Kanisa na matukio mbali mbali ya kitaifa na kimataifa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2019 itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 2 Juni 2019 inawahamasisha wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuuvua uongo, kusema ukweli kwa maana wao ni viungo, kila mmoja kiungo cha mwenzake. Huu ni mchakato wa kujenga na kudumisha jumuiya inayofumbatwa katika mawasiliano, kwa kukazia ukweli na mafungamano ya kijamii. Katika miaka 30 ya maisha na utume wa Shirika hili kumekuwepo na maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano, lakini daima wamekuwa makini kwa kuzingatia: malengo, nidhamu katika matumizi ya lugha. Hifadhi ya kumbu kumbu pamoja na kutoa kipaumbele cha pekee kwa matukio mbali mbali ya kidini na kikanisa.

Baba Mtakatifu amelitaka shirika hili kuwa makini dhidi ya habari za kughushi “FAKE NEWS”, janga linaloendelea kusambaa kwa kasi miongoni mwa vyombo vya mawasiliano ya jamii. Weledi na ukweli wa mambo ni muhimu sana kuzingatiwa kwa kuhakiki vyanzo vya habari ili kuondokana na tabia ya kuchapisha habari za kughushi ambazo zimekuwa ni chanzo cha mipasuko ya kijamii, badala ya kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu analitaka shirika la SIR kujikita katika upyaisho, ili kuwafikia walengwa wengi zaidi, daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza, bila kuwasahau wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. SIR wawe ni walinzi wa ukweli kama sehemu ya utume wao katika ulimwengu mamboleo!

Mlengwa wa kwanza ni binadamu anayepaswa kuhabarishwa. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kikamilifu kwa kukuza na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kuibua ukweli pamoja na kudumisha ubora wa habari zinazotolewa. Waandishi wa habari wawe ni wajenzi wa madaraja ya majadiliano na maelewano kati ya watu wa Mataifa.

Papa: SIR

 

 

30 October 2018, 10:38