Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, watakatifu wamechangia ustawi, maendeleo na mafao ya nchi zao: kiroho na kimwili. Papa Francisko asema, watakatifu wamechangia ustawi, maendeleo na mafao ya nchi zao: kiroho na kimwili.  (ANSA)

Watakatifu wapya wamechangia ustawi, maendeleo na mafao ya nchi zao: kiroho na kimwili

Papa Francisko ametumia fursa hii kuwasalimia waamini, mahujaji na wawakilishi maalum waliofika kushuhudia tukio hili la kihistoria. Watakatifu hawa wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili mintarafu nchi wanamotoka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili, tarehe 14 Oktoba 2018 mara baada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwatangaza watakatifu wapya saba ambao ni Papa Paulo VI, Askofu mkuu Oscar Romero, Vincenzo Romano, Maria Caterina Kasper, Nazaria Ignazia, Francesco Spinelli na Nunzio Sulprizio ametumia fursa hii kuwasalimia waamini, mahujaji na wawakilishi maalum waliofika kushuhudia tukio hili la kihistoria. Watakatifu hawa wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili mintarafu nchi wanamotoka!

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amemshukuru Malkia Sofia wa Hispania, Rais Sergio Mattarella wa Italia, wengine ni Marais kutoka Chile, El Salvador pamoja na Panama. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Askofu mkuu mstaafu Rowan Williams na ujumbe kutoka kwa Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametoa salam na shukrani kwa waamini, mahujaji na kwa wale wote waliokuwa wanafuatia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Ametambua kwa namna ya pekee Kikundi cha Chama cha Wafanyakazi Nchini Italia ambacho kimekuwa na uhusiano na mafungamano ya pekee na Mtakatifu Paulo VI.

Baba Mtakatifu amekamilisha hotuba yake kwa kusali Sala ya Malaika wa Bwana, ili kumwomba Bikira Maria, mwanafunzi wa kwanza aliyekuwa mkamilifu, ili kwa sala na tunza yake, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufuata mifano ya watakatifu wapya waliotangazwa, Jumapili ya XXVIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, ujumbe kutoka Uganda katika maadhimisho haya umeongozwa na Bwana Edward Ssekambi Kiwanuka, Makamu wa Rais wa Uganda. Kulikuwepo pia ujumbe kutoka Cameroon kwa upande wa Bara la Afrika.

Papa: sala ya Malaika wa Bwana
14 October 2018, 14:51