Tafuta

Catitas Internationalis inaendesha kampeni ya ukarimu na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji duniani! Catitas Internationalis inaendesha kampeni ya ukarimu na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji duniani! 

Papa Francisko: Shirikini safari ili kuondoa chuki na uhasama dhidi ya wakimbizi na wahamiaji

Papa Francisko anasema, kampeni ya kimataifa ya ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi: “Share the journey” yaani “Shiriki safari” ni kielelezo cha dhati kabisa cha kutaka kutembea kwa pamoja, ili kufahamiana na hatimaye, kuondoa chuki na uhasama dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kufanya matembezi ya kilometa milioni moja dhidi ya chuki na uhasama kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi kuliko kule walikotoka. Matembezi haya yanaongozwa na kauli mbiu “Share the journey” yaani “Shiriki safari”. Ni matumaini yanayowabidisha watu wa Mungu kushiriki katika safari hii, ili kukutana na wahamiaji pamoja na wakimbizi! Matumaini ndiyo nguzo inayowasukuma hata kuthubutu kuvuka vikwazo mbali mbali katika safari yao! Bila matumaini ni kazi bure anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 21 Oktoba 2018, amempongeza kwa namna ya pekee, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, Maaskofu, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kwa kushiriki kampeni ya Caritas Internationalis “Share the journey” yaani “Shiriki safari” kama kielelezo cha dhati kabisa cha kutaka kutembea kwa pamoja, ili kufahamiana na hatimaye, kuondoa chuki na uhasama dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.

Hii ni kampeni ambayo tayari imekwisha valiwa njuga na nchi kama: Marekani, Canada, Uingereza, New Zealand na Chile, ili kusaidia mchakato wa mageuzi katika mahusiano na mafungamano ya kijamii kati ya wenyeji, wakimbizi na wahamiaji. Kuna Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kitaifa yanayotekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 160 yanaendesha kampeni hii katika ngazi ya kitaifa na kikanda!

Baba Mtakatifu Francisko, mwezi Septemba 2017 alizindua Kampeni ya Kimataifa ya Ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi inayoratibiwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Huu ni mwaliko na changamoto endelevu kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha wema na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali ya misaada ya Kanisa Katoliki sanjari na vyama vya kiraia vinavyojielekeza katika huduma ya upendo kwa wahamiaji na wakimbizi.

Hii ni kampeni ya umoja na mshikamano na wale wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi pamoja na wenyeji wanaowaendea kwa unyenyekevu, ili waweze kuonja wema na ukarimu wao; kwa kuwaelewa na kuthamini tamaduni, lugha na desturi zao njema. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto changamani kwa wakati huu kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya nchi zinaanza kuweka sera na mikakati ya kufunga mipaka ya nchi zao, kwa kukataa kuwapokea na kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji. Changamoto hii inapaswa kujibiwa kwa moyo wa ukarimu na upendo badala ya kuendekeza uchoyo na ubinafsi, ili kuweza kuleta mageuzi makubwa katika mahusiano na mafungamano ya kijamii na wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Lengo ni kuvunja na kufyekelea mbali mawazo mgando na maamuzi  mbele yanayotishia: maisha, usalama, mshikamano na mafungamano ya kijamii, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali anasema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo, huruma na upole, kwa watu wanaokimbia: vita, umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwatambua kuwa wote ni ndugu wamoja, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, licha ya shida na mahangaiko yao mazito! Wongofu wa ndani ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha upendo na amani.

Itakumbukwa kwamba, kuanzia tarehe 17-24 Juni 2018, Caritas Internationalis iliendesha kampeni hii kwa vitendo. Mwezi Septemba, 2018, Caritas Internationalis ikahamishia mchakato wa uragibishaji wa kampeni hii kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, nchini Marekani, ili kuweza kupitisha miswada miwili ya kimataifa kwa ajili ya ulinzi, usalama na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji duniani. Mwishoni mwa mwaka 2019, Caritas Internationalis itakuwa inahitimisha kampeni hii ya Shiriki safari na wakimbizi pamoja na wahamiaji duniani!

Shiriki safari
22 October 2018, 07:50