Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, Neno la Mungu lina nguvu ya kuleta mageuzi katika maisha ya watu! Papa Francisko asema, Neno la Mungu lina nguvu ya kuleta mageuzi katika maisha ya watu!  (ANSA)

Papa Francisko: tafakari kuhusu nguvu ya Neno la Mungu!

Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu na lina ukali kuwili kuliko upanga ukatao kuwili, tena la choma hata kuzigawanya nafsi na roho. Neno la Mungu li hai tena lina nguvu ambayo imejionesha kwa namna ya pekee katika kazi ya uumbaji. Katika utimilifu wa nyakati, Kristo Yesu amewakirimia waja wake Neno la Mungu ambalo ni roho tena ni uzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Neno la Mungu li hai tena lina nguvu; Neno la Mungu ni tamu kuliko asali kutoka mwambani; lina ukali kuwili kama upanga; ni ukweli na uzima! Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Biblia Marekani, waliomtembelea mjini Vatican, Jumatano, tarehe 31 Oktoba 2018 kabla ya kuanza mafungo yao ya mwaka yanayojikita katika “Nguvu ya Neno la Mungu”.

Baba Mtakatifu amewataka wajumbe, hawa kuendelea kujibidisha ili maisha ya watu wengi yaweze kubadilika kwa chachu ya Neno la Mungu, kwani Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu na lina ukali kuwili kuliko upanga ukatao kuwili, tena la choma hata kuzigawanya nafsi na roho. Neno la Mungu li hai tena lina nguvu ambayo imejionesha kwa namna ya pekee katika kazi ya uumbaji. Katika utimilifu wa nyakati, Kristo Yesu amewakirimia waja wake Neno la Mungu ambalo ni roho tena ni uzima. Kwa njia ya Neno lake, Kristo Yesu aliweza kupyaisha maisha ya watu kama Zakayo na Mathayo watoza ushuru, walioacha yote wakaamua kumfuasa Kristo!

Nguvu ya Neno la Mungu inatenda kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka katika maisha ya waja wake. Baba Mtakatifu anawaalika wakristo kuhakikisha kwamba, wanalitafakari Neno la Mungu katika umoja wake, yaani Agano la Kale linalopata utimilifu wake kwenye Agano Jipya. Neno la Mungu ni nguvu ya Roho Mtakatifu, mleta uzima anayepyaisha maisha ya waja wake ili yaweze kuwa na tija! Hakuna kitabu chochote chenye nguvu zaidi kwani, kwa njia ya Neno la Mungu, waamini wanaweza kumfahamu Roho Mtakatifu mleta uzima. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu, Neno la Mungu linaweza kupokelewa, kumwilishwa, kutangazwa na kushuhudiwa, kwani Roho Mtakatifu anafundisha na kuwakumbusha yote ambayo Kristo alinena na kutenda!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Neno la Mungu ni tamu kuliko asali kutoka mwambani; lina ukali kuwili kama upanga. Neno la Mungu linazama katika undani wa mtu kiasi hata cha kumsaidia kuondoa giza moyoni mwake: Neno la Mungu linatakasa na kuondoa mambo ambayo yanawasababisha waamini kuwa mbali na Mwenyezi Mungu pamoja na upendo wake! Neno la Mungu ni faraja, linaganga na kuponya, linamwezesha Mwenyezi Mungu kuwachunguza na kuwajua waja wake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Neno la Mungu ni ukweli na uzima, linasafisha na kuondoa uwongo na maisha ya undumilakuwili! Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha yanayomwelekea Mwenyezi Mungu. Maandiko Matakatifu yanayosomwa na kutafakariwa kwa ari na moyo mkuu, yanawawezesha waamini kwa wakati wao kuwa ni “Vitabu wazi” vya maisha ya watu wanaomwilisha Neno la Mungu linalo okoa na mashuhuda wa Kristo Yesu anayewakirimia upya wa maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, baada ya Mafungo ya Mwaka, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Biblia Marekani watakuwa na ari na nguvu mpya katika kutekeleza utume wao, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Amewaomba wajumbe hawa kuendelea kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Chama cha Biblia USA
31 October 2018, 15:01