Tafuta

Mtakatifu Oscar Romero alikuwa ni shuhuda, nabii na mtetezi wa maskini nchini El Salvador Mtakatifu Oscar Romero alikuwa ni shuhuda, nabii na mtetezi wa maskini nchini El Salvador 

Mt. Oscar Romero ni shuhuda wa Injili, chombo cha upatanisho na mtetezi wa maskini!

El Salvador ni nchi ambayo imetikishwa sana kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, Mtakatifu Oscar Armulfo Romero awe sasa ni chachu ya umoja na upatanisho wa kitaifa, tayari kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Oscar Armulfo Romero ni shuhuda wa Injili ya Kristo anayewakumbusha wakristo kwamba wanapaswa kuwa ni wafiadini, yaani mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia ujumbe wa ukombozi, unaowaweka wote huru kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Mtakatifu Oscar Romero ni mfano wa mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huu ni mwaliko wa kupambana na ubaya wa dhambi, ili kweli ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. El Salvador ni nchi ambayo imetikishwa kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, Mtakatifu Oscar Armulfo Romero awe sasa ni chachu ya umoja na upatanisho wa kitaifa, tayari kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa watu wa Mungu.

Kwa ufupi, huu ndio ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 15 Oktoba 2018 alipokutana na kuzungumza na mahujaji kutoka El Salvador, waliomiminika kwa wingi mjini Vatican, ili kushuhudia Askofu mkuu Oscar Armulfo Romero pamoja na wenzake wakitangazwa kuwa watakatifu, kwenye Ibada iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 14 Oktoba 2018 na kama kielelezo cha uwepo wao wa karibu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Oscar Romero ni kiongozi aliyefanikiwa sana kumwilisha ile sura na chapa ya Mchungaji mwema katika maisha na utume wake. Akahubiri na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto na mwaliko kwa wakristo kuwa ni wafiadini, yaani mashuhuda wa Kristo Mfufuka! Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Oscar Romero, mtetezi wa maskini, aliuwawa kikatili kunako tarehe 24 Machi 1980 wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, changamoto kwa familia ya Mungu Amerika ya Kusini kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anawaita na kuwatuma waja wake kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; kwa kung’oa kutoka katika sakafu ya nyoyo ndago za chuki na uhasama, ili kuanza kujikita katika mchakato wa kupenda pasi na mipaka. Huu ni uhuru wa kweli unaozingatia maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kuchochea tena matumaini ya wokovu katika nyoyo za watu! Mtakatifu Oscar Romero ni kielelezo na mfano bora wa mchungaji mwema na mfano wa kuigwa na Maaskofu wa El Salvador, ili kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini, amana na utajiri wa Kanisa.

Huu ni mwaliko wa kupambana na ubaya wa dhambi, kwa kuhakikisha kwamba, wakleri wanakuwa kweli ni vyombo vya huduma ya huruma ya Mungu, kwa wale wote wanaotaka kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao. Mtakatifu Oscar Romero alikuwa ni nabii na shuhuda wa huruma ya Mungu, mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuambata utakatifu katika maisha na utume wao na kamwe wasiwe ni vikwazo kwa watu wa Mungu.

El Salvador ni nchi ambayo katika historia yake, imepekenywa sana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kiasi cha kuwafanya baadhi ya wananchi wake kukimbia ili kutafuta usalama wa maisha na mali zao. Mtakatifu Oscar Romero awe ni chachu ya toba, wongofu wa ndani, umoja na mshikamano wa dhati kwa familia ya Mungu Amerika ya Kusini. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa na kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Kipaimara ni “Sakramenti ya ushuhuda”. Baba Mtakatifu anaiombea familia ya Mungu nchini El Salvador ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kwa maombezi ya Mtakatifu Oscar Romero, waamini wachangamotishwe kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Papa: El Salvador
16 October 2018, 14:30