Papa Francisko anasali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali nchini Jordan Papa Francisko anasali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali nchini Jordan 

Telegram ya Papa Francisko kwa wathirika wa mafuriko nchini Jordan

Katika Telegram iliyotumwa kwa Askofu mkuu Alberto Ortega Martín, Balozi wa Kitume nchini, Baba Mtakatifu anaelezea kwa masikitiko makubwa na mshikamano wake,kwa ajili ya wote walioathirika na janga la Asili nchini Jordan na wengi wao wakiwa ni watoto wa shule

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Telegram ya Papa Francisko, iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican  imetumwa kwa  Balozi wa Kitume nchi Giordania Askofu mkuu Alberto Ortega Martín kufutia na janga la mafuriko makubwa yaliyotokea nchini Jordan. Katika Telegram, Baba Mtakatifu anaonesha masikitiko makubwa kuhusu janga lililotokea ambalo limesababisha kupoteza maisha kwa vijana, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali nchini Jordan.

Baba Mtakatifu anaelezea mshikamano wake kwa moyo wote, walioathirika na janga hilo la asili. Kwa namna ya pekee sala zake ziwaendee hasa vijana na wote waliopoteza maisha yao, waliojeruhiwa wapone haraka na kupata faraja wote wanaoomboleza kwa ajili ya wapendwa wao. Na katika maombi yake kwa ajili yao, pia anawatia moyo viongozi wa raia na wale wanaojihusisha katika harakati za uokoaji. Kwa wote anawatakia Baraka za Mungu na zawadi ya nguvu na amani.

Kuhusiana na tukio hilo

Idadi kamili ya watu waliokufa bado haijajulikana lakini wengi wao ni watoto wa shule  kwani katika taarifa kutoka vyombo mahalia vinasema kuwa, watu wasiopungua 18 wengi wao wakiwa ni watoto wa shule na walimu wameaga dunia katika mafuriko ya ghafla wakati walipokuwa katika matembezi ya kishule karibu na Bahari ya Chumvi  nchini Jordan. Mafuriko hayo yametajwa kuwa ni maafa makubwa zaidi kuwahi kuikumba Jordan katika miaka ya karibuni.

Mkuu wa polisi ya Jordan, Brigedia Jenerali Farid al Sharaa ameiambia televisheni ya nchi hiyo kuwa, watu 34 wameokolewa katika oparesheni kubwa iliyohusisha helikopta za polisi na askari jeshi. Baadhi ya watu walionusuriwa katika mafuriko hayo wana hali mbaya na wengi walioaga dunia ni watoto wenye umri wa  chini ya miaka 14. Na msemaji wa ulinzi wa raia Kapteni Iyad al Omar amesema kuwa idadi ya waliopoteza maisha huwenda ikaongezeka.

Sababu za mafuriko ya ghafla

Mafuriko hayo ya ghafla yametokea  Jordan baada ya mvua kali zilizonyesha nchini humo baada ya kumalizika msimu wa joto. Wakati huo huo Omar Razzaz Waziri Mkuu wa Jordan amesema kuwa inaonekana kuwa shule hiyo ilikiuka miongozo ya Wizara ya Elimu inayozuia safari katika eneo la Bahari ya Chumvi kutokana na hali mbaya ya hewa. Ameahidi kufanyika uchunguzi ambao utawafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wote watakaopatikana na makosa.

                                                          

 

 

 

 

 

 

27 October 2018, 12:32