Cerca

Vatican News
Amri ya Mungu: Usizini! Maana yake: Uaminifu, ukarimu na huruma! Amri ya Mungu: Usizini! Maana yake: Uaminifu, ukarimu na huruma!  (Vatican Media )

Amri ya Mungu inasema: Usizini: Maana yake: dumisha: uaminifu, ukarimu na huruma!

Usizini! Hiki ni kielelezo makini cha uaminifu kwa Kristo Yesu kinachofumbata mwanga wa uzuri na upendo wa kibinadamu, mwaliko wa kuchuchumilia wito wa upendo unaojifunua katika misingi ya: uaminifu, ukarimu na huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amri ya Sita inasema “Usizini”. Hiki ni kielelezo makini cha uaminifu kwa Kristo Yesu kinachofumbata mwanga wa uzuri na upendo wa kibinadamu, mwaliko wa kuchuchumilia wito wa upendo unaojifunua katika misingi ya: uaminifu, ukarimu na huruma! Hii ni Amri ambayo inawahusu kwa namna ya pekee kabisa watu wa ndoa na familia, kumbe inapaswa kutafakariwa kwa kuzingatia wito huu! Mtakatifu Paulo mtume, anaonesha mageuzi makubwa katika uelewa wa upendo, huku akikazia upendo wa dhati kati ya wanandoa, kama Kristo Yesu alivyolipenda Kanisa lake!

Ufafanuzi huu umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 31 Oktoba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Amri ya Sita “Usizini” ni mwaliko kwa watu wote, kwani hili ni Neno la Mungu lenye uzima linaloelekezwa kwa watu wote, kama kielelezo cha ukomavu wa upendo wa kibinadamu unaopaswa kupaliliwa, ili hatimaye, uweze kujitoa bila ya kujibakiza, tayari kupokea zawadi ya uhai na kurithisha uhai huu kwa wengine!

Kuwa watu wazima maana yake ni kuwajibika barabara, kama watu wa ndoa, wazazi na walezi, mambo yanayojifunua katika hatua mbali mbali za maisha, kwa kusaidia wengine kubeba mizigo yao na kupenda bila kujibakiza! Huu ni mwelekeo unaomwilisha uhalisia wa maisha na kuanza kujikita katika mahusiano na mafungamano ya dhati na watu wengine! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, uasherati, uzinzi na ukahaba ni misiba ya kijamii inayoonesha dalili za mtu kutokuwa mkomavu katika mahusiano, kiasi cha kumgeuza mtu mwingine kuwa kama chombo cha biashara na kutimizia anasa zake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kufunga ndoa, bali kuna haja ya kwenda mbele zaidi kama sehemu ya hija ya mchakato wa ukomavu wa mtu, kutoka katika ubinafsi na kuanza kujikita katika umoja na utakatifu wa maisha ya ndoa yanayowapatia waamini nafasi ya kusaidiana na kukamilishana, kila mmoja akiwajibika kwa mwenzi wake! Huu ndio ukomavu unaowajibisha! Kumbe, Ndoa ni sehemu ya wito wa Kikristo!

Upadre ni wito wa Kristo ndani ya Kanisa kwa ajili ya huduma kwa jumuiya, dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa kwa upendo, uaminifu na hekima kadiri wanavyojaliwa na Kristo Yesu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linawahitaji Mapadre watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, na wala si watu wanaotaka kufanya majaribio ya wito wa Upadre, watu wa namna hiyo, ni vyema wakabaki majumbani mwao. Mapadre wanapaswa kupenda, kwani wamewekwa wakfu na Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

Mapadre wapende na kuwajibika, kama wanavyopaswa pia watawa na wale wote wanaowekwa wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Changamoto kubwa ni kuwa waaminifu na kutekeleza nyajibu zao kwa furaha na moyo mkuu, daima wakijitahidi kuwa na mahusiano mema yanayoonesha ubaba na umama wao! Kila wito ndani ya Kanisa unawawajibisha wahusika kwa sababu ni matunda ya uhusiano wa upendo na Kristo Yesu kama anavyokazia Mtakatifu Paulo katika Nyaraka zake. Wito hauna budi kujikita katika: uaminifu, upole, ukarimu na imani; mambo yanayopaswa kushuhudiwa katika maisha ya ndoa na familia na hata katika wito wa kipadre na kitawa kama ushuhuda wa ukamilifu wa upendo!

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, mwanadamu ameumbwa mwili na roho; mwanaume na mwanamke, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; katika uzuri na utakatifu wao, ni watu wanaopenda na kupendwa. Mwili wa mwanadamu si chombo cha kutosheleza tamaa za kimwili, bali ni mahali patakatifu panapoweza kumwilisha upendo wa kweli unaozama katika undani wa maisha ya watu. Usiue ni Amri ya Mungu inayowaelekeza watu kuwa na upendo mkamilifu unaofumbatwa katika uaminifu kama ulivyofunuliwa na kutolewa sadaka na Kristo Yesu!

Amri ya Mungu: Usizini

 

 

31 October 2018, 14:25