Tafuta

Papa Francisko asema, "Usiue" maana yake ni kupenda, kusamehe na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Papa Francisko asema, "Usiue" maana yake ni kupenda, kusamehe na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! 

Papa Francisko: Usiue maana yake ni: kupenda, kusamahe na kuenzi uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Amri ya tano inasema “Usiue”, kwa kukazia heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu. Hakuna mazingira yoyote yanayoweza kujwitalia haki ya kuharibu, kubeza au kufisha uhai wa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maisha ya binadamu ni kito cha thamani na kitakatifu kwa sababu tangu mwanzo wake yanahusiana na tendo la Mungu muumbaji na daima yanabaki na uhusiano wa pekee na Muumba aliye peke yake hatima ya uhai wa mwanadamu. Ndiyo maana Amri ya tano inasema “Usiue”, kwa kukazia heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu. Hakuna mazingira yoyote yanayoweza kujwitalia haki ya kuharibu, kubeza au kufisha uhai wa binadamu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ya mwanadamu yanafumbata sura na upendo wa Mungu bila kujali hali na mazingira anamoishi mtu! Kristo Yesu katika mafundisho yake anawataka wafuasi wake kudumisha upendo kati yao, ndiyo maana Mtume Yohane anakaza kusema, kila amchukiane ndugu yake ni mwuaji. Kristo Yesu anaendelea kufafanua kwamba hata yule anayemtukana, kumlaani na kumbeza ndugu yake ni mwuaji wa utu na heshima ya binadamu. Mafundisho haya ya Yesu yanapaswa kuingia na kugota katika akili na nyoyo za watu, ili kila mtu aweze kujizuia kuwatukana, kuwalaani na kuwabeza watu wengine!

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Oktoba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa waamini, mahujaji na wageni kutoka ndani na nje ya Italia. Amri hii ni muhtasari wa kanuni maadili na utu wema. Yesu anawaalika waja wake kujipatanisha na ndugu zao, kabla ya kujongea Altareni kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka na wao wenyewe kukutakatifuzwa.

Huu ndio mwelekeo wanaopaswa kuwa nao waamini wanapokwenda kushiriki katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, yaani kujipatanisha na wale wote ambao wamekoseana nao, ili kweli sadaka yao, iweze kumpendeza Mwenyezi Mungu nao wenyewe kutakatifuzwa. Upatanisho huu unaweza kutokana na kukosana hata kwa mawazo, maneno na kwa kutotimiza wajibu. Mambo yote haya, Yesu anayafananisha ni mauaji si tu ya kimwili, bali mauaji yanayoharibu utu na heshima ya ndugu zao. Yesu anapenda kukazia umuhimu wa zawadi ya maisha kwa kila binadamu bila kuangalia makando kando yake.

Waamini wajifunze kuwa watu wema na wakarimu kwa jirani zao, kwa kutoa faraja kwa watoto, kutowakwaza wanawake kwa ubaridi wa moyo sanjari na kuwanyima vijana matumaini! Kupenda kwa dhati ni hatua moja ya kulinda na kudumisha uhai wa binadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Katika Maandiko Matakatifu sentesi ya mauaji inasikika kutoka kwa Kaini kuhusu mauaji ya ndugu yake Abel, kwa kukana kwamba, yeye si mlinzi wa ndugu yake! Kila mtu anao wajibu na dhamana ya kuwa ni mlinzi wa maisha ya ndugu yake, changamoto ya kulinda uhai, unaopaswa kufumbatwa katika upendo.

Kristo Yesu ameonesha huruma, upendo na msamaha na kwamba, hizi ni tunu msingi katika maisha ya mwanadamu. Mauaji yanahusisha kuondoa uhai wa mtu pamoja na kudhalilisha utu na heshima yake. Kupenda maana yake ni kuhudumia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kumjali na kumthamini mtu jinsi alivyo, tayari hata kumsamehe pale ambapo ametekeleza na kuanguka dhambini.

Kila mtu anahamasishwa kutenda mema, kupenda bila ya kujibakiza, kusamehe na kusahau, kielelezo makini kilichotolewa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Kila mwamini ajitahidi kutenda mema na kuachana na ubaya katika maisha kama alivyofanya Kristo Yesu, Mkuu wa uzima ambaye Mungu amemfufua kutoka kwa wafu. Kristo ni kielelezo cha upendo mkubwa unaopita kifo na kwa njia ya nguvu ya Roho Mtakatifu, anawakirimia waja wake uwezo wa kupokea lile Neno “Usiue”, maana yake, wakumbatie upendo na msamaha!

Papa Katekesi: Kifo
17 October 2018, 13:39