Papa Francisko amemteua Kardinali Njue kumwakilisha katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania. Papa Francisko amemteua Kardinali Njue kumwakilisha katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania. 

Papa Francisko amemteua Kardinali Njue kumwakilisha kwenye Jubilei, Tanzania

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema, tarehe 2 Novemba, ni siku ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wote na kwa namna ya pekee, wamisionari waliosadaka maisha yao kwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania na matunda ya kazi zao yanaonekana bayana katika medani mbali mbali za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, kuwa mwakilishi wake maalum katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 nchini Tanzania, yanayoongozwa na kauli mbiu: “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, furaha ya Injili. Kilele cha maadhimisho haya ni kuanzia tarehe 2-4 Novemba 2018.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, tarehe 2 Novemba, ni siku ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wote na kwa namna ya pekee, wamisionari waliosadaka maisha yao kwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania na matunda ya kazi zao yanaonekana bayana katika medani mbali mbali za maisha! Ibada hii ya Misa itaadhimishwa mjini Bagamoyo, Mlango wa Imani kwa Kanisa Afrika Mashariki, kama alivyofafanua hivi karibuni Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, alipokuwa anagusia chimbuko la Kanisa Katoliki Afrika Mashariki.

Askofu Kassala anakaza kusema, tarehe 3 Novemba 2018, itakuwa ni siku ya Ibada ya toba na wongofu wa ndani kwa kutambua kwamba, Jubilei ni wakati muafaka wa: kumshukuru Mungu kwa neema na baraka zake; ni muda wa kuomba toba na msamaha kutokana na mapungufu ya kibinadamu na hatimaye, kuomba tena baraka na neema, ili kuweza kukabiliana na changamoto za mbeleni kwa imani, matumaini na mapendo! Ni siku ya makongamano, ili kuangalia fursa, changamoto na matarajio ya watu wa Mungu nchini Tanzania kwa siku za usoni! Makongamano haya yataongozwa na Waraka wa Mtakatifu Paulo VI aliyetangazwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa kitume “Africae Terrarum” yaani “Bara la Afrika” uliochapishwa kunako tarehe 29 Oktoba 1967, anakazia pamoja na mambo mengine: Utajiri, amana na urithi mkubwa wa Mapokeo kutoka Barani Afrika sanjari na mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mtakatifu Paulo VI, alikazia umoja na mshikamano kama chachu msingi ya maendeleo endelevu na fungamani, kwa kutambua kwamba, Bara la Afrika lilikuwa limebarikiwa kuwa na tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiroho, kiutu na kijamii; tunu ambazo zinapaswa kuendelezwa ili kupambana na ubaguzi, ukabila, udini, vita na misigano, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani, haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kufutilia mbali maadui wakuu wa Afrika ambao ni ujinga, umaskini na magonjwa!

Mtakatifu Paulo VI alionesha pia matumaini ya Bara la Afrika wakati ambapo nchi nyingi zilikuwa zinajipatia uhuru wake; vikwazo na vizingiti ambavyo vilikuwa mbele yao na kwamba, maendeleo na msaada wa hali na mali ni mambo msingi katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwataka Wakleri na watawa kujikita zaidi katika utamadunisho na huduma makini kwa watu wa Mungu, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kwa viongozi wa Serikali, alikazia umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, demokrasia ya kweli na uhuru na kwamba, wanazuoni na wasomi, wasadake maisha yao kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika. Alizitaka familia kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu, bila kusahau kuheshimu, kulinda na kudumisha haki, utu na heshima ya wanawake wa Bara la Afrika.

Askofu Kassala anakaza kusema, Kanisa nchini Tanzania linataka kuangalia jinsi ya kuumwilisha Waraka huu katika maisha na utume wake, kama njia ya kumuenzi Mtakatifu Paulo VI aliyechangia sana: maendeleo na ustawi wa familia ya Mungu Barani Afrika. Umefika wakati wa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari ndani na nje ya Tanzania; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo makini ya mihimili ya uinjilishaji, ili isaidie kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Huu ni mchakato wa kulitegemeza Kanisa la Tanzania, kwa kuhakikisha kwamba, linatumia kikamilifu rasilimali watu, fedha na vitu katika uinjilishaji kwani Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Ni wakati kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kushuhudia furaha na ukarimu unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo!

Papa: Jubilei Tanzania

 

23 October 2018, 11:57