Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Kardinali Wuerl kung'atuka kutoka madarakani lakini ataendelea kuwa Msimamizi wa Kitume, Jimbo kuu la Washington, USA. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Kardinali Wuerl kung'atuka kutoka madarakani lakini ataendelea kuwa Msimamizi wa Kitume, Jimbo kuu la Washington, USA.  (ANSA)

Papa Francisko ampongeza Kardinali Wuerl kwa maisha na utume wake ndani ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi amekubali ombi lake na kung’atuka kutoka madarakani, lakini anamwomba aendelee kuwa ni Msimamizi wa Kitume, Jimbo kuu la Washington, hadi pale, kiongozi mkuu atakapoteuliwa tena.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Donald William Wuerl wa Jimbo kuu la Washington, Marekani la kung’atuka kutoka madarakani kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amemwandikia barua ya shukrani Kardinali Wuerl aliyekita maisha na utume wake wa Kikuhani kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, akajibidisha kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu aliokuwa amekabidhiwa kwake na Mama Kanisa. Huyu ni kiongozi na mchungaji mkuu aliyekuwa na jicho la umoja, upendo na mshikamano wa watu Mungu, karama ambazo Kardinali Wuerl amebahatika kukirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kwa hakika Kardinali Donald William Wuerl amelipa gharama kubwa kuhakikisha kwamba, umoja wa watu wa Mungu unalindwa na kudumishwa na kwamba, watu hawa wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili, ili wote wawe wamoja ili ulimwengu upate kusadiki kwamba, kweli Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliyetumwa ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ndio mwelekeo na dira ambayo viongozi wa Kanisa wanapaswa kuivalia njuga katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anampongeza Kardinali Wuerl kwa kuwa na upeo mpana zaidi uliomwezesha kuangalia mafao, ustawi na maendeleo ya watu wengi zaidi. Ni kiongozi aliyekita maisha yake, ili kuhakikisha kwamba, umoja wa Kanisa unalindwa na kudumishwa na wote na kwamba, utume na maisha ya Kanisa yalipaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Alisimamia ukweli ili Kondoo wake, “wasitokomee” mahali pasipojulikana. Kwa hakika alionesha sifa na karama za kiongozi bora kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ukuaji wa watu wa Mungu na kamwe hakusita kuchukua hatua madhubuti kwa kuogopa eti ataweza kukosea. Kwa mwelekeo huu, Mpango wa Mungu kwa ajili ya waja wake, ukapewa msukumo wa pekee, kwa ajili ya ustawi wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza kwa kutoka kifua mbele, kutangaza nia ya kung’atuka kutoka madarakani, kielelezo makini cha uwajibikaji na unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu anayeendelea kuliongoza Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi amekubali ombi lake na kung’atuka kutoka madarakani, lakini anamwomba aendelee kuwa ni Msimamizi wa Kitume, Jimbo kuu la Washington, hadi pale, kiongozi mkuu atakapoteuliwa tena. Anamwomba Kardinali Donald William Wuerl kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu na kwamba, thawabu yake ni kubwa zaidi. Mwishoni, anamwombea ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na nguvu ya Roho Mtakatifu ili aendelee kulitumikia Kanisa katika kipindi hiki kipya cha maisha na utume wake ndani ya Kanisa.

Jimbo kuu la Washington

 

13 October 2018, 10:58