Papa Francisko asema, mapambano ya baa la njaa yatekelezwe kwa vitendo zaidi! Papa Francisko asema, mapambano ya baa la njaa yatekelezwe kwa vitendo zaidi! 

Papa Francisko: Baa la njaa duniani lishughulikiwe kwa vitendo zaidi, maskini wanateseka!

Ni wakati wa kuwekeza katika mchakato wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya silaha duniani pamoja na vita vinakoma, kwani vita ni mama wa majanga makubwa ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu zinazotolewa na Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, kuna ongezeko kubwa la watu wanaoendelea kupekenywa na baa la njaa duniani, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, umoja, upendo na mshikamano katika mapambano dhidi ya baa la njaa unazidi kumong’onyoka kila kukicha. Umefika wakati wa kutekeleza kwa vitendo sera na mikakati inayopania kufutilia mbali baa la njaa na umaskini duniani badala ya kuendelea kuendekeza mtindo wa sasa wa kufanya mikutano na makongamano yasiyokuwa na tija katika mchakato wa mapambano ya baa la njaa na umaskini duniani!

Ni wakati wa kuwekeza katika mchakato wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya silaha duniani pamoja na vita vinakoma, kwani vita ni mama wa majanga makubwa ya binadamu! Kwa muhtasari huu ndio ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Professa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, tarehe 16 Oktoba 2018.

Baa la njaa linaongezeka duniani, lakini upendo na mshikamano kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa unaendelea kumong’onyoka kila kukicha anasema Baba Mtakatifu kwa masikitiko makubwa. Watu wasukumwe na dhamiri nyofu ili kupambana na baa la njaa duniani kwa kuwapatia mamilioni ya watu matumaini ya kuwa na uhakika wa chakula cha kila siku. Ni wakati wa kuthubutu kugeuza mateso na mahangaiko ya watu kwa kuongeza maradufu jitihada za kuzalisha chakula, kwa kukazia wingi na ubora, ili kamwe asiwepo mtu anayefariki dunia kutokana na baa la njaa duniani!

Baba Mtakatifu anasema, inawezekana kabisa kulipatia kisogo baa la njaa ifikapo mwaka 2030, ikiwa kama Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 yatatekelezwa kwa vitendo. Maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanasubiri kwa vitendo matokeo makubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, ukuaji wa miundo mbinu mambo yanayopaswa kwenda sanjari na mshikamano wa kimataifa, ili watu wote waweze kupata mahitaji yao msingi.

Kumbe, sera za maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimataifa ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza rasilimali fedha katika sekta ya kilimo, kuondoa vikwazo vya masoko, lakini zaidi kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na utunzaji bora wa mazingira ili kuweza kukabiliana vyema na changamoto ya athari za mabadiliko ya tabianchi; myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na kusitisha vita inayoendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa umaskini na maafa makubwa katika maisha ya binadamu! Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 yanayopania kuhakikisha kwamba: baa la njaa linafutika, kwa kuboresha uhakika wa usalama wa chakula duniani pamoja na kuendelea kujikita katika mchakato wa kilimo endelevu. Hakuna tena muda wa kupoteza, bali Jumuiya ya Kimataifa ishikamane ili kuhakikisha kwamba, malengo yaliyowekwa yanafikiwa, kwani changamoto ya baa la njaa duniani ni changamani na inapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa ipambane na baa la njaa kwa kuzishirikisha taasisi  mbali mbali ambazo zitasaidia kuleta mabaoresho katika jamii kwa kukuza na kudumisha uchumi, ili maskini kamwe wasijisikie kwamba, wametelekezwa. Kinachohitajika hapa ni utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kilimo endelevu inayofumbatwa katika mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaozingatia mahitaji msingi ya watu mahalia. Hapa kuna haja ya kujiondoa kutoka katika maneno na kuanza kutekeleza sera hizi kwa vitendo, kwa kujenga na kudumisha usawa na ugawaji mzuri wa raslimali za dunia. Vita, kinzani na migogoro katika medani mbali mbali za maisha zinakwamisha mchakato wa mapambano ya baa la njaa duniani

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kufutilia mbali baa la njaa duniani, wananchi wanapaswa kuhusishwa kikamilifu, vyombo vya habari na taasisi za elimu ziunganishe nguvu, ili kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya mapambano dhidi ya baa la njaa inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Umoja na mshikamano, haki na amani ni silaha madhubuti ya mapambano ya baa la njaa na athari zake kwa maisha ya binadamu.

Hii ni tafakari ambayo Baba Mtakatifu amependa kumshirikisha Professa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2018. Ni mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutokana na baa la njaa! Kanisa kama sehemu ya mkakati wake wa uinjilishaji, litaendelea kupambana na baa la njaa na utapiamlo; kwa kujenga na kudumisha udugu na haki msingi za binadamu; mambo yanayopaswa kumwilisha katika uhalisia wake!

Papa: FAO 2018
17 October 2018, 09:36