Tafuta

Mkutano wa Papa Francisko na mahujaji kutoka Poland Mkutano wa Papa Francisko na mahujaji kutoka Poland 

Papa Francisko amekutana na mahujaji wa Jimbo Kuu la Krakow

Papa Francisko, katika hotuba kwa mahujaji wa Jimbo Kuu la Krakow amesema, Mtakatifu Yohane Paulo II alitajirisha Kanisa la ulimwengu kwa zawadi kubwa ambazo katika sehemu kubwa imerithiwa kama tunu ya imani na utakatifu wa nchi yao na Kanisa lao

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Baba Mtakatifu Francisko, kabla ya Katekesi yake, amekutana na mahujaji wote kutoka katika Jimbo la nchini Krakow, Poland mjini Vatican, tarehe 10 Oktoba 2018 na kumshukuru Askofu Mkuu Marek kwa hotuba yake, pia kuwasalimia hata Kardinali Sanslaus na Maaskofu waliokuwapo katika mkutano wao. Papa ameelezea kuwa, wao wamefika Roma kama wawakilishi wa Kanisa Takatifu la Mungu ambalo ni Krakow, na ambao amesema, walimkaribisha kwa mikono wazi, katika kiangazi cha mwaka 2016. Wamefika na wachungaji wao na watu walio wekwa wakfu ili kumshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II wakati anakaribia kuadhimisha miaka 40 tangu alipochaguliwa kuwa katika kiti cha Mtakatifu Petro. Anasalimia wote kwa namna ya pekee maskini, wagonjwa na idadi kubwa ya vijana ambao wameshiriki hija hiyo.

Maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II

Baba Mtakatifu Francisko, akiendelea na hotuba amesema, Mtakatifu Yohane Paulo II alitajirisha Kanisa la ulimwengu kwa zawadi kubwa  ambazo katika sehemu kubwa imerithiwa kama tunu ya imani na utakatifu wa nchi yao na Kanisa lao. Yeye alikuwa anachukua ndani ya moyo wake, kwa namna ya kusema, mwili wa ushuhuda wa watakatifu wa Cracow, kuanzia kwa Mtakatifu  Stanislaus, Mtakatifu malkia Edvige, Mtakatifu Alberto na Mtakatifu Faustina. Kutoka kwao, alijifunza kujitoa kwa Kristo Mungu na umakini mkubwa kwa kila mtu; kujikita kwa kina katika umakini wa kuonesha huduma yake ya kipadre, kiaskofu hadi Papa.

Mtakatifu Yohane Paulo II, alipokea kutoka kwa Mungu zawadi kuwa ya kutambua na usoma alama za nyakati kwa njia ya mwanga wa Injili na kutoa matunda hayo kwa ajili ya faida ya watu wote lakini zaidi watu wao, ambao katika matukio ya uchungu wa kihistoria hawakukosa kamwe kuwa na  matumaini kwa Mungu na imani binafsi katika utamaduni ambao umechimba mizizi katika roho ya kikristo. Akiwa mwaminifu katika mizizi hiyo Mtakatifu Yohane Paulo II, alitafuta kwa njia zote kufanya Kanisa liwe kama mlinzi wa haki za binadamu, za familia na watu wote, ili kuwa ishara ya amani, haki na maendeleo fungani kwa ajili ya familia nzima ya kibinadamu. Wakati huo huo, Yeye alitoa kipaumbele cha neema na utii kwa mapenzi ya Mungu kuliko hesabu za kibinadamu.

Utajiri wa kurithi wa Mtakatifu Yohane Paulo II

Utajiri wa kurithi ambao Mtakatifu Yohane Paulo II alituachia , kwa namna ya pekee raia wa Poland, ni changamoto ya kuwa waaminifu wa Kristo na kujibu kwa furaha hasa  kujikita katika suala la kuitwa kwenye utakatifu, ambao Bwana anaawalika kila mmoja na kila hali  binafsi kama familia na kijamii. Kwa maana hiyo Papa Francisko amehitimisha kwamba:  Mtakatifu Yohane Paulo II aachi kamwe kusimamia Kanisa  lake ambalo ni la Kracow na kwake  yeye binafsi alilipenda sana. Kutoka mbinguni Baba Mtakatifu ameongeza, awasindikize katika safari yao. Familia, vijana, bibi na babu, mapadre, watawa wote kike na kiume; wasio na fursa, na wanaoteseka. Na kwa njia hiyo Papa pia, amewakabidhi maombi yao. Anawashukuaru ziara yao ya kumtembelea na kuwabariki Jumuiya nzima ya Jimbo Kuu la Kracow. Lakini pia wasisahau kusali kwa ajili ya Papa. Na kabla ya kuwabariki, wamesali sala kwa Bikira Maria.

 

 

10 October 2018, 16:35