Papa atakutana na marais wa mabaraza ya Maaskofu duniani kote!
Sr. Angela Rwezaula - Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, atakutana mjini Vatican na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani kote kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019, ili kuongea juu ya namna ya kuzuia manyanyanyaso ya kingono dhidi ya watoto na watu wazima waathirika. Hayo yameleezwa na Kaimu Msemaji mkuu wa vyombo vya habari Vatican, Paloma Garcia Ovejero, wakati wa kikao kidogo, mara baada ya Mkutano wa Baraza la Makardinali washauri wa Papa (C9) ambapo hata Papa Francisko alikuwapo katika shughuli hiyo ya mkutano. Pamoja na hayo, Papa pia amempongeza Kardinali Sean Patrick O’ Malley, mara baada ya kukutana naye na kusasishwa juu ya kazi inayoendelea ya Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi wa watoto.
Katika Mkutano huo makardinali wote 9 wameonesha kupendezwa na mafanikio ya Mkutano wa IX wa Familia Duniani, uliofanyika hivi karibuni Mjini Dublin Ireland. Katika Kikao cha Baraza la Makardinali (C9) kwenye sehemu ya kwanza, liyofunguliwa Jumatatu tarehe 10 Septemba,walianza na tafakari ya kina kwa mtazamo wa pamoja kuangalia kazi ya muundo wenyewe wa Baraza hilo, kwa kuzingatia hata umri wa baadhi ya wajumbe katika Baraza. Pamoja na hayo hawakutoa habari zaidi, japokuwa wametoa taarifa juu ya mkutano wa (C9) ujao ambao utafanyika tarehe 10-12 Desemba 2018 ambayo walikuwa wameombwa na Papa Francisko
Ikumbukwe mkutano huo ulianza tarehe 10 Septemba mjini Vatican, wa Baraza la washauri wa Papa akiwemo hata Baba Mtakatifu Francisko. Huo ni mkutano wa XXVI wa Baraza la Ushauri la Makardinali. Baraza la Ushauri la Makardinali ambalo linaitwa C9 liliundwa kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko ilikushirikiana katika majukumu ya huduma ya Kanisa na ushirikiano kwa ajili ya mageuzi ya Vatican. Shughuli yao inaongozwa na Papa mwenyewe. Hiki ni Kikao cha XXVI tangu kuanza kwake kunako tarehe 1-3 Oktoba 2013.
Kwa miaka hii mitano sehemu kubwa ya shughuli imejikita katika mtazamo wa Katiba mpya ya mageuzi ya Vatican yenye kauli mbiu ya muda "Praedicate evangelium" yaani "Hubirini Injili". Makardinali Washauri 9 wameweza kwa sasa kumkabidhi Papa rasimu ya muda , ili kuweza kutoa marekebisho ya muundo na kusomwa na wanasheria. Mkutano huo umeudhuriwa na makardinali sita, kwa maana ya kutoweza kufika Kardinali Francisco Javier Errázuriz Ossa, Askofu mkuu mstaafu wa Santiago ya Chile, Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya,Askofu mkuu wa Kinshasa na George Pell, Rais wa Sektreatarieti ya Uchumi Vatican