Tafuta

Sherehe ya kung'ara Bwana. Sherehe ya kung'ara Bwana. 

Sherehe ya kung'ara Bwana! Utimilifu wa sheria na unabii: Fumbo la Msalaba

Kung’ara kwa Bwana ni tukio ambalo Kristo Yesu alilitumia ili kuwaimarisha mitume wake, waweze kukabiliana na Kaskfa ya Msalaba, kielelezo cha: hekima, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika Fumbo la Msalaba!

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Agosti anaadhimisha Sherehe ya Kung’ara kwa Bwana, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii unaofumbatwa katika Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kung’ara kwa Bwana ni tukio ambalo Kristo Yesu alilitumia ili kuweza kuwaimarisha mitume wake, ili waweze kukabiliana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba, kielelezo makini cha: hekima ya Mungu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika Fumbo la Msalaba!

Mama Kanisa katika maadhimisho haya anaungama kwa dhati kabisa: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene.  Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele!

Ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuisikiliza sauti yake na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yule Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu”. Sherehe ya Kung’ara Bwana ni mwendelezo wa Siku kuu ya Ubatizo na Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Mwanga unaong’ara katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwanga utakaojionesha kwa namna ya pekee, Siku ile Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho!

Kusikiliza ni sanaa inayohitaji majiundo makini na endelevu, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kuwa wasikivu wema na wazuri, tayari kumwilisha kile wanachokisikia kutoka katika dhamiri zao nyofu! Yesu kama ilivyokuwa kwa mitume wake wa karibu yaani: Petro, Yakobo na Yohane, Wakristo pia wanahamasishwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu imefunuliwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu katika Sheria na Unabii na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Bikira Maria.

Wakristo wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anaandama nao katika hija ya maisha yao. Sherehe ya kung’ara kwa Bwana ni chachu ya mabadiliko katika maisha kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu katika maisha, mambo msingi yanayowaelekeza waamini katika ukamilifu na utakatifu wa maisha.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Kanisa  kwa mwaka huu, 2018, linafanya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipofariki dunia akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Itakumbukwa kwamba, alitangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 19 Oktoba 2014 na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa kwa sasa linajiandaa kumtangaza Mwenyeheri Paulo VI hapo tarehe 14 Oktoba 2018 kuwa Mtakatifu. Kanisa mwaka huu 2018 limeadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”.  

Ni waraka unaopembua kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Anahimiza: wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha. Huu ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia.

Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

04 August 2018, 14:43