Mapendelezo ya Vijana kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, Oktoba, 2018 Mapendelezo ya Vijana kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, Oktoba, 2018 

Mapendekezo kutoka kwa vijana kwa Mababa wa Sinodi ya vijana 2018

Mama Kanisa anapaswa kuangalia jinsi ambavyo atasaidia kuwaongoza, kuwainua na kuwaimarisha vijana katika maisha yao. Hati hii ni muhtasari wa changamoto za vijana kutoka katika mabara, dini na tamaduni mbali mbali duniani, inayoonesha mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Wajumbe wa vijana waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba 2018 wametoa “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” itakayowasilishwa kwa Mababa wa Sinodi kama sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi”. Vijana wa karne ya ishirini na moja, wanakabiliana na changamoto na fursa ambazo ziko ndani na nje yao wenyewe, na kadiri ya mazingira wanamotoka. Mama Kanisa anapaswa kuangalia jinsi ambavyo atasaidia kuwaongoza, kuwainua na kuwaimarisha vijana katika maisha yao. Hati hii ni muhtasari wa changamoto za vijana kutoka katika mabara, dini na tamaduni mbali mbali duniani, inayoonesha mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Mama Kanisa.

Ni hati ambayo inashuhudia hali halisi, watu, imani na mang’amuzi ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia na wala si mafundisho mapya ya kitaalimungu. Itakuwa ni “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya kutendea Kazi” kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Umati mkubwa wa vijana umeshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii na hivyo itakuwa ni sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi” kwa Maaskofu. Ni matumaini kwamba, Kanisa pamoja na taasisi mbali mbali zitaweza kujifunza kuwasikiliza vijana.

Hati hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza inagusia changamoto na fursa kwa vijana katika ulimwengu mamboleo: majiundo ya vijana kiutu; mahusiano na watu wengine; vijana na matumaini kwa siku za usoni; mahusiano ya vijana na maendeleo ya teknolojia; vijana na maana ya maisha. Sehemu ya pili inagusia: Imani na miito; mang’amuzi pamoja na kuwasindikiza. Hapa vijana wanaangalia uhusiano wao na Kristo Yesu; Imani na Kanisa; Maana ya wito katika maisha; Mang’amuzi ya miito; Vijana na dhamana ya kuwasindikiza.

Sehemu ya tatu inapembua mchakato wa elimu na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa. Yaani: Mfumo wa Kanisa; vijana kama wadau wakuu; mahali pa upendeleo; Sera na mikakati mbali mbali inayopaswa kuendelezwa; Nyenzo za kutumia, maadhimisho ya matukio mbali mbali ya Kanisa; sanaa na uzuri; Ibada ya kuabudu, Tafakari ya Neno la Mungu na Taamuli; Ushuhuda na mwishoni ni dhana ya Sinodi inayofumbatwa katika majadiliano, maamuzi na utekelezaji wa pamoja kama familia ya Mungu!

SEHEMU YA KWANZA: Changamoto na fursa kwa vijana katika ulimwengu mamboleo. Familia ni mahali pa kwanza kabisa pa kufunda utu na utambulisho wa vijana, lakini kutokana na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, vijana pia wanaathirika katika utu na heshima yao. Baadhi ya vijana wanaona kana kwamba, wazazi na walezi wao wamepitwa na wakati na sasa wanataka mambo mapya. Kumbe, Kanisa halina budi kujizatiti katika kukuza na kudumisha utume wa familia, kwa kuhakikisha kwamba, familia zinajikita katika tunu msingi za kifamilia na kiutu pamoja na kusaidia malezi ya vijana wa kizazi kipya katika maeneo ambayo uhuru wa watoto unapewa kipaumbele cha pekee. Utambulisho wa vijana ni muhimu sana, ili kuendelea kubaki katika urithi wa imani na utamaduni wao. Vijana wahamiaji wanajikuta wakikabiliana na changamoto ya kuongokea dini nyingine, ili waweze kukubalika katika nchi wanamopatiwa hifadhi.

Vyama vya kitume na mihimili mingine ya uinjilishaji, isaidie mchakato wa malezi na makuzi ya vijana, daima imani ikipewa msukumo wa pekee. Makundi ya vijana, marafiki pamoja na mitandao ya kijamii inaweza kuwa pia ni mahali muafaka pa malezi na makuzi ya vijana, ili kuwa na uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao! Ni mahali muafaka pa kuunda utambulisho wa vijana kuhusu masuala: ya tendo la ndoa, matumizi haramu ya dawa za kulevya, ndoa mpito, familia tenge bila kusahau changamoto kubwa za athari za magenge ya kihalifu, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo; ghasia, rushwa na ufisadi; unyonyaji na nyanyaso za kijinsia; mauaji ya wanawake; dhuluma na uharibifu wa mazingira, nyumba ya wote. Vijana wana wasi wasi na mashaka kutokana na vita, kinzani za kisiasa na kijamii bila kusahau athari za kiuchumi.

Kuhusu mahusiano na watu wengine: tofauti msingi kati ya watu ni utajiri na fursa katika ulimwengu mamboleo; ni mahali pa kukuza na kudumisha majadiliano na maridhiano kati ya watu; kwa kuheshimu na kuthamini mawazo ya wengine. Lakini, pia vijana wanajisikia mara nyingi kwamba, wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwani dini katika baadhi ya nchi haina tena mashiko katika maisha ya hadhara. Ubaguzi ni changamoto nyingine inayogumisha mahusiano kati ya vijana na matokeo yake, inakuwa vigumu sana kusikiliza Habari Njema ya Wokovu. Vijana wanavutwa na shuhuda za wafiadini na waungama imani, ambao wameacha urithi mkubwa wa imani na maisha ya kiroho, changamoto ya kukuza na kudumisha ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa kulinda na kudumisha utu na heshima yao.

Vijana na matumaini yao kwa siku za usoni: Fursa za ajira, mtindo wa maisha na utambulisho wa vijana ni changamoto zinazowaandama vijana wengi. Vijana wanataka kusikilizwa na kushirikishwa katika majadiliano, maamuzi na utekelezaji wa mambo msingi yanayogusa maisha yao. Kanisa liwasaidie vijana kung’amua wito pamoja na kuendelea kuwachangamotisha kuambata utakatifu wa maisha kama utimilifu wa furaha ya kweli. Vijana wengi wanakabiliana na magonjwa na ulemavu; hawana fursa za kupata elimu ya juu gharama kubwa, kiasi hata cha kuweka utu na heshima yao rehani kutokana na ukosefu wa fursa za kazi. Kumbe, haki jamii inapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali ili kuwajengea tena vijana matumaini kwa kutatua vita, migogoro na kinzani mbali mbali zinazogumisha maisha ya watu wengi duniani, sanjari na kutunza mazingira, kudumisha usawa na usalama. Vijana wanatamani kuona amani inatawala, Kanisa hasa Barani Afrika linajitegemea na kwamba, vijana wanakuwa ni sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu kwa kufanya maamuzi kuhusu mustakabali na hatima ya maisha yao!

Mahusiano ya vijana na maendeleo ya teknolojia: Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ambayo imewafaidisha vijana wengi, lakini pia, maendeleo haya yamewaathiri vijana kwa kubomoa mahusiano na utengamano wa maisha ya kijamii. Athari za mitandao ya kijamii ni kubwa sana miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwani kimekuwa ni kiungo cha kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kushirikisha habari, mawazo, tunu na mambo mengine yenye mafao ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita! Hatari yeke ni upweke hasi, uvivu na hali ya kukata tamaa.

Tofauti zinaonekana kuwa ni kero! Vijana wafundwe kuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, kwa kukazia utu na heshima yao badala ya kutumia mitandao ya kijamii kwa kujidhalilisha kwa picha za utupu na hatimaye kukosa utambulisho makini. Majadiliano haya yanaweza kupanuliwa hata kugusa: Kanuni maadili viumbe; Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; matumizi ya roboti katika uzalishaji na utoaji wa huduma. Kumbe, mitandao ya kijamii inaweza kuwa ni uwanja unaoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji mpya, pamoja na Kanisa kulivalia njuga janga la picha za utupu, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na ubabe wa mitandao “Cyberbulism”.

Vijana na maana halisi ya maisha: Vijana wengi wanatafuta maana ya maisha, imani na mafanikio kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao kiasi hata cha kuzikimbia familia, tamaduni na imani zao kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, kidini, kisiasa na kiuchumi. Kashfa zilizoikumba Kanisa zimekuwa ni kikwazo cha imani kwa vijana wengi. Kumbe, Kanisa linapaswa kuwekeza zaidi katika imani na ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, lakini zaidi wanawake na wasichana; usawa na umuhimu wa wanawake na wasichana katika maisha na utume wa Kanisa.

Bado vijana wanasigana sana na Kanisa mintarafu mafundisho kuhusu: utoaji mimba, ndoa za watu wa jinsia moja, uchumba sugu, ndoa; maisha na wito wa kitawa na kipadre, una mwelekeo tofauti sana katika maisha na utume wa Kanisa. Haya ni mambo nyeti yanayopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa kwa kuimarisha utume miongoni mwa vijana, pamoja na kuendelea kupyaisha maisha ya Kikristo, ili yasionekane kana kwamba, yamepitwa na wakati. Vijana wamekumbusha kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha na matumaini yao ya kweli, kumbe wanapaswa kujenga na kudumisha uhusiano wa dhati na Yesu.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

11 August 2018, 10:21