Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akisalimiana na mahujaji wa Chama cha Watumishi wa Altareni, 31 Julai 2018. Papa Francisko akisalimiana na mahujaji wa Chama cha Watumishi wa Altareni, 31 Julai 2018.  (ANSA)

Siku ya Upashanaji Habari Tanzania, 5 Agosti 2018

Mawasiliano ni sehemu ya mpango wa Mungu kwetu na ni njia muhimu ya kung’amua mshikamano. Tukiwa tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tuna uwezo wa kujieleza na kushirikishana ukweli, uzuri na wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Ukweli utawaweka huru, habari potofu na uandishi wa amani ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Duniani, ambayo nchini Tanzania inaadhimishwa, kila mwaka katika Jumapili ya kwanza ya mwezi Agosti. Huu ni muda muafaka wa kutafakari kwa kina na mapana mchango unaotolewa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Waamini wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kuviwezesha vyombo hivi ili viweze kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ndani nan je ya Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mawasiliano ni sehemu ya mpango wa Mungu kwetu na ni njia muhimu ya kung’amua mshikamano. Tukiwa tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tuna uwezo wa kujieleza na kushirikishana ukweli, uzuri na wema. Tuna uwezo wa kuelezea mang’amuzi binafsi katika dunia na kujenga kumbukumbu ya uelewa wa matukio. Lakini tukiwa tunaongozwa na kiburi na ubinafsi hatuwezi kutoa mawasiliano mema kama inavyojionesha katika matukio ya Biblia katika historia ya Kaini na Abeli, hata tukio la Mnara wa Babeli. (Mw 4: 1-16; 11, 1-9). Uwezo wa kubadilisha ukweli ni dalili ya kawaida ya upotofu ambayo mtu hufanya binafsi na kwa pamoja. Kwa upande mwingine, tukiwa waaminifu katika mpango wa Mungu, mawasiliano huwa ni sehemu ya kuelezea uwajibikaji kwa kutafuta ukweli na ujenzi wa wema.

Katika ulimwengu wa leo wenye mabadiliko ya kasi ya mifumo ya kidigitali, tunashuhudia kuenea kwa kile kinachojulikana kama ‘habari potofu’ (fake news). Hii inatualika kutafakari, ndio maana nimeamua kurudisha kwenu tena suala la ukweli katika ujumbe wangu wa siku ya upashanaji habari, ambao mara nyingi watangulizi wangu kuanzia Mwenye Heri Paulo VI (katika ujumbe wa mwaka 1972; ulikuwa na mada ya “Mawasiliano ya kijamii katika huduma ya ukweli”).  Katika hali hii, ningependa kuchangia katika jitihada za pamoja za kupinga kuenea kwa habari za uongo na kugundua tena utu wa uandishi wa habari na wajibu binafsi wa mwandishi wa habari kuwasilisha ukweli.

1.      Nini cha “uongo” katika habari potofu?

Neno "habari potofu" limekuwa kitu cha majadiliano makubwa na mjadala. Kwa ujumla, linahusisha kuenea kwa taarifa isiyo sahihi katika mitandao au katika vyombo vya habari. Inahusiana na taarifa za uongo zisizo na msingi kwa uwepo wake; zenye nia ya kutaka kudanganya hadi wasomaji na watazamaji wake. Usambazaji wa habari za uongo unaweza kujibu lengo walilokusudia, kwa kushawishi maamuzi ya kisiasa na kukuza mapato yao kiuchumi.

Ufanisi wa habari potofu unajitokeza awali ya yote mahali ambapo wao wanaigiza kwa asili yao yaani uwezo wa kutaka kuonekana na kusifika. Na hatua ya pili, habari za uwongo lakini zinaaminika huwa zinavutia, kwa maana ya kupendwa na kuchukuliwa makini na walengwa. Kwa kuwa na uwezo wao wa kulaghai, hufanya marudio ambayo yanasambaa kwa haraka ndani ya maisha ya kijamii na kuwatumia wenye hisia rahisi, kuziamsha kwa haraka, kwa mfano wa kuleta wasiwasi, dharau, hasira na kuchanganyikiwa. Usambazaji wa habari potofu unatumia kwa ujanja mitandao ya kijamii na kwa mantiki ya kuhakikisha inafanya kazi. Habari za uongo zinaweza kuenea kwa haraka sana.

Ugumu wa kufichua na kuondokana na habari potofu ni kwa sababu watu wengi mara nyingi wako katika mazingira ya kidigitali ya pamoja, ambayo ni rahisi kupitia mantiki nyingi na maoni tofauti. Na matokeo ya mantiki ya habari potofu, ni kwamba, badala ya kukabiliana vema na vyanzo vingine vya habari, jambo ambalo linaweza kuleta uchanya wa mjadala na kufungua mazungumzo ya ujenzi, inageuka kuwa hatari hata bila utashi wa wadau wake ambao usambaza maoni ya uwongo na ushahidi. Tishio la habari potofu ni ung’oaji wa mzizi wa mwingine na uwepo wake unakuwa kama adui, hata kuwa shetani ambaye anaweza kutoa ushahidi wa migogoro ya uongo; ndivyo habari za uwongo zinavyojionesha uwepo wake hasa  tabia ya kutojali.

2.      Ni jinsi gani tutatambua habari potofu?

Hakuna hata mmoja anayeweza kusamehemewa jukumu la kupinga uongo huo. Hii siyo kazi rahisi, kwa maana usambazaji wa uongo unapitia katika mazungumzo mengi ambayo yanaenea kichini chini pia udanganyifu wake mara nyingi ni wenye mfumo wa kisirisiri. Jitihada zinafanyika kuanzishwa programuu za elimu zinazojikita katika kuwasaidia watu waweze kutafsiri na kuchunguza taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari, na kuwafundisha kuwa sehemu ya msingi katika kuuondoa uongo na kuutambua badala ya kuchangia kueneza uongo bila wao kujua.

Licha ya hatua hiyo ya mafunzo ni pamoja na ile ya kuanzisha taasisi na kisheria ambazo zinajikita kwa kina katika kusitisha matukio hayo, kama vile taaluma ya hali ya juu ya kiteknolojia na makampuni ya mitambo ya kutafuta dhana mpya ya kuhakiki na kuwatambua wahusika wanaojificha nyuma ya mamilioni ya picha za kidigitali.

Uzuiaji na njia ya ugunduzi wa habari potofu, awali ya yote unahitaji hata umakini wa kina na mang’amuzi. Ki ukweli ili kuweza kuwagundua, kile  ambacho chaweza kuelezwa kwamba ni mantiki ya nyoka,  mwenye uwezo wa kujificha mahali popote ili aweze kuuma. Inahitaji mkakati wa nyoka mjanja ambaye anatajwa katika Kitabu cha Mwanzo, yeye alikuwa wa kwanza kumdanganya binadamu ikawa ndiyo habari ya uongo ya kwanza (Mw 3:1-15), baadaye ikasababisha majanga yote ya dhambi hadi kufikia  mauaji ya kwanza,  Kitabu cha mwanzo sura ya 4, na  hata katika idadi kubwa ya mitindo ya ubaya dhidi ya Mungu, jirani, jamii na kazi ya uumbaji.

Hayo yanajionesha katika maelezo ya dhambi ya asili, kwani, mshawishi alimkaribia mwanamke na kujifanya kama rafiki akionesha  kujali wema wake, akaanza  mazungumzo utafikiri ya kweli, lakini yalikuwa ukweli nusu nusu: “Ni kweli Mungu alisema: mwaweza kula matunda ya mti wowote katika bustani, lakini matunda ya mti wa ujuzi wa wema na mabaya msile.... (Mw 2:17).

Mwanamke alijibu na kuelezea nyoka, lakini kwa kutaka kumfafanulia zaidi: “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini, lakini matunda yaliyoko katikati ya bustani msiuguse ili tusije tukafa  (Mw 3:2). Jibu hili la mwanamke  linatolewa kama vile la kisheria na lenye ugumu: kwa maana alionesha imani kwa mshawishi na kujiachia avutiwe naye, ndiyo maana mlaghai  akabadilisha majibu hayo, akamwambia mwanamke “hamtakufa (Mw 3:4) “kwa maana alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu mkijua mema na mabaya”! Mw 3:5).

Nyoka alikuwa amefanya kazi yake ya kumuondoa mwanamke katika amri ya Mungu iliyokuwa ya wema na kufuata ushawishi wa adui shetani kwa maana “mwanamke huyo aliona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula na wavutia macho” (Mw 3:6). Katika matukio hayo ya Biblia yanaonesha wazi  hali halisi na msingi katika kuthibitisha na kuonesha juu ya utoaji wa habari za uongo kwamba, hakuna maelezo ya kutofahamika; kinyume chake, kuamini uongo huzalisha matokeo mabaya. Hata upotofu wa ukweli unaoonekana  kidogo unaweza kuwa na athari za hatari.

Mchezo huo kiukweli unaonekana wazi katika habari za uongo ambazo daima zinasambaa kwa namna ya haraka na rahisi kiasi kwamba huwa vigumu kuzuia, siyo kwa sababu ya dhana ya kushirikishana ambayo ni mtindo wa mitandao ya kijamii, lakini pia ni kushikilia tamaa isiyoweza kushindwa ambayo inarudi kwa urahisi na inawaka katika maisha ya binadamu. Na sababu hizo wakati mwingine ni sawa na za kiuchumi na fursa za mawasiliano ya uongo yana mizizi yake katika kiu ya madaraka, au kutaka kuwa navyo, anasa ambapo mwisho wake tunakuwa waathirika wa kudanganyika zaidi kuliko tukio la  ubaya ambao pia unazungusha uongo wa hapa na pale ili kuiba uhuru wa moyo.

3.       “Ukweli utawaweka huru” (Yn 8:32)

Kuendeleza uchafuzi wa lugha za uongo huishia kuleta giza ndani ya moyo wa mtu. Mwanafalsafa mmoja Dostoevskij aliandika jambo maarufu akisema: “anayejidanganya na kusikiliza uongo wake, mwisho wake atafikia kushindwa kuchanganua ukweli, uwe wa ndani  na hata unaomzunguka, baadaye ataanza  kukosa thamani yake  mwenyewe hata ya wengine. Ukosefu wa kuthamini mwenyewe tena na pia mtu yeyote, ataacha kupenda na baadaye kukosa upendo, kwa maana hujisikia kujitenga binafsi na kuwa na tamaa na ubaya; na kutokana na maovu yake hugeuka kama mnyama, kwa maana ya mazoeza ya uongo unaoendelea (Taz Ndugu wa Karamazov, II, 2).

Je, tujilinde vipi? Mzizi wa kuzuia virusi vya uongo ni ukweli. Katika upeo wa kikristo ukweli si msingi ambao unatazama juu ya mambo na kutengenisha ukweli au uwongo tu. Ukweli si kuyapa mwanga mambo yenye giza tu: ukweli ni kutoa hali halisi ilivyo, kama vile neno la kizamani la kigiriki lisemavyo aletheia (da a-lethès) kisichofichwa, kinatupelekea kuamini.

Ukweli unajikita katika safari ya maisha yetu yote, kwa sababu hiyo, katika Biblia, ukweli  unachukua hali ya msaada, ni msingi, ni imani pia ni kama mzizi  wa “aman” ikiwa na  maana ya Amina katika neno la kiliturujia. Ukweli ni kitu ambacho tunaweza kusimama juu yake ili tusianguke. Na uhusiano wa ukweli wa kuamini ambao unastahili kuwa na matumaini ya  kutambua  ukweli ni Mungu anayeishi. Ndiyo uthibitisho wa Yesu; “Mimi ni ukweli (Yh 14:6) kwa maana hiyo binadamu anazidi kugundua kwa mara nyingine tena  ukweli huo wakati anafanya uzoefu wake mwenyewe katika imani na kuamini anayempenda. Ni kwa njia hiyo binadamu anakuwa huru kwa maana ukweli utawapeni uhuru (Yh 8:32)

Kujikomboa dhidi ya uongo na kutafuta uhusiano ndiyo viungo viwili ambayo haviwezi kukosa  ili maneno yetu na matendo yetu yaweze kuwa ya kweli, dhati na kuaminika. Ili kupata  mang’amuzi ya ukweli ni lazima kukesha, na kusema kile ambacho ni cha ukweli  na kukuza wema na kupinga  kile ambacho ni kinyume, kile kinachojitenga, kinachogawanya na kinachopinga. Ukweli hujitenga  kwa hakika pale ambapo  unataka kulazimisha jambo lisilo la kawaida  la kibinafsi; ukweli hutokana na mahusiano ya bure kati ya watu, kwa kusikilizana.

4.      Amani ni habari ya kweli  

Dawa ya kuzuia uongo siyo mkakati, bali ni watu: watu ambao ni huru, kutokana na kiu, wako tayari kusikiliza na kwa njia ya jitihada za mazungumzo ya dhati ili ukweli uonekane; watu ambao, wamevutiwa na mema wanawajibika hata katika matumizi ya lugha. Iwapo njia ya kuondokana na usambazaji wa habari za uongo ni kuwajibika kwa namna ya pekee ni kujumuisha hasa wale wahusika wa ofisi za mawasiliano, waandishi wa habari na walinzi wa habari. Hawa katika ulimwengu mamboleo si kazi tu, bali ni utume wa kweli. Wanalo jukumu, licha ya uharaka wao wa kutaka kutoa habari wa  kwanza, wanapaswa kukumbuka kuwa kiini  cha habari si katika uharaka wa kutoa habari kwa wasikilizaji, lakini kitovu ni watu.

Kuhabarisha watu ni kuwatengeneza, kwa sababu inahusiana na maisha ya watu, na kwa njia hiyo kuhifadhi vyanzo na ulinzi wa mawasiliano ndiyo ukweli na mchakato wa maendeleo ya wema ambayo yanazaa matumaini na kufungua njia za mawasiliano na amani. Ningependa sasa kumualika kila mmoja kuhamasisha uandishi wa habari wa amani.  Kwa  kufanya hivyo si kwa  maana ya kuwa na uandishi wa uzuri kwa kukataa matatizo makubwa yaliyopo ya kutotoa  sauti isiyo nzuri. Kinyume chake kuna ulazima wa uandishi wa habari za kweli bila uongo, zenye uadui na uongo na kushikilia matukio kutangaza yaliyo kinyume, zenye kutafuta ufanisi na matangazo kama mabomu; uandishi ambao unafanywa na watu kwa ajili ya watu ambao wanatambua kama huduma ya watu wote, hasa wale ambao wako katika ulimwengu, sehemu kubwa hawana sauti.

Uandishi wa habari unaojibidiisha kutafuta sababu za kweli za migogoro, ili kukuza uelewa wa mizizi na ushindi  kwa njia  ya mchakato wa fadhila; uandishi  ambao unajikita katika kuelekeza suluhisho tofauti dhidi ya mlolongo wa habari mbaya na  unyanyasaji wa maneno. 

Na mwisho, kwa mwaliko wa sala ya kifranciskani, tunaweza kuelekeza ukweli binafsi kwa maneno haya:

Bwana, tufanye tuwe vyombo vya amani yako.

Tusaidie kubaini uovu uliopo katika mawasiliano ambao haujengi umoja.

Tusaidie kuondoa chuki katika hukumu zetu.

Tusaidie tuweze kuzungumza na wengine kama kaka na dada zetu

Wewe ni mwaminifu; tunaomba maneno yetu yawe mbegu ya wema kwa ulimwengu:

Palipo na kelele, tujifunze kusikiliza;

Palipo na mkanganyiko, tuhamasishe maelewano;

Palipo na utata, tulete ufafanuzi;

Palipo na utengano, tulete ushirikiano;

Palipo na ukuzaji wa mambo, tulete uhalisia;

Palipo na mambo ya juu juu, tuibue maswali halisi;

Palipo na ubaguzi, tuamshe uaminifu;

Palipo na uadui, tulete heshima;

Palipo na uongo, tulete ukweli.

Amina.

02 August 2018, 07:13