Vijana wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican. Vijana wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican. 

Kardinali Bassetti inalipa kwa Kanisa kuwekeza kwa vijana!

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema katika hija, hii vijana wameonesha ujasiri, imani na udumifu katika kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali katika hija ya maisha yao ambayo imewakirimia: amani na utulivu wa ndani. Imekuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya maisha ya ujana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Vijana nchini Italia ambayo limefikia kilele chake kwa Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili tarehe 12 Agosti 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayotimua vumbi, mwezi Oktoba 2018. Katika hija, hii vijana wameonesha ujasiri, imani na udumifu katika kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali katika hija ya maisha yao ambayo imewakirimia kwa namna ya pekee kabisa: amani na utulivu wa ndani. Imekuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya maisha ya ujana.

Hii ni sehemu ya utangulizi uliotolewa na Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia wakati wa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na vijana baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maaskofu Katoliki Italia wanapenda kuonesha na kushuhudia upendo na mshikamano wao na Baba Mtakatifu. Kwa muda wa juma zima, vijana wameshuhudia na kutangaza kuwa wao ni sehemu muhimu ya Kanisa, wako tayari kujisadaka na kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, chemchemi ya furaha ya maisha mapya.

Vijana wameweza kujenga umoja na urafiki na Kanisa limewabeba wote bila hata ya kumtelekeza kijana awaye yote! Kwa hakika inalipa kwa vijana kushirikiana na kushikamana, alama wazi ya matumaini ya walimwengu. Vijana katika hija ya maisha yao, wamegundua amana na utajiri unaofumbatwa katika imani, tamaduni na Mapokeo ya Kanisa na kwamba, kwa sasa wanaendelea kuandika kurasa za kuwajibika kwa kuchota utajiri na uzoefu wa majadiliano na watakatifu pamoja na mashuhuda wa imani. Kwa namna ya pekee kabisa, Injili imeweza kupandikizwa tena katika nyoyo za vijana.

Baba Mtakatifu ni kielelezo cha Uso wa mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Hawa ndio Mitume wa Yesu na Watakatifu waliotangaza na kushuhudia Injili. Vijana wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa utayari wake. Sasa wanarejea tena majumbani mwao, hali ambayo ni ngumu sana, kwani kwa sasa changamoto kubwa mbele yao ni kumwilisha umoja na udugu; kuendelea kutakasa kumbu kumbu na mambo ya mpito ili kuachia nafasi kwa mambo msingi katika maisha. Uzoefu na mang’amuzi haya, yawawezeshe vijana kuwajibika kwa njia ya ukarimu, kwa kujenga maagano ya udugu na kutekeleza kwa vitendo yale mambo msingi walioyasikia wakati wa hija yao mjini Roma kwa kuzingatia ukweli na uwazi.

 

 

12 August 2018, 14:30