Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na vijana kutoka Italia, Circo Massimo, 11 Agosti 2018. Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na vijana kutoka Italia, Circo Massimo, 11 Agosti 2018. 

Papa Francisko: Siku ya Vijana Italia 2018: Maswali na majibu!

Baba Mtakatifu amejibu maswali makuu matatu. Vijana wamemuuliza kuhusu: changamoto ya kuunda utambulisho wa mtu binafsi na utekelezaji wa ndoto za maisha ya ujana katika uhalisia wake! Pili ni kuhusiana na mang’amuzi ya maisha, dhana ya sadaka na uwajibikaji katika ulimwengu wa vijana. Tatu, vijana wamegusia kuhusu imani na maana ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Siku ya Vijana wa Italia kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, hapa mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 11 Agosti 2018 kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” ulioko mjini Roma, amekutana na umati wa bahari ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia! Baba Mtakatifu amejibu maswali makuu matatu. Vijana wamemuuliza Baba Mtakatifu kuhusu changamoto ya kuunda utambulisho wa mtu binafsi na utekelezaji wa ndoto za maisha ya ujana katika uhalisia wake! Pili ni kuhusiana na mang’amuzi ya maisha, dhana ya sadaka na uwajibikaji katika ulimwengu wa vijana. Tatu, vijana wamegusia kuhusu imani na maana ya maisha!

Baba Mtakatifu amewaambia vijana kwamba, kuwa na ndoto ni jambo la muhimu sana katika maisha ya ujana, kwani hii ni dira na mwongozo wa maisha; chachu ya matumaini inayotoa mwanga kuhusu utu wa mtu. Mwaliko ni kuhakikisha kwamba, ndoto hizi zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa ajili ya siku za usoni, hali inayohitaji ujasiri na udumifu pasi na kukata wala kukatishwa tamaa kutokana na vikwazo mbali mbali wanavyoweza kukutana navyo katika maisha.

Ndoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowawezesha vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani, udugu na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ndoto ya amani inakwenda kinyume cha ubinafsi na uchoyo ambao kimsingi ndicho chanzo kikuu cha vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii. Vijana wajifunze kujenga utamaduni wa amani unaosimikwa katika maisha ya kijumuiya, ili kudumisha urafiki, upendo na mshikamano wa kweli!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, vijana wamegusia dhana ya woga na wasi wasi katika maisha, kiasi hata cha kushindwa kuthubutu kutekeleza zile ndoto zao! Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mfano bora wa kuigwa aliyehakikisha kwamba, anatekeleza ile ndoto ya maisha yake, licha ya vikwazo vilivyokuwa vimewekwa na wazazi wake. Vijana wasikate tamaa wanapokutana na vikwazo kutoka kwa wazee na watu wazima kwani muda wao wa kuota ndoto umekwisha kufutika.

Lakini, ili kuweza kuwa na ndoto njema zinazotekelezeka katika maisha, vijana hawana budi kuwa na waalimu na walezi bora, watakaowaelekeza na kuwasindikiza, watakaowaonjesha: imani, matumaini na mapendo, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao! Vijana wanapaswa kuondokana na woga na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko katika maisha yao! Waendelee kuwa ni mahujaji wa ndoto zao, kwa kuthubutu kuzimwilisha katika uhalisia wa maisha.

Pili ni kuhusiana na mang’amuzi ya maisha, dhana ya sadaka na uwajibikaji katika ulimwengu wa vijana, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, vijana wanapaswa kuamua katika ukweli unaowawajibisha katika maamuzi ya maisha na upendo wa dhati. Uhuru wa kweli katika upendo unaomwilishwa katika maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Uhuru uwawezeshe vijana kujizatiti katika maisha yao tayari kujisadaka bila ya kujibakiza wala kutafuta njia ya mkato. Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake, aliwaumba mwanaume na mwanamke ili waweze kukamilishana katika safari ya maisha.

Kristo Yesu katika Agano Jipya ameupatia utimilifu huu hadhi ya hali ya juu kabisa kama Sakramenti ya Ndoa. Kazi katika maisha ya ndoa na familia, inawawezesha wanandoa kutekeleza dhamana na wajibu wao kama sehemu ya utimilifu wa utu na heshima yao. Upendo wa dhati katika maisha ya ndoa na familia, unawawezesha wanandoa kutakatifuzana. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuhifadhi upendo wao kama sehemu ya amana na utajiri wa maisha; upendo lazima ufumbatwe katika uaminifu, sadaka na uwajibikaji na kwamba, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na matunda ya upendo wa dhati!

Tatu, vijana wamegusia kuhusu imani na maana ya maisha! Mwanadamu katika hija ya maisha yake anakutana na vishawishi, ndiyo maana katika Sala ya Baba Yetu iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni, waamini wanamwomba, Mwenyezi Mungu asiwaache vishawishini, awaokoe kutoka katika dhambi na ubaya wa moyo. Neno la Mungu na Liturujia ya Kanisa ni kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kukombolewa. Maisha na utume wa Kanisa, unapaswa kufumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kuwasindikiza, kuwasikiliza na kuwashuhudia yale matakatifu yanayobubujika kutoka katika Neno, Sakramenti na Mafumbo ya Kanisa.

Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni kazi ya Roho Mtakatifu, kama ilivyojitokeza kwa Kanisa la Mwanzo. Ni ushuhuda unaojikita katika unyenyekevu na heshima kwa jirani, kama chemchemi ya majadiliano katika ukweli na uwazi na haya ndiyo majibu wanayohitaji watu si tu kusikia, bali kuyaona katika uhalisia wa maisha. Kanisa linapaswa kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Kila mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ujumbe wa Kristo Yesu ni wazi kabisa, ushuhuda wa imani usiomwilishwa katika matendo, ni ubatili mtupu!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

11 August 2018, 13:05