Tafuta

Uhusiano kati ya Serikali na Kanisa unafumbatwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhusiano kati ya Serikali na Kanisa unafumbatwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Mahusiano kati ya Serikali na Kanisa yanafumbatwa katika huduma kwa binadamu

Yaliyojadiliwa kati ya Rais Magufuli na viongozi wa TEC, imekuwa ni nafasi ya kujitambulisha kama viongozi wapya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; Pili kumshukuru kwa kuendelea kujenga mahusiano mema na Kanisa, tatu kumpongeza kwa ujasiri, ari na mwamko wa maendeleo nchini Tanzania na hatimaye, kuwasilisha rai ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, Jumanne, tarehe 7 Agosti 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Wakristo Tanzania, CCT pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, walioomba kukutana naye na kujitambulisha, Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Ujumbe wa Jumuiya ya Wakristo Tanzania umeongozwa na Askofu Anikilisa Cheyo, Mwenyekiti na kwa upande wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ujumbe umeongozwa na Askofu Gervas John Nyaisonga, Rais wa Baraza.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amewahakikishia viongozi wa Makanisa kwamba, yuko pamoja nao na kuwataka kufanya kazi kwa kujiamini na kwa uhuru na ikiwa kama wanalo jambo lolote lile, wamjulishe na kwamba, atalishughulikia. Amewataka viongozi wa Makanisa kuwahubiria Watanzania amani, upendo na mshikamano pamoja na kuipenda nchi yao!

Katika mahojiano maalum na Vatican News baada ya Rais Magufuli kukutana na viongozi wa Makanisa nchini Tanzania, Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema, katika mkutano huu, mambo makuu manne yamejadiliwa kwa kina na mapana: Kwanza kabisa ilikuwa ni nafasi ya kujitambulisha kama viongozi wapya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; Pili kumshukuru kwa kuendelea kujenga mahusiano mema na Kanisa, tatu kumpongeza kwa ujasiri, ari na mwamko wa maendeleo nchini Tanzania na hatimaye, kuwasilisha rai ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, Askofu Kassala linampongeza Rais Magufuli kwa moyo wake wa uzalendo, ari na moyo mkuu wa kutaka kuwaletea watanzania maendeleo endelevu ambayo kwa namna ya pekee kabisa yanajionesha katika ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, vyombo vya usafiri pamoja na majengo ya huduma. Kanisa linampongeza Rais kwa kukuza na kudumisha nidhamu katika utumishi wa umma; mapambano kwa vitendo dhidi ya rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma, mambo ambayo yalianza kulitumbukiza taifa katika utovu wa nidhamu na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema.

Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kusimamia rasilimali za taifa na hasa madini ili faida inayopatikana, iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote. Wameipongeza Serikali kwa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, jambo ambalo linatoa fursa kwa watoto wengi kupata elimu, tayari kupambana na hali na mazingira yao. Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa maboresho makubwa katika huduma ya afya na ustawi wa jamii. Serikali ya awamu ya tano imeendelea kusimama kidete katika kutatua migogoro ya ardhi, ambayo ilikuwa ni kero kubwa ya kitaifa. Ikumbukwe kwamba, ardhi ni mtaji wa maskini, unaoweza kuwasaidia watanzania wengi kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao, kwa kuwekeza katika kilimo na makazi.

Askofu Kassala anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limewasilisha rai kwa serikali, ili kujenga jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi kuhusiana na masuala ya elimu, afya na ustawi wa jamii, ambayo, kwa hakika Kanisa limekuwa ni mdau mkuu. Kumbe, kabla ya Serikali haijatoa maamuzi ambayo yanaweza kuwa athari kwa huduma zinazotolewa na Kanisa, ni vyema, kukawa na utamaduni wa kujadiliana, ili kupima: matatizo, changamoto na mafanikio ya sera na mikakati kama hiyo. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kutoa huduma bora na makini kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Pale ambapo kuna maridhiano ya pande zote zinazohusika, kwa hakika hata utekelezaji wake utakuwa na ufanisi mkubwa.

Askofu Kassala anakaza kusema, uhusiano kati ya Serikali na Kanisa unafumbatwa katika huduma za kijamii, hususan: afya, elimu na ustawi wa jamii. Ndiyo maana, leo hii, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya mfumo rasmi wa elimu ulioanzishwa mjini Bagamoyo na Shirika la Roho Mtakatifu na matunda yake yakaanza kuonekana miaka mia moja baadaye, kwa shule za Kanisa kutoa viongozi wazalendo, waliojisadaka kwa ajili ya uhuru, ustawi na maendeleo ya watanzania wengi! Kati yao ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Askofu Kassala anasema, mazungumzo yao na Rais Magufuli yalikuwa katika hali ya utulivu, amani na maelewano kwani lengo ni kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Umekuwa ni muda wa kusikilizana na kuondoa shaka pale ilipojitokeza. Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza Maaskofu na kuwataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi. Anasema, si rahisi sana kuona mafanikio na kwamba, bado anahitaji watanzania kumsindikiza katika sala, ili daima aweze kumtanguliza Mungu katika maisha na maamuzi yake, kwani yanagusa watu wengi na hata wakati mwingine, yanabeba changamoto kubwa kwake binafsi na kwa taifa katika ujumla wake. Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Makanisa pamoja na taasisi zake katika sekta ya elimu na afya, kwa kutoa ruzuku kadiri ya Mkataba wa PPP “Public Private Partinership, yaani Mkataba wa Mahusiano Kati ya Taasisi za Umma na Sekta Binafsi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limempatia pole Rais Magufuli kufuatia ajali ya gari iliyopelekea Bwana Hamza Temba, Mwandishi wa Habari wa Wizara ya Utalii kupoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa vibaya, akiwemo Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Utalii ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu zaidi. Mwishoni, Askofu Flavian Matindi Kassala amekaza kusema, Kanisa litaendelea kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano mema na Serikali kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu za kitaifa na kimataifa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tayari limetangaza nia ya kuhamishia Makao makuu yake Dodoma na kwamba, Mkutano wa AMECEA kwa Mwaka 2022, Tanzania itakuwa ni mwenyeji wake.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

08 August 2018, 10:42