Tafuta

Vatican News
Papa Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na vijana wa Italia kwenye Uwanja wa Circo Massimo Papa Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na vijana wa Italia kwenye Uwanja wa Circo Massimo   (Vatican Media)

Papa Francisko awataka vijana kushuhudia imani katika matendo

Baba Mtakatifu katika tafakari yake amekazia: Shukrani kwa ushuhuda wa imani; umuhimu wa kutoka kwa haraka ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu; Ushuhuda wa imani ili kwa kuona waweze kuamini na kwamba, vijana wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Siku ya Vijana Italia, kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” ulioko mjini Roma, Jumamosi, tarehe 11 Agosti 2018 alianza kwa kutoa tafakari kama mwongozo wa mkesha huu kwa kukazia yafuatayo: Shukrani kwa ushuhuda wa imani; umuhimu wa kutoka kwa haraka ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu; Ushuhuda wa imani ili kwa kuona waweze kuamini na kwamba, vijana wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu ameishukuru familia ya Mungu nchini Italia na kwa namna ya pekee, vijana waliothubutu kufanya hija ya imani kwa kutembelea amana na utajiri unaofumbatwa katika utamaduni na maeneo matakatifu. Hii ni hija ambayo imewaonjesha furaha ya ndani, matatizo na changamoto za maisha na imani ya watu wa Mungu nchini Italia. Kuna umuhimu wa kutoka kwa haraka ili kwenda kushuhudia na kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kama alivyofanya Mtakatifu Maria Magdalena, Petro na Yohane na Bikira Maria aliyetoka kwa haraka kwenda kumsaidia binamu yake Elizabeth.

Waamini wanahamasishwa kutoka kwa haraka kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na matumaini kwa watu waliokata tamaa kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu baada ya kukumbana mubashara na Kashfa ya Msalaba, “wakanywea na kubaki wadogo sana”. Baba Mtakatifu anawaalika vijana pale wanapokumbana na vikwazo katika imani au imani yao inapoanza kuyeyuka kama ndoto ya mchana, wawe na ujasiri wa kumkimbilia Bikira Maria, Mama wa Kanisa, ili awafundishe, kwani anawaelewa na atawasaidia katika mchakato wa kupyaisha imani, ili kuwa na mwelekeo wa matumaini mapya katika maisha. Kamwe vijana wasiridhike na mafanikio waliyopata, bali wawe na ujasiri wa kuthubutu kuota ndoto, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu sanjari na kuwasaidia walimwengu kujenga dunia inayofumbatwa katika udugu.

Ushuhuda wa imani uwawezeshe vijana ili kwa kuona waweze kuamini. Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kujenga na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Wamtambue Kristo anayeteseka kati ya wagonja, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wawe na subira, wajenge utamaduni wa upendo na mshikamano, tayari kuthubutu kufanya hija katika umoja, inayowawezesha kushikamana kama watu wa Mungu na hivyo kuwa na uhakika wa maisha. Ubinafsi na uchoyo ni sumu ya maisha ya pamoja. Mtakatifu Petro katika Injili kuhusu Ufufuko wa Kristo aliingia kaburini, akaona na kuamini. Haya ndiyo yale yaliyojitokeza kwenye Arusi ya Kana, Yesu alipogeuza maji yakawa divai; alipowaponya wagonjwa na kuwalisha watu elfu tano, Neno la uzima na mkate ulioshuka kutoka mbinguni! Ni ushuhuda wa Yesu aliyemfufua Lazaro; ufunuo wa Uso wa Mungu asiyeonekana!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwani katika udhaifu wao wa kibinadamu, neema ya Mungu inaweza kuwainua na kuwakirimia matumaini mapya kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu baada ya kupata Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Ufufuko wa Kristo ni ushuhuda kwamba, kifo hakina sauti ya mwisho na hata katika mazingira kama haya ya kukatisha tamaa, bado Injili ya uhai inaweza kupeta na kung’ara. Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa kushinda dhambi na udhaifu wa binadamu. Fumbo la Pasaka lilileta mabadiliko makubwa katika maisha ya Mitume, hapa, ujasiri unatiliwa mkazo zaidi.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini ili kweli mwanga wa Kristo Mfufuka uweze kupenya katika maeneo yenye giza. Hii ndiyo changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapatia vijana wanaporejea majimboni mwao, huku wakitambua kwamba, kwa hakika wanapendwa na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Kwa njia hii, safari ya maisha inasonga mbele pasi na woga wala wasi wasi unaowakatisha tamaa vijana wengi. Vijana watoke kwa haraka kumwendea Kristo na kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao, huku wakiwa wamesheheni upendo, imani na furaha ya kweli!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

11 August 2018, 14:00