Papa Francisko akizungumza na Wayesuiti tarehe 01 Agosti 2018 Papa Francisko akizungumza na Wayesuiti tarehe 01 Agosti 2018 

Papa Francisko: Idadi ya vijana wasiokuwa na ajira inatisha na kukatisha tamaa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema Ili kukabiliana na changamoto za maisha, vijana wengi, wamejikuta wakitumbukia na kutumbukizwa katika utumwa mamboleo: ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na ngono za utalii; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe1 Agosti 2018 amekutana na Kikundi cha Wayesuit kutoka Barani Ulaya ambacho kiko katika majiundo endelevu kinachojadili kuhusu vijana, mawasiliano na miito kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu amekumbushia kwamba, enzi zao wakiwa bado majandokasisi walivyokuwa wanajitambulisha na kupendeza katika kanzu zao nyeusi, lakini leo hii mambo yamebadilika. Amegusia ushauri uliotolewa na Mwenyeheri Paulo VI kwenye mkutano mkuu  XXXII wa Shirika la Wayesuit na umuhimu wa kudumisha mchakato wa mawasiliano ndani ya Shirika la Wayesuit pamoja na watu wanalowahudumia.

Uhuru na umoja katika utofauti ni kati ya mambo ambayo yanawatambulisha Wayesuit katika maisha na utume wao, daima wakionesha utii katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ambazo wamekabidhiwa na Mama Kanisa. Baada ya tafakari na mang’amuzi ya kina, Wayesuit wanaweza kupanga na kuchagua utume wanaoweza kuutekeleza kwa ufanisi mkubwa, hali inayoonesha umoja katika utofauti! Mwenyeheri Paulo VI alipokuwa anawahutubia wajumbe wa Mkutano mkuu wa XXXII wa Shirika, baada ya kuona matatizo, changamoto na matumaini ya Wayesuit kwa siku za usoni, licha ya mashaka na wasi wasi wao, aliwataka Wayesuit kuwa na ujasiri wa kutoka kifua mbele kwenda kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu pembezoni mwa jamii.

Mwenyeheri Paulo VI alisema, huko ndiko mahali ambapo watakutana na kupambana na mawazo, matatizo na changamoto za shughuli za kichungaji zinazopaswa kuvaliwa njuga kwa utekelezaji makini. Changamoto hii, ikapewa kipaumbele cha pekee na Padre Pedro Arrupe, Mkuu wa Shirika la Wayesuit. Changamoto hii, imebaki kuwa ni urithi na amana kutoka kwake kwa ajili ya Shirika la Wayesuit. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ujasiri ni fadhila inayowaelekeza Wayesuit: kujitawala na kuishi maisha ya adili, changamoto inayohitaji kupaliliwa kwa njia ya sala na sadaka ya maisha, kwa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia fadhila hii.

Kuhusu changamoto ya mawasiliano, Baba Mtakatifu amewarejesha kwenye mbinu mkakati uliokuwa unatumiwa na Mtakatifu Pietro Favre, aliyekuwa anatoa kipaumbele cha kwanza kwa wengine na hatimaye, kujiundia mazingira na sanaa ya kusikiliza kwa makini. Haya pia ni mawasiliano aliyojijengea hata katika maisha ya sala na tafakari kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza ili aweze kuzungumza naye kutoka katika undani wa maisha yake. Baba Mtakatifu amewataka Wayesuit hawa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu pasi na kuogopa hata kidogo, daima wakijiaminisha kwa Kristo Yesu! Dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro si lele mama hata kidogo!

Wayesuti hawa wamemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko kwamba, changamoto kubwa mbele yao ni utume wa vijana na mawasiliano ya jamii na kwamba, huko wanao uwanja mpana zaidi wa kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wengi ambao kwa sasa licha ya kupata elimu ya juu kabisa, lakini, wanajikuta hawana fursa za ajira. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ukosefu wa fursa ya ajira ni tatizo na changamoto changamani kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anafanya rejea katika dhana ya kazi, kwa kukazia umuhimu wa elimu makini, huduma bora za afya na kazi inayojikita katika: uhuru, ubunifu, ushirikishwaji na mshikamano kama kielelezo makini cha utu na heshima ya binadamu, ulinzi na utetezi wa maisha. Kazi ni wajibu unaopaswa kukidhi mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ukweli katika upendo, kazi na maendeleo ya mwanadamu ni sawa na chanda na pete, kamwe hayawezi kutenganishwa, kwani yanalenga mafao ya wengi.

Bila kazi, mafao ya wengi na utu wao uko mashakani. Kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, vijana wengi wamejikuta wakihemea kwenye vituo vya Misaada vya Kanisa Katoliki. Jambo la msingi ni kujiuliza, Je, ni kwanini kuna umati mkubwa wa vijana ambao hawana fursa za kazi? Ukosefu wa fursa za kazi ni sehemu ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na sera chafu za fedha ambazo hazitoi kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu.

Kuna haja ya kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya: uchumi, utu na maisha ya kiroho; ili hatimaye, kujenga uchumi shirikishi unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa binadamu na wala si faida kubwa kwa watu wachache. Kwa makampuni kutaka kupata faida kubwa, fursa za ajira zitaendelea kupungua siku hadi siku duniani. Kipaji cha ubinifu, utu na heshima ya binadamu ni mambo muhimu sana katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Kutokana na ukosefu wa ajira, Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na ongezeko la vijana wanaokata tamaa ya maisha na hatimaye, kuishia kujinyonga. Kashfa hii bado inaendelea kufumbiwa macho na serikali nyingi kwa kutotoa taarifa kamili. Ili kukabiliana na changamoto za maisha, vijana wengi, wamejikuta wakitumbukia na kutumbukizwa katika utumwa mamboleo: ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na ngono za utalii; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Kuna wafanyabiashara na viwanda vinavyoendelea kushamiri kwa kutengeneza, kusambaza na kuuza dawa za kulevya. Kuna tatizo linaloendelea kukomaa la vijana kuwa wategemezi wa simu za viganjani; wengine wameishia hata kufanya maamuzi machungu kwa kujiunga na vikundi vya kigaidi na uhalifu wa kimataifa, kwani hawaoni tena thamani ya maisha. Utume wa vijana ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwafahamu vijana, changamoto, matatizo na matarajio yao ya siku za usoni. Vijana wanahitaji maneno na ushuhuda wa kinabii; wanahitaji majibu muafaka ili waweze kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Kumbe, sera na mchakato wa mawasiliano, uiwezeshe mihimili ya uinjilishaji kung’amua mbinu mkakati utakaowasaidia vijana kuwa tena na matumaini ya leo na kesho iliyo bora pasi na kukata tamaa ya maisha! Wayesuit hawa ambao wamekuwa wakikutana tangu tarehe 23 Julai, wanatarajia kumaliza semina hii hapo tarehe 18 Agosti 2018.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

 

02 August 2018, 14:02