Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akizungumza na wanafamilia Papa Francisko akizungumza na wanafamilia  (Vatican Media)

Papa Francisko: Tangazeni Injili ya familia na upendo wa Mungu!

Chama cha kitume cha "Knights of Columbus" kinaendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika umoja, upendo, udugu na mshikamano wa dhati, kwa njia ya majiundo makini yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Chama cha Kitume cha "Knights of Columbus" kwa kujisadaka kwa ajili ya kukuza na kudumisha upendo na mshikamano kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma huko Mashariki ya Kati sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika tunu msingi za kifamilia. Baba Mtakatifu ametuma ujumbe huu kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa 136 wa Chama cha Kitume cha "Knights of Columbus" waliokuwa wanakutana tangu tarehe 7 – 9 Agosti 2018 katika Jimbo kuu la Baltimore, nchini Marekani.

Hiki ni chama ambacho kina utirhi wa utajiri wa historia ya miaka mia mbili tangu kuanzishwa kwake na Mtumishi wa Mungu Padre Michael McGivney na kwa wakati huu kinatekeleza maisha na utume wake sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano wa mwaka huu, umeongozwa na kauli mbiu “Wajumbe na mashuhuda wa upendo”. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anawapongeza wanachama kwa kuendelea kuwa waaminifu katika kutangaza na kumwilisha Injili ya upendo, kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Hiki ni chama ambacho kinaendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika umoja, upendo, udugu na mshikamano wa dhati, kwa njia ya majiundo makini yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. Wanachama wake wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa kusaidiana kwa hali na mali, wakati wa raha na shida, changamoto endelevu hata kwa walimwengu wa nyakati hizi, anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kupendana, kusaidiana na kuwajibikiana, kama ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu, chemchemi ya utakatifu wa maisha. Huu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, changamoto ambayo Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuivalia njuga na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Kumbe, sala na imani ni mambo yanayopaswa kumwilishwa katika matendo, kama ushuhuda wa upendo wenye mvuto na mashiko; mshikamano wa upendo na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa "Knights of Columbus" kwa ushuhuda wanaotekeleza katika hali ya unyenyekevu, kielelezo cha Mwenyezi Mungu anayejishusha kama kielelezo cha huruma na upendo kwa watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Chama hiki kimekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera na mipango yake, inayojikita katika kipaji cha ubunifu ili kupambana na baa la umaskini unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kuwekeza zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Siku ya IX ya Familia Duniani inayoadhimishwa katika Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 21- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Maandalizi haya yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema familia ni hospitali iliyoko karibu nawe na ni huduma ya kwanza yenye mvuto na mashiko. Familia ni kiini cha upendo, umoja na ukarimu. Familia ni shule ya kwanza ya imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, familia ni makazi maalum ya wazee na wagonjwa. Familia ina tunu na changamoto zake hasa katika ulimwengu mamboleo ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwatia moyo wanachama wote, ili waendelee kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya familia inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, daima, wakiendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawapongeza kwa namna ya pekee kwa mchango wao katika kuwasaidia na kuwahudumia Wakristo huko Mashariki ya Kati, wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma. Anawasihi waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu; toba na wongofu wa ndani, ili kweli majadiliano katika ukweli na uwazi, yasaidie kuleta suluhu na amani ya kudumu huko Mashariki ya kati!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

10 August 2018, 14:56