Cerca

Vatican News
Papa Francisko wakati wa Katekesi yake, Kila Jumatano. Papa Francisko wakati wa katekesi yake, kila Jumatano.  (AFP or licensors)

Papa Francisko azungumzia kuhusu: China, Wakimbizi na Mageuzi ndani ya Kanisa

Baba Mtakatifu katika mahojiano maalum na REUTERS amedadavua kwa ufanisi mahusiano kati ya Vatican na China, wimbi la Wahamiaji, kashfa za dhuluma ya ngono dhidi ya watoto wadogo kwa Kanisa nchini Chile na mabadiliko katika Mabaraza, Tume, Taasisi, na Ofisi za Kipapa.

Na Padre Celestine Nyanda. – Vatican.

Shirika la habari la Reuters, tarehe 1 Julai 2018, limefanya mahojiano na Baba Mtakatifu Francisko. Katika mahojiano hayo, Baba Mtakatifu amedadavua kwa ufanisi mahusiano kati ya Vatican na China, wimbi la Wahamiaji, kashfa za dhuluma ya ngono dhidi ya watoto wadogo kwa Kanisa nchini Chile na mabadiliko katika Mabaraza, Tume, Taasisi, na Ofisi za Kipapa.

Mahusainao kati ya Vatican na China yanazidi kukua siku hadi siku na matumaini yapo makubwa sana kwa siku za usoni kuwa bora zaidi. Kuna mahusiano ya kidiplomasia ambapo Ujumbe wa China hufika Roma kwa mikutano na baadae Ujumbe wa Vatican huenda China katika mazungumzano ya kujenga. Kuna pia mahusiano ya wote katika yote, yaani mahusaino yasiyo rasimi kati ya viongozi, ndugu na jamaa wa pande zote mbili za Vatican na China. Kisha kuna mahusiano ya tamaduni, mila na desturi, mfano maonesho yaliyofanyika mjini Vatican na baadae nchini China kuhusu utajiri wa kihistoria kwa pande zote mbili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, taifa na watu wa China wana fadhila ya subira na busara, ndio sababu baadhi ya watu wanadhani kana kwamba mambo yanaenda pole pole sana. Lakini ukweli ni kwamba, huu ni utajiri wa tamaduni unaopaswa kuzingatiwa katika mahusiano hayo, na kwa hakika watu wa China wanastahili kutunukiwa Tuzo ya subira.

Katika mabadiliko ya Ofisi za Kipapa, Baba Mtakatifu Francisko anakiri wazi kwamba ni kazi inayohitaji muda na ni endelevu katika historia ya Ofisi hizo. Anakiri pia kwamba kuna hitaji la kuwa na usawa wa kutosha wa jinsia kwa kuongeza wanawake kushikiria nafasi za juu katika baadhi ya Ofisi zisizohitaji mamlaka ya Daraja Takatifu ya Upadre. Hata hivyo ameweka wazi kwamba suala la kupadirisha wanawake lisifikiriwe kabisa sababu ni kinyume cha Mafundisho Tanzu ya Kanisa, na watangulizi wake Mtakatifu Yohane Paulo II na Benedikto XVI walishafafanua na kuufunga mjadala huo naye Papa Francisko haoini sababu za kuufungua tena.

Baba Mtakatifu Francisko ametoa tahadhari kutokuwa na mtazamo wa utendaji kijinsia, bali mtazamo wa utu na thamani ya mwanamke. Itakumbukwa kwamba Baba Mtakatifu mwaka 2016 alimteua Bi Paloma Garcia Ovejero kuwa Msemaji mkuu msaidizi wa Vatican, kisha mnamo mwezi Novemba 2017 aliwateua wanawake wawili kuwa ni makatibu wasaidizi katika Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, nao ni Bi Gabriella Gambino na Bi Linda Ghisoni. Mtazamo wa Baba Mtakatifu kuhusu hulka na vipaji vya wanawake ni kwamba, wana uwezo tofauti na wenye ubora wa kuelewa mambo, wana mtazamo tofauti wa maisha na wana mtindo tofauti wa kutatua migogoro na matatizo. Ingawa watu kadhaa wamekuwa wakisema kwamba kutakuwa na umbea sana kwenye Ofisi za Vatican wakiwemo wanawake wengi, Baba anasema, hata wanaume wapo wambea pia.

Mwaliko ni ule wa kuwa na Kanisa linalotoka ili kukutana na watu hata kama kuna hatari za kupata ajali katika hija hiyo, ni bora zaidi kuliko Kanisa lililojifungia sababu litaishia kuugua. Pamoja na hitaji la mabadiliko na maboresho, Papa Francisko amewakumbuka watendaji wengi wa Vatican wenye kushuhudia utakatifu wa maisha katika utendaji wao wa kila siku. Wamekuwepo siku zote watendaji wa namna hiyo na hawajioneshi wala kujivuna. Huu ni mfano bora wa kuigwa.

Kufuatia dhuluma na nyanyaso za ngono, kashifa iliyoibuka tena kwa Kanisa nchini Chile, Baba Mtakatifu Francisko hafichi maumivu aliyonayo kwa tukio hilo. Hakupenda sana kulizungumzia suala hilo, kwani takwimu zinaonesha kwamba dhuluma na nyanyaso nyingi za ngono nchini humo, zimekua zikifanyika katika familia, katika mitaa ya makazi ya watu, mashuleni na hata kwenye maeneo ya mazoezi wanakopelekwa watoto, hata hivyo Kanisani pia kumekuwepo na dhuluma na nyanyaso za ngono dhidi ya watoto wadogo.

Haidhuru hata kama takwimu zitaonesha kanisani ni chache kuliko sehemu zingine, kwani hata kama angekuwa ni padri mmoja tu aliyefanya hivyo kwa mtoto mmoja, anakuwa kafanya kosa kubwa sana la kumpotezea njia ya matumaini mtoto huyo na familia yake katika hija ya kumtafuta Mungu. Padre ni Baba na mchungaji, anayepaswa kuonesha kondoo njia ya kwenda kwa Mungu Baba, kwenye malisho ya majani mabichi, na sio kuwapoteza wanakondoo hao.

Inaonekana nchini Chile kumekuwa na historia ndefu ya madonda na maumivu makali ya dhuluma na nyanyaso za ngono dhidi ya watoto wadogo. Baada ya hija yake ya kitume nchini Chile mnamo mwezi Januari 2018, Baba Mtakatifu Francisko alimtuma Askofu mkuu Charles Scicluna wa Malta, aliyebobea katika uchunguzi wa nyanyaso za ngono dhidi ya watoto wadogo, kwenda nchini Chile na Marekani waliko wahanga wa nyanyaso hizo ili kuupata ukweli. Taarifa yake ya kurasa 2,300 kutoka kwa mashahidi 64, ilimsononesha sana Baba Mtakatifu kwa yaliyokuwamo, na hivyo akaamua kuwaita maaskofu wote wa Chile ili kuzungumzana. Tukio hili lilifuatiwa na nyakati za sala na baadae maaskofu wote wa Chile kuomba kujiudhuru kufuatia ugumu wa kesi zilizopatikana sehemu mbali mbali.

Mpaka sasa Baba Mtakatifu karidhia kujiudhuru kwa maaskofu watatu, inawezekana akaridhia tena kwa baadhi yao na hasa kwa sababu za umri. Hata hivyo yupo mwingine ambaye Baba Mtatakifu amependekeza apewe kwanza nafasi ya kujitetea kisheria katika mahakama za Kanisa. Taifa la Chile ambalo lilikuwa na asilimia 70% ya wakristo sasa idadi imepungua na kubakia asilimia 40%. Kwa masikitiko makubwa Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kazi ya shetani kulivuruga Kanisa nchini humo na duniani kote. Kwani matukio ya namna hii yalianza nyakati za Mtakatifu Yohane Paulo II kwa tuhuma zilizoibuka Boston, nchini Marekani na baadae wakati wa Papa Benedikto XVI kwa kashifa zilizoibuka nchini Ireland.  

Wimbi la wahamiaji limekuwa maumivu ya kichwa kwa mataifa na watu wengi duniani kwa miaka ya hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko anatambua ugumu na changamoto zilizopo katika kutafuta suluhu ya kudumu ya suala hili. Hata hivyo anasikitishwa na baadhi ya nchi kukwepa kushirikiana na wengine katika kukabiliana na changamoto hii. Kazipongeza nchi kama Italia, Yordani, Uturuki, Lebanon, Ugiriki na Ujerumani zinavyojitahidi kulihangaikia suala hili. Hata hivyo bado anasikitishwa na baadhi ya tabia, mfano nchi ya Italia ilipoikatalia Meli ya Aquarius kutua nanga na hivyo kulazimika kwenda Uhispania ikiwa na wahamiaji 629.

Anasikitika uamuzi wa Rais Trump kwanza kabisa kuwazuia wahamiaji kutoka Mexico kuingia nchini Marekani, baadae kuwatenganisha watoto wadogo 2000 na familia zao jambo ambalo sio la kiutu hata kidogo, lakini pia anasikitishwa na uamuzi wa Rais huyo kuitoa nchi yake Marekani kwenye makubaliano ya Paris kuhusu kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi, pia kurudi kwake nyuma baada ya hatua iliyokuwa imepigwa na Rais Barack Obama katika majadiliano na mahusiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba.

Kuhusu suala la Wahamiaji, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bara la Afrika lisichukuliwe kuwa ni eneo la kwenda kunyonya na kupora mali, bali ni Bara la kwenda kuwekeza katika elimu na shughuli zingine za maendeleo ili kuepuka wimbi la Wahamiaji. Katikia hili, Baba Mtakatifu Francisko anampongeza sana Chansela Angela Merkel kwa utayari wake.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

08 August 2018, 08:12