Katekesi ya Papa Francisko, tarehe 8 Agosti 2018 Katekesi ya Papa Francisko, tarehe 8 Agosti 2018 

Utupu wa binadamu ni mahali pa kukutana na nguvu ya Mungu inayo okoa!

Baba Mtakatifu Francisko asema,jangwa la maisha ya binadamu au udhaifu na mapungufu ya binadamu ni mahali pa kukutana na huruma, upendo na nguvu ya Mungu inayomwokoa mwamini na kishawishi cha kuabudu miungu vitu na watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Mungu aliye hai ni chanzo cha maisha ya uzima wa milele na ndiye anayepanga na kuratibu historia ya maisha ya mwanadamu. Ibada za miungu hazihusu tu ibada potofu za kipagani. Zinabaki kuwa kishawishi cha kudumu cha imani. Ibada za miungu ni kufanya mungu kile ambacho si Mungu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 8 Agosti 2018 ameendelea kudadavua kuhusu Amri za Mungu kwa kujikita zaidi katika kuabudu miungu na kwa namna ya pekee, jinsi ambavyo Waisraeli walimwasi Mwenyezi Mungu kwa kuabudu Ndama ya dhahabu, huko jangwani, mahali ambapo watu hawa walikuwa wanamsubiri Musa aliyekuwa amepanda mlimani kupokea Amri na Maagizo ya Mungu.

Jangwani ni mahali pa mapambano anasema Baba Mtakatifu, kwani hapa kunakosekana mahitaji msingi ya binadamu kama vile: maji, chakula na malazi. Hiki ni kielelezo cha maisha ya kila siku na kwamba, mwanadamu hawezi kupata mahitaji yote katika maisha hali ambayo inawajengea watu hofu na wasi wasi wa maisha kuhusu chakula, kinywaji na mavazi; mambo ambayo hata Yesu mwenyewe ameyagusia katika Injili. Jangwa la maisha ya binadamu ni chanzo cha hofu na mashaka ya mambo yote haya.

Musa baada ya kupanda mlimani na kukaa huko kwa muda wa siku arobaini, watu walianza kukata tamaa na kuona hofu juu ya hatima ya maisha yao kwa siku za usoni. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, walikuwa hawana tena kiongozi wa kufanyia rejea, kwani kwao, Musa alikuwa ni kiongozi aliyewahakikishia usalama wa maisha, ndiyo maana, watu wakataka kuwa na mungu wanayemwona, wakamgusa na kutembea pamoja naye. Ili kuridhisha utupu wa maisha yao ya ndani, Waisraeli wakamwomba Haruni awatengenezee mungu, lakini kwa bahati mbaya iliyoje, huyu mungu wao kama anavyosema Mzaburi, sanamu zao ni fedha na dhahabu zina vinywa lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, miungu hii inajiweka mbele ya watu na kutaka ipewe kipaumbele cha kwanza na kuabudiwa, lakini, ikumbukwe kwamba, hii ni kazi ya mikono yao! Haruni akawatengenezea Ndama wa dhahabu kielelezo cha nguvu na ufanisi katika maisha. Dhahabu ni alama ya utajiri, ufanisi, nguvu na fedha. Hata leo hii miungu hawa wanajionesha kwa njia ya mafanikio, madaraka na fedha. Hivi ni vishawishi ambavyo vinaendelea kumwanadama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kiasi cha kumchanganya, kumpotezea dira na mwelekeo wa maisha na hatimaye, kumgeuza kuwa mtumwa wa vitu!

Yote haya ni matokeo ya binadamu kutokuwa na imani mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kumfanya kuwa ni kinga na nguzo ya maisha! Mwamini anayemtumaini Mungu anakuwa na ujasiri wakati wa magumu na mahangaiko ya ndani. Bila ya Mwenyezi Mungu kupewa kipaumbele cha kwanza, kuna hatari kubwa ya kuteleza na kuanguka katika dhambi ya kuabudu miungu vitu! Katika mchakato wa kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwamini Misri, Mwenyezi Mungu alitenda miujiza na kuwaonesha huruma na upendo wake wa dhati! Lakini ilikuwa ni kazi ngumu sana kuondoa tabia ya kuabudu miungu vitu kutoka katika nyoyo za Waisraeli. Hii ni changamoto endelevu hata kwa waamini wa nyakati hizi. Umefika wakati wa kuondokana na “makapu ya nyama na vitunguu swaumu ambayo yamekita mizizi katika akili na nyoyo za watu, kiasi cha kuwageuza kuwa watumwa wa kuabudu miungu vitu!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumpokea na kujiaminisha kwa Kristo Yesu, kwa njia ya neema alivyojifanya kuwa maskini kwa ajili ya yao, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, wao wapate kuwa matajiri katika umaskini wake. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni changamoto ya kujiaminisha mbele ya Mungu ambaye ana nguvu na uweza, kwani wanapokuwa dhaifu hapo ndipo wanapokuwa na nguvu kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo. Uhuru wa mwanadamu unajionesha pale ambapo anatoa nafasi ya kwanza kwa Mungu aliye kweli, kiasi hata cha kuweza kupokea udhaifu na mapungufu ya kibinadamu, ili hatimaye, kufutilia mbali miungu vitu inayotaka kutawala nyoyo za watu.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kumwinulia macho yao Kristo Yesu pale juu Msalabani, anakoteseka na kuhangaika; akashutumiwa na kutemewa mate, kiasi hata cha kuvuliwa utu na heshima yake. Lakini, kwa bahati iliyoje, katika mazingira yote haya, Kristo Yesu anaufunua Uso wa Mungu wa kweli; utukufu wa huruma na upendo wa Mungu usiodanganya kamwe. Nabii Isaya anasema alijeruhiwa kwa makosa yetu, akachubuliwa kwa maovu yetu, ili kuwafungulia binadamu njia ya wokovu wa Mungu.

Uponyaji wa binadamu unabubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyejifanya kuwa maskini, akaonekana kana kwamba, ameshindwa katika yote, ili kuwajaza na kuwakirimia binadamu nguvu na upendo wake usiokuwa na kifani. Kristo Yesu anawafunulia watu ubaba wa Mungu na kwamba, kwa njia ya Kristo Yesu, udhaifu wa binadamu si tena laana, bali mahali muafaka pa kukutana na Mwenyezi Mungu, chemchemi ya nguvu itokayo juu.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

08 August 2018, 12:01