Tafuta

Ibada ya Mazishi ya Mwenyeheri Paulo Vi tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican. Ibada ya Mazishi ya Mwenyeheri Paulo Vi tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican. 

Mwenyeheri Paulo VI alilipenda Kanisa, sasa analiombea mbinguni

Papa Paulo VI Aliliongoza Kanisa kati ya mwaka 1963 - 1978, wakati wa kumwilisha maazimio ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kiongozi aliyekazia umuhimu wa Katekesi kama chombo cha: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Alisimamia mageuzi ya maadhimisho ya Liturujia, ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na mwanadamu kupata wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 5 Agosti 2018 amesema, katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Kanisa  kwa mwaka huu, 2018, linafanya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipofariki dunia akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Itakumbukwa kwamba, alitangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 19 Oktoba 2014 na Baba Mtakatifu Francisko.

Mwenyeheri Paulo VI, alizaliwa kunako mwaka 1897 huko Concesio, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Mei 1920 na hatimaye, kuteuliwa na kuwekwa wakfu kama Askofu mwaka 1954. Kanisa kwa sasa linajiandaa kumtangaza Mwenyeheri Paulo VI hapo tarehe 14 Oktoba 2018, kuwa Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko, anamwomba Mwenyeheri Paulo VI  huko mbinguni aendelee kuliombea Kanisa alilolipenda upeo na kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Injili ya amani duniani na kwa hakika ni Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa nyakati hizi. Mwenyeheri Paulo VI atatangazwa kuwa Mtakatifu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.

Sinodi ni chombo kilichoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1965 kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwashirikisha watu wa Mungu katika mchakato wa kupanga, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, dhana ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kulihamasisha Kanisa kwa nyakati hizi, kuivalia njuga kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Aliliongoza Kanisa la Kristo kati ya mwaka 1963 hadi mwaka 1978, wakati wa kumwilisha maazimio ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kiongozi aliyekazia umuhimu wa Katekesi makini kama chombo cha: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Alisimamia mageuzi ya maadhimisho ya Liturujia, ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa vyema na mwanadamu kupata wokovu. Alisisitizia sana majiundo awali na endelevu ya wakleri, ili kweli Kanisa liweze kupata watenda kazi watakatifu, wachamungu na wachapa kazi kweli kweli.

Ni kiongozi aliyesimamia kwa nguvu zote: utu, heshima na haki msingi za binadamu, akajisadaka ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linakuwa kweli ni chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Akasimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kiasi hata cha kubaki pweke ndani na nje ya Kanisa, lakini daima akaendelea kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, Kristo na Kanisa lake. Akakazia majadiliano ya kiekumene na kidini, akaanzisha safari za kitume, ili kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo. Ni kiongozi aliyechakarika kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Antonio Marrazo anayesimamia mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Paulo VI kuwa Mtakatifu anakaza kusema, amana na ujumbe wa Mwenyeheri Paulo VI ni: Uhai, utu na heshima ya binadamu inayofumbatwa katika utamaduni wa upendo, haki na amani duniani. Kanisa mwaka huu 2018 limeadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”.

Ni waraka unaopembua kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Anahimiza: wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Huu ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia.

Mwenyeheri Paulo VI aliamini na kushuhudia kwamba, ujenzi wa amani duniani unafumbatwa katika diplomasia, sanaa na majadiliano katika: haki, ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kutokana na ushuhuda wa maisha na utume wake, Kanisa linataka kumweka mbele ya macho ya waamini kama kielelezo na mfano bora wa kuigwa. Alipenda kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa kukazia umuhimu wa ujenzi wa Jumuiya inayo amini, ili kumtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

05 August 2018, 08:29