Tafuta

Vatican News
Sala ya Malaika wa Bwana wakati wa Sherehe ya Kung'ara Bwana. Sala ya Malaika wa Bwana wakati wa Sherehe ya Kung'ara Bwana.  (ANSA)

Mahubiri ya Papa Paulo VI katika Sherehe ya Kung'ara Bwana, 1978

Tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya mashuhuda linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Huu ni ukamilifu wa Sheria na Unabii katika Fumbo la Pasaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Kung’ara kwa Kristo Yesu inaangaza nuru ya ajabu katika maisha ya kila siku ili kufukuzia mbali giza la kifo linalosumbua akili ya mwanadamu. Mlimani Tabor, Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake. Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Hapa Yesu anadhihirisha utukufu wa Fumbo la Pasaka, kielelezo makini cha sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kustahilishwa kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Mwili uliotukuka mbele ya Mitume wa Yesu ni mwili wa Kristo na kwamba, hata mwili wa binadamu utapata urithi wa mwanga wa uzima wa milele, kwa kushiriki katika utukufu na kwa njia hii wapate kushiriki tabia ya Uungu kwa kuokolewa na uharibifu ulioko duniani kwa sababu ya tamaa.

Hii ni sehemu ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, iliyokuwa imeandaliwa na Mwenyeheri Paulo VI kwa ajili ya Sherehe ya Kung’ara kwa Yesu, tarehe 6 Agosti 1978, lakini kutokana na homa kali iliyomshika siku hiyo, hakuweza kutokeza mbele ya waamini na matokeo yake, jioni akafariki dunia katika amani. Mwenyeheri Paulo VI anakaza kusema, waamini wanasubiri kushirikishwa utukufu wa Mungu ambao walianza kuutafuta kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kipindi cha likizo ya kiangazi, ni wakati muafaka wa kutafakari mambo msingi ya imani sanjari na kujikita katika mchakato wa kupyaisha na kukomaza tunu msingi za maisha ya kiroho.

Mwenyeheri Paulo VI katika tafakari yake, aliwakumbuka hata wale ambao kutokana na sababu mbali mbali walikuwa wanateseka, ili nao, hata katika hali na mazingira kama haya waweze kupata walau mwanya wa mapumziko. Hawa ndio wale watu wasiokuwa na fursa za ajira, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu katika familia na jamii zao: Watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa sehemu mbali mbali za dunia pamoja na wale wote walioathirika kutokana na sera na mikakati ya uchumi na maendeleo jamii. Kutokana na mahitaji msingi ya umati wote huu, Kanisa linapenda kumtolea Bikira Maria sala na maombi yake, ili aweze kusaidia kuombea umoja, udugu na mshikamano wa dhati; mwishoni, akawaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

 

 

06 August 2018, 14:03