Cerca

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na vijana wa Italia. Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na vijana wa Italia.  (Vatican Media)

Mfahamu Mtakatifu Petro, Dibaji na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Mwandishi, anatusimulia na kutufafanulia simuli zinazomuhusu Mtakatifu Petro, kama zilivyowasilishwa katika Injili nne. Anatuonyesha kuwa ingawa wanatofautiana, waandishi wa simulizi za Mtakatifu Petro, hawaandiki uongo, kila mmoja aliandika katika mazingira yake, nyakati zake, hadhira yake, na kwa lengo la kutaka watu wake wajifunze kitu kutokana na maisha ya Mtakatifu Petro.

Na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. - Dar es Salaam.

DIBAJI: Ukiwauliza Wakristo wote duniani, watakwambia wanamfahamu Mtakatifu Petro. Na kwamba habari zake wamezisoma katika Biblia Takatifu na hasa kwenye Injili za Matayo, Marko, Luka na Yohane. Jibu hili si la kushangaza kwani mtakatifu huyu, ndiye kiongozi wa kwanza wa Kanisa na Mtume wa Bwana wetu Yesu Kristo. ukiendelea kuuliza zaidi, utapata simulizi zinazotofautiana kuhusu Mt. Petro. Kwani, hata katika Injili hizi nne, amesimuliwa kwa namna mbalimbali. Swali kubwa hapa ni kwa nini kuwe na masimulizi tofauti juu ya mtu yuleyule? Swali hili, linazaa swali lingine muhimu: masimulizi haya ni uongo au ukweli unaosimuliwa na watu tofauti, nyakati tofauti na mazingira tofauti? mazingira tofauti?

Mwandishi wa kitabu hiki cha MFAHAMU MTAKATIFU PETRO, anajibu maswali haya na kufafanua zaidi juu ya utata huu unajitokeza daima kwenye maandishi na simulizi mbali mbali katika historia ya mwanadamu, na hasa katika historia ya Kanisa. Ni dhahiri kwamba matukio mengi katika historia ya mwanadamu yamekuwa yakisimuliwa kwa namna mbali mbali. Tukio moja linaweza kuwa na simulizi mbalimbali, kutegeana na msimuliaji, hadhira, nyakati, mazingira na lengo la masimulizi yenyewe.

Kwa mfano ikitokea ajali mahali fulani, wanahabari wanaweza kuhitilafiana sana katika kuwahabarisha wasomaji, au wasikilizaji wao. Kama gari lililosababisa ajali ni Toyota, lakini magari mengi katika jamii husika, ni aina ya Benz, anaweza kusema gari aina ya Benz ndilo lilohusika, vile vile, anaweza kusema wamekufa watu ishirini, badala ya kumi, kwa kuwahesabu na waliozimia au kuonekana wamelala eneo la tukio. Pia, idadi inaweza kuongezwa ili kuwafanya wasomaji waogope ajali, na kuwa makini barabarani. Ukweli ni kwamba tukio hili la ajali linasimuliwa tofauti kulingana na mazingira, lengo, na macho ya shuhuda.

Bila shaka, mantiki ya msingi ya tukio lolote lile katika historia, si kuchambua ili kubaini simulizi lipi ni la uongo na lipi ni sahihi, bali ni kutambua uhalisia wa tukio lenyewe na mafunzo yanayotokana na tukio hilo. Hivyo, mantiki ya mfano wa ajali tuliouona juu, ni kwamba ajali hutokea, na kwamba tuwe makini barabarani. Kwa kuzingatia msingi huu Mwandishi, anatusimulia na kutufafanulia simuli zinazomuhusu Mtakatifu Petro, kama zilivyowasilishwa katika Injili nne. Anatuonyesha kuwa ingawa wanatofautiana, waandishi wa simulizi za Mtakatifu Petro, hawaandiki uongo, kila mmoja aliandika katika mazingira yake, nyakati zake, hadhira yake, na kwa lengo la kutaka watu wake wajifunze kitu kutokana na maisha ya Mtakatifu Petro.

Tumpongeze Mwandishi, kwa kazi njema inayolenga kuimarisha imani zetu kwa kufanya tufahamu kwa kina misingi ya Kanisa letu, kupitia maisha na utume wa Mtakatifu Petro. Tunawaomba Watanzania wakitafute kitabu hiki na kukisoma na Bwana wetu awajalie neema ya kulifahamu zaidi Neno lake, kwa ajili ya afya ya roho zetu. Amina.

 

14 August 2018, 17:28