Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella akisalimiana na Papa Francisko Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella akisalimiana na Papa Francisko 

Kufutwa kwa adhabu ya kifo ni mwendelezo wa Mafundisho ya Kanisa

Kufutwa kwa adhabu ya kifo ni mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho yaliyotolewa na: Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Yohane Paulo II na hata Mwenyeheri Paulo VI katika nyaraka na nyakati mbali mbali. Kwa mabadiliko haya, Baba Mtakatifu Francisko anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima na binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbali mbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia: njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameendelea kuwa mstari wa mbele kupinga utamaduni wa kifo, unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee kwa binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni  mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho yaliyotolewa na watangulizi wake, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Yohane Paulo II na hata Mwenyeheri Paulo VI katika nyaraka na nyakati mbali mbali. Kwa mabadiliko haya, Baba Mtakatifu Francisko anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima na binadamu.

Ikumbukwe kwamba, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala. Kwa mara ya kwanza ilichapishwa kunako mwaka 1992 na kufanyiwa marekebisho kunako mwaka 1997 “Editio typica” iliyorekebisha kuhusu adhabu ya kifo kwa kusoma alama za nyakati! Lengo ni kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Hii ni amana ya imani ya Kanisa Katoliki mintarafu mwanga wa Injili.

Adhabu hii ni kielelezo cha ukatili wa hali ya juu kabisa na wala haiwezi kukubalika tena, kwani inakwenda kinyume cha mwanga wa Injili. Hii ni changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali kujizatiti katika kulinda, kutunza na kudumisha uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa nchi zile ambazo bado zinaendekeza adhabu ya kifo, sasa ni wakati wa kutafuta adhabu mbadala, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwarithisha vijana wa kizazi kipya.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo maendeleo makubwa juu ya tafsiri na uelewa wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu utu na heshima ya binadamu kadiri ya mwanga wa Injili, hali ambayo imepelekea hata Baba Mtakatifu Francisko kuamua kufanya mabadiliko kwenye kifungu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki kinachofuta adhabu ya kifo kama sehemu ya Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu katika mawazo yake kuhusu adhabu ya kifo anakazia umuhimu wa kulinda uhai wa binadamu na kuuendeleza, changamoto na mwaliko wa kuleta mwono na mwelekeo mpya kuhusu: maisha, utu na heshima ya binadamu. Hii ni hatua kubwa na muhimu katika kutafsiri Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa kadiri ya Mwanga wa Injili na kwa kusoma alama za nyakati.

Kanisa anasema Askofu mkuu Fisichella, linatambua uchungu wa watu walioguswa na kutikiswa na matukio ambayo yamepelekea adhabu ya kifo kwa wahusika, lakini, Kanisa linavitaka vyombo vya sheria kutenda haki na kuwajibika barabara badala ya kuendeleza chuki, uhasama pamoja na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa njia ya adhabu ya kifo. Kanisa linayasema yote haya kwa kutoa fursa kwa wale waliotenda makosa kama haya yanayostahili kupewa adhabu ya kifo, kupata muda wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; tayari kuanza kuandika ukurasa mpya kwa kujivika utu mpya na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Toba na wongofu wa ndani; msamaha, upatanisho na haki ni mambo msingi yanayozingatiwa na Mama Kanisa katika mchakato wa kufutilia mbali adhabu ya kifo. Hii ni hatua mpya katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na familia inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mauaji ya aina yoyote ile ni jambo ambalo haliwezi kukubalika katika mwanga wa Injili.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuitumia Katekisimu ya Kanisa Katoliki kama kitabu cha rejea katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala. Hiki ni chombo muhimu sana katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Katekesimu itawawezesha waamini kuzama kwa kina katika Mapokeo ya Kanisa, ili hatimaye, waweze kuwa tayari kuitangaza na kuishuhudia katika medani mbali mbali za maisha na wala kisiwe ni kitabu kinachoelea kwenye ombwe na fikira za binadamu!

Mama Kanisa nataka kutangaza na kushuhudia mbiu ya wokovu, ili kwa kusikia watu waweze kusadiki, na kwa kusadiki waweze kutumaini na kwa kutumaini, waweze kupenda. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema,  kwa njia ya ufunuo, ukweli kamili juu ya Mwenyezi Mungu na juu ya wokovu wa mwanadamu unang’ara kwa binadamu katika Kristo Yesu, ambaye Yeye mwenyewe ndiye mshenga na utimilifu wa ufunuo wote.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

04 August 2018, 14:59