Vatican News
Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. 

Baada ya miaka 110: Uingereza kuandamana na Ekaristi, Sept. 2018

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, baada ya kupita miaka 110 tangu waamini wa Kanisa Katoliki walipofanya maandamano ya Ekaristi, kuanzia tarehe 7-9 Septemba, 2018, Kanisa Katoliki nchini Uingereza linaadhimisha Kongamano na Hija ya Ekaristi Takatifu, inayoongozwa na kauli mbiu “ Adoremus – Liverpool 2018” yaani “Tunakuabudu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo, ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu anayejitoa mwenyewe kama: Kuhani, Altare na Sadaka ili kuwafunulia watu wa Mungu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Huu ndio upendo unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Ekaristi Takatifu ni chakula cha kweli kilichoshuka kutoka mbinguni!

Ni Fumbo la imani linalopaswa kusadikiwa, kuadhimishwa na kumwilishwa katika huduma ya upendo, udugu na mshikamano; hasa na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani Ekaristi Takatifu ni shule ya umoja, upendo na ukarimu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya maisha mapya inayowawezesha waamini kushiriki uhai wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kujenga na kudumisha Agano Jipya na la milele linalofungwa kwa njia ya Damu Azizi ya Mwanakondoo wa Mungu.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni kielelezo makini cha umoja wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu na kwa uelewa mpana maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha yao na kamwe wasiwe ni watazamaji wa mafumbo ya Kanisa! Lengo ni waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa kile wanacho amini na kuadhimisha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, baada ya kupita miaka 110 tangu waamini wa Kanisa Katoliki walipofanya maandamano ya Ekaristi, kuanzia tarehe 7-9 Septemba, 2018, Kanisa Katoliki nchini Uingereza linaadhimisha Kongamano na Hija ya Ekaristi Takatifu, inayoongozwa na kauli mbiu “ Adoremus – Liverpool 2018” yaani “Tunakuabudu”. Historia inaonesha kwamba, kwa mara ya mwisho Kongamano la Ekaristi Takatifu liliadhimisha nchini Uingereza kunako mwaka 1908 na tangu wakati huo, maandamano ya Ekaristi Takatifu yakapigwa marufuku nchini Uingereza na Waziri mkuu wa wakati huo Bwana Herbart Asquith. Kukatokea machafuko ya kidini kiasi kwamba, baadhi ya viongozi wa Serikali wakalazimika kubwaga manyanga.

Leo hii, waamini wa Kanisa Katoliki ni sehemu ya jumuiya ya wananchi wa Uingereza na wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Uingereza na Walles. Kumbe, hii ni nafasi nyingine tena kwa waamini kuonesha ushuhuda wa imani na matumaini yao kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo. Kongamano hili litapembua kwa kina na mapana: Maandiko Matakatifu kuhusu Ekaristi Takatifu, Taalimungu Kanisa, Ekaristi Takatifu: Lugha na Katekesi; Ibada na Nyimbo za Kuabudu Ekaristi Takatifu. Kutakuwa na Ibada ya Misa Takatifu na siku ya mwisho, waamini watafanya maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu.

Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles katika barua yake ya kichungaji anawakumbusha waamini umuhimu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kama chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni shule inayoonesha: huruma, ukarimu na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye ameamua kukaa pamoja na waja wake katika maumbo ya Mkate na Divai, kilelelezo cha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Waamini wanahimizwa kujenga utamaduni na mazoea ya kutembelea Ekaristi Takatifu kwa ajili aya kuabudu. Waamini wajenge mazoea ya kuzungumza na Kristo Yesu katika ukimya na hivyo kutoa nafasi ya kumsikiliza kutoka katika undani wa maisha, ili hatimaye, kujiaminisha kwake.

Kongamano hili anasema, Kardinali Vincent Nichols, ni mwaliko wa kumwabudu Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi, ili kujiandaa kumwilisha huruma, ukarimu, umoja na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali zao za maisha. Kanisa Katoliki nchini Uingereza linataka kuendelea kujikita zaidi katika mchakato wa kudumisha maisha na utume wa Kanisa kwa kukazia: maisha ya sala, tafakari pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Hii ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

07 August 2018, 14:20