Baba Mtakatifu akisalimiana na wachumba na familia vijana katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria mjini  Dublin, Ireland Baba Mtakatifu akisalimiana na wachumba na familia vijana katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria mjini Dublin, Ireland 

Papa: Inafurahisha kuona vijana wanachagua kufunga ndoa !

Katika Kanisa kuu ya Mtakatifu Maria mjini Dublin, Baba Mtakatifu Francisko amewasha mshumaa kwa ajili ya waathirika wa manyanyaso ya kingono na kujibu maswali juu ya upendo na imani, kwa baadhi ya wanandoa wapya na wachumba.

Sr. Angela Rwezaula - Vatican.

Baba Mtakatifu amepiga magoti na kusali mbele ya Ekaristi Takatifu na mshumaa ukiwa umewaka kukumbuka waathirika wa manyanyaso, katika moja ya Kikanisa kidogo cha Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Dublin, mahali ambapo amekwenda huko kukutana na vijana wachumba na familia mpya za vijana. Aliye mpokea katika Kanisa muhimu la Mji Mkuu wa Ireland ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Dublin Diarmuid Martin na familia moja ya vijana, mara baada ya Baba Mtakatifu kusimama kidogo kusali mbele ya masalio la mtumishi wa Mungu Matt Talbot, anayejulikana kwa watu wa Ireland kama “Mtakatifu wa walevi” kutokana na maisha yake kwani kabla ya uongofu wake yeye alikuwa mlevi.

Umuhimu wa kusikiliza wazee

Wakati wa kukutana na familia mpya za vijana na wachumba vijana ulitolewa utangulizi na mmoja wa familia ambayo imeishi ndoa kwa muda wa miaka 50, Vincent na Theresa, ambao wanatoka katika moja ya parokia za Dublin. Ni wanandoa, wazazi, babu na bibi. Katika utangulizi wanasema ushuhuda wao ni kiongozi kwa ajili ya wakati ujao na maisha ya familia ni kazi, lakini ni muhimu wamemwambia Baba Mtakatifu. Hata hivyo Baba Mtakatifu akiwajibu amesema, “Tunayo mengi ya kujifunza kutoka katika uzoefu wa maisha ya ndoa ambayo inapaswa isindikizwe kila siku na neema ya sakaramenti na kwamba: inafurahisha kuona vijana wangapi wamechagua kufunga ndoa.

Kuoa na kuolewa na kushirikishana maisha ni jambo zuri: Kuna msemo wa lugha ya kihispania usemao: uchungu wa kushirikishana wawili ni nusu ya uchungu. Furaha ya wawili pia ni furaha na nusu. Na hiyo ndiyo njia ya ndoa! Ni katika hali ya faragha na furaha, mahali ambapo machozi ya watoto ndiyo mziki mzuri sana, ndiyo mahubiri mazuri, na kilio cha matumaini. Kadhalika Baba Mtakatifu amesema, umuhimu wa kusikiliza wazee, ambao ni walinzi wa kumbukumbu ya pamoja, mahali ambapo ushuhuda kamili wa imani ni rasilimali kwa ajili ya familia changa.

Ndoa siyo kitu rahisi

Vijana wachumba wamwemweleza moja kwa moja Papa walivyo na wasiwasi na kuomba ushauri. Denis na Sinead watafunga ndoa tarehe 27 Septemba mwaka huu, Wanaomba waweze kufanya nini katika shughuli ya kudumu ya ndoa na marafiki zao ambao wanaishi suala la ndoa kibinafsi na hawana haja ya kujikita katika taasisi husika.

Baba Mtakatifu amejibu kuwa: Ndoa siyo kitu rahisi, bali ndoa ni wito, ni maisha ambayo yanakwenda mbele, maamuzi ya utambuzi na kwa ajili ya maisha yote na kuchukua wajibu wa kulea, kusali na kulinda kwa pamoja. Katika jamii ya sasa ambayo inataka utamaduni wa muda tu, mahali ambapo nikihisi nina njaa au kiu ninaweza kupata, lakini hisia hazipo za kuweza kutoshelezwa na hata kudumu kwa siku moja; ni mahali ambapo kazi, watu na ahadi huhatarisha mabadiliko, na utafikiri hakuna kilicho na thamani ambacho kinaweza kudumu hata upendo kwasababu upendo hudumu kidogo. Baba Mtakatifu amekazia kuwa Upendo unaozungumziwa hapa ni ule unaodumu maisha yote, ni shughuli ya kufanya ukue upendo kwasababu katika upendo hakuna muda mfupi, bali ni upendo unaodumu milele.

Kati ya mtindo wa kibinadamu unaozaa, ndoa ni aina ya pekee. Ni upendo ambao unatoa asili ya maisha mapya. Hiyo ni katika kujikita kwenye uwajibikaji wa kuonesha zawadi ya Mungu ya maisha ambayo inatoa mazingira ya kudumu, mahali ambapo maisha mapya yanaweza kukua na kuchanua. Ndoa katika Kanisa yaani sakramenti ya ndoa, inashiriki kwa namna ya pekee katika fumbo la upendo wa Mungu milele.

Ndoa ni ishara ya upendo kwa binadamu

Upendo wa pekee na wa kudumu ni ishara ya sakramenti ya agano kati ya Bwana na mchumba wake, na Kanisa ni mahali ambapo yupo Yesu daima na upendo wake; Kanisa ni mwamba na kimbilio katika nyakati za majaribu, lakini zaidi ya hayo ni kisima cha kukua daima na upendo msafi na daima. Inabidi kuahidi kwa nguvu maisha yenu yote anasisitiza Baba Mtakatifu na kuwaomba: “Hatarisheni. Kwasababu ndoa ni kuhatarisha”. Lakini pia ni hatari ambayo iliyo bora, yafaa kabisa kufanya hivyo. Na katika maisha yoyote kwasababu upendo ni hivyo. Upendo ni ndoto ya Mungu kwa ajili yetu na familia nzima ya binadamu. Hilo msisahau kamwe. Mungu ana ndoto kwa ajili yenu na anaomba hata sisi kufanya hivyo. Msiwe na hofu ya kuota! oteni makubwa! Amesisitiza Baba Mtakatifu.

Imani inajionesha katika nyumba

Wachumba wengine Stephen na Jordan ambao wamefunga ndoa karibu mwezi mmoja uliopita, wanajiandaa kupata mtoto ambapo wamemwomba Baba Mtakatifu, jinsi gani wanaweza kuonesha umuhimu wa imani. Papa Francisko amewasifu kwa mpango wao wa kufanya katekesi ili kuelimisha imani katika shule na katika parokia, kuandaa Kanisa la Irelanda, lakini zaidi amewausia kuanzia nyumbani, kwa utulivu wa kila siku kwa mfano wa wazazi ambao walipenda Bwana na kuamini maneno yake, nyumbani ndiyo sehemu ya kwanza ya kuonesha imani, amekazia na kuendelea: Ni katika nyumba tunamoitwa kuwa Kanisa dogo la nyumbani, watoto wanajifunza maana ya uaminifu, ukarimu na sadaka. Wanatazama namna gani mama na Baba wanachukuliana kati yao, wanavyotunza mmoja na mwingine, namna gani wanampenda Mungu na Kanisa. Kwa maana hiyo watoto wanaweza kuvuta hewa mwanana ya Injili na kujifunza kuchukuliana, kuhukumu na kutenda kwa namna ya kuwa imani ambayo wamerithi.

Kumbukumbu ya Baba Mtakatifu ambayo siyo rahisi kusahau

Imani inajionesha katika lugha ya kuzaliwa, lugha ya nyumbani ambayo ni moto wa maisha ya familia. Watoto wanajifunza kwa namna hiyo kutoka kwa wazazi jinsi gani ya kuishi ukristo anasema Baba Mtakatifu Francisko na kukumbusha uzoefu wake binafsi: “Ninakumbuka ilikuwa labda ni miaka mitano, siku moja niliingia nyumbani, katika chumba cha chakula, baba alikuwa kitoka kazini, lakini siku ile nilimwona akimpa busu mama. Hilo ni jambo ambalo sitalisahau kamwe, kwa maana lilikuwa ni jambo jema: alikuwa amechoka na kazi lakini alikuwa bado ana nguvu ya kuonesha upendo kwa mke wake! Kwa maana hiyo watoto wenu waweze kuona hali hiyo ya kukumbatiana na kupeana busu, ni jambo jema, kujifunza lugha ya upendo.

Mapinduzi ya ukarimu

Kwa njia ya sala pamoja, pia kutoa nafasi uli Mama Maria apate kuingia katika Maisha ya familia, kuadhimisha sikukuu ya kikristo na kuishi kwa kina mshikamano na wale ambao wanateseka, waliobaguliwa na kuachwa pembezoni mwa jamii. Dunia leo hii ina ukosefu wa kuwafikiria wadhaifu, waathirika na wote ambao wanadhaniwa hawazalishi. Baba Mtakatifu anaongeza kusema, dunia ya leo inatafuta wale wenye nguvu na kujitegemea lakini haina muda wa kutunza na hata nafasi kwa wale ambao hawajazaliwa, wazee, wagonjwa au ambao wanakaribia kifo.

Katika hitimisho anasema kinachohitajika sasa ni mapinduzi ya upendo ambayo lazima yaanzie kwao na katika familia zote: Taratibu taratibu tumeanza kusahau ile lugha ya moja kwa moja ya ukarimu, nguvu ya ukarimu. Utafikiri neno la ukarinu limeondolewa katika kamusi. Kwa mfano wa maisha yenu amebainisha: watoto wenu wanaweza kuongozwa na kugeuza kizazi cha upendo, utajiri na imani, kwa ajili ya kupyaisha Kanisa na jamii nzima ya Ireland!

26 August 2018, 15:01