Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana 22 Julai 2018 Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana 22 Julai 2018  (AFP or licensors)

Papa Francisko asema: Yesu alikuwa na jicho la moyo, huruma na bidii ya kufundisha

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa na jicho la moyo lililopenyeza katika undani wa mtu kiasi cha kung'amua mahitaji msingi: kiroho na kimwili; alikuwa ni kiongozi mwenye huruma kwa watu wake na daima alipenda kuwalisha watu wa Mungu mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni, yaani Neno la Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Kristo Yesu kama Bwana, Mwalimu na Mchungaji mwema, alikita maisha na utume wake katika kuangalia kwa jicho la moyo linalopenya na kugusa undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili; alikuwa na huruma kiasi cha kuamua kutenda kwa haraka ili kukidhi mahitaji ya watu wake: kwa kuwalisha, kuwaponya na kuwaondolea dhambi zao. Yesu alikuwa ni Mwalimu aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 22 Julai 2018 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Injili ya Jumapili ya XXVI ya Mwaka B wa Kanisa inaonesha Mitume wa Yesu wakirejea kwa kishindo na kuanza kumjuza habari za mambo yote waliyofanya na kufundisha. Haya ni mang’amuzi ya utume wa kwanza, yaliyoambatana na uchomvu, kiasi hata cha kuhitaji muda wa kujitenga kidogo faragha, ili wapate kupumzika. Yesu aliguswa na mahitaji msingi ya mitume wake, akatambua kwamba, kwa hakika walikuwa wanahitaji muda wa kujipumzisha baada ya “patashika nguo kuchanika” katika kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu.

Lakini kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu Francisko, ndoto ya Kristo Yesu kutaka kuwapumzisha Mitume wake, ikayeyuka na kupotea, baada ya kukutana na umati mkubwa wa watu, akawahurumia kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. Mwinjili Marko katika sehemu hii anakazia mambo msingi katika maisha na utume wa Kristo Yesu yaani: Kuona, huruma na kufundisha, kama sehemu ya mbinu mkakati wake wa shughuli za kichungaji. Jicho la Yesu lilipenyeza katika undani wa mtu na kugusa mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.

Hiki ni kielelezo cha mtazamo na mwelekeo wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu anayemwangalia mtu mzima na historia inayomzunguka. Kwa njia hii, Yesu anataka kujenga na kuimarisha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Yesu aliguswa na mahitaji ya umati huu mkubwa uliokuwa unatafuta kiongozi na msaada muhimu katika maisha yake: kiroho na kimwili. Umati huu, ulitegemea kwamba, Yesu angeweza kufanya miujiza, lakini kwa mshangao mkubwa, akaanza kuwafundisha mambo mengi. Yesu anawapatia waja wake “Mkate wa Neno la Mungu unaoshibisha kiu ya maisha ya kiroho” katika ukweli na haki na hivyo kuwa ni dira na mwongozo wa maisha. Kristo Yesu ni ukweli na uzima anayewakirimia waja wake mwongozo wa kufuata katika safari ya maisha ya hapa duniani.

Baba Mtakatifu anasema, pale waamini wanapotoweka na kusambaratika kutoka katika uso na uwepo wake Kristo Yesu; kwa kukosa upendo na huruma yake, hapo ndipo watu wanapokata tamaa na kutoridhika katika maisha. Waamini wakiambatana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, wawe na uhakika wa usalama; na kwamba, wanaweza kuvuka kinzani, migogoro na majaribu katika maisha na hivyo kuanza kujielekeza katika upendo kwa Mungu na jirani. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu amejifanya sadaka na zawadi kwa ajili ya wengine na hivyo kuwa ni kielelezo na ushuhuda makini wa upendo na huduma kwa watu wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao, kwa kushirikiana nao na kuwapatia huduma makini wanayohitaji kwa wakati huo!

Yesu mchungaji mwema

 

22 July 2018, 07:34