Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana 22 Julai 2018. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana 22 Julai 2018.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Jumuiya ya Kimataifa itende kwa nguvu na ushupavu kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha masikitiko na majonzi makubwa kutokana na wakimbizi na wahamiaji kuendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutenda kwa nguvu na ushupavu ili kuokoa maisha ya watu! Usalama, utu, heshima na haki zao msingi zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko mengine yote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 22 Julai 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameyaelekeza mawazo na sala yake kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kufariki dunia kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania. Baba Mtakatifu anasema, katika taarifa za maafa kama haya, anapenda kuwahakikishia ndugu na jamaa wa wale waliofariki dunia, uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kuialika Jumuiya ya Kimataifa kutenda kwa nguvu na ushupavu, ili kuokoa maisha ya watu wanaofariki maji kwenye Bahari ya Mediterrania ili kwamba, matukio haya yasijirudiea na kuwa kama sehemu ya habari za kawaida zisizokuwa na mguso wala mashiko! Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuhakikishiwa usalama, haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku ya wakimbizi na wahamiaji duniani kwa mwaka 2018 anafanua kwamba, Kuwaendeleza wakimbizi na wahamiaji maana yake ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya inayowapokea na kuwakirimia inawapatia fursa ya kujiendeleza katika utimilifu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wapewe uhuru wa kuabudu na kuungama imani yao; fursa za kazi na ajira; nafasi ya kujifunza lugha na tamaduni za watu mahalia, ili kweli waweze kushiriki kikamilifu katika maisha ya Jamii inayowahifadhi.

Watoto wadogo walindwe dhidi ya kazi za suluba zinazoweza kuwapoka utu na heshima yao kwa kuwadumaza! Wakimbizi na wahamiaji wapewe fursa ya kuungana tena na wanafamilia wao bila ya kuweka uchumi kuwa kikwazo kikuu kinachowatenganisha. Jumuiya ya KImataifa ishirikiane katika kuwahudumia na kuwatunza wakimbizi na wahamiaji.

Usalama wa wahamiaji
22 July 2018, 07:43