Cerca

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko akiwa na familia za wana ukatekumeni mpya. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na familia za wana ukatekumeni mpya. 

Tangazeni na kushuhudia Injili ya familia duniani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema familia ni hospitali iliyoko karibu nawe na ni huduma ya kwanza yenye mvuto na mashiko. Familia ni kiini cha upendo, umoja na ukarimu. Familia ni shule ya kwanza ya imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, familia ni makazi maalum ya wazee na wagonjwa. Familia ina tunu na changamoto zake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, familia bado inaendelea kuwa ni kitovu na chemchemi ya Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni wajibu wanafamilia kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu! Familia kadiri ya mpango wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu, Mafundisho tanzu ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema na familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia!

Siku ya IX ya Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 21- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Maandalizi haya yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi, hata kama wataziba masikio yao, lakini watambue kwamba, kwa hakika wamehubiriwa Injili ya familia.

Bi Brenda Drumm, Mkurugenzi wa mawasiliano katika maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani kwa mwaka 2018 anasema, sehemu kubwa ya maandalizi ya maadhimisho haya tayari imekamilika na kwamba, familia ya Mungu nchini Ireland iko tayari kuwapokea na kuwakirimia wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaoshiriki katika maadhimisho haya na kwamba, kilele cha maandalizi haya ni pale, watakapompokea Baba Mtakatifu Francisko nchini humo, kuanzia tarehe 25-26 Agosti, 2018. Anasema, Baba Mtakatifu anaendelea kufuatilia kwa karibu sana maadhimisho haya kwani kwake, Injili ya familia inapewa kipaumbele cha pekee sana katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Kumbe, uwepo wake katika maadhimisho haya ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Akiwa nchini Ireland, sehemu kubwa ya muda wake, itakuwa ni kukaa na kuzungumza na familia pamoja na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili nao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Injili ya familia.

Baba Mtakatifu atapata muda wa faragha kusali na kutafakari kidogo kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Knock nchini Ireland. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tayari wamekwishajipatia tiketi za kuhudhuria katika matukio mbali mbali. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi wakati huu familia na mahujaji 15, 000 kutoka katika nchi 116 wanatarajiwa kushiriki kwa ukamilifu na uchangamfu mkuu. Kanisa linataka kuwekeza zaidi katika utume na Injili ya familia, kwani maisha ya binadamu yanarithishwa kwa njia ya familia kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. Kwa kuzitegemeza na kuziwezesha familia, jamii inaweza kuboreka zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, familia ni hospitali iliyoko karibu nawe na ni huduma ya kwanza yenye mvuto na mashiko. Familia ni kiini cha upendo, umoja na ukarimu. Familia ni shule ya kwanza ya imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, familia ni makazi maalum ya wazee na wagonjwa. Familia ina tunu na changamoto zake, kwani kuna wakati wanandoa wanarushiana sahani utadhani kana kwamba, ni mbayuwayu wanaruka kutafuta chakula, lakini pia ni shule ya msamaha, upendo, haki na amani!

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani, ametoa rehema kamili kwa waamini watakaoshiriki kikamilifu katika maandalizi na maadhimisho hayo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika upendo, daima wakijitahidi kuzitakatifuza familia zao, kwa kufuata mfano bora wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Haya ni maadhimisho yanayopambwa kwa matukio mbali mbali kuzunguka Jimbo kuu la Dublin kama kielelezo cha mshikamano wa upendo. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, tarehe 21 Agosti 2018 kutakuwa na ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani katika ngazi ya kitaifa, na kwamba, wahusika wakuu ni waamini wote kutoka katika majimbo 26 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Ireland. Tukio la pili ni kuanzia tarehe 22-24 Agosti, 2018, siku tatu za Kongamano la Kichungaji kuhusu Familia. Wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watapata nafasi ya kusali, kutafakari na kujadiliana kuhusu kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu”. Vijana wa kizazi kipya watapata nafasi ya kushirikisha mawazo, mang’amuzi, vipaumbele na changamoto wanazokabiliana nazo katika mchakato wa maandalizi ya kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kama furaha ya ulimwengu! Hata watoto ambao ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, watahusishwa nao!

Tukio la tatu litakuwa ni tarehe 25 Agosti 2018, Siku ya Kuadhimisha Injili ya Familia. Utakuwa ni muda wa sala, tafakari; shuhuda za imani kutoka kwa wawakilishi wa familia mbali mbali duniani. Tukio hili litapambwa kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Kilele cha maadhimisho ya Siku ya IV ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 ni Jumapili tarehe 26 Agosti 2018. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu. Padre Tim Barlett, Katibu mkuu wa Maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 anasema, Injili ya Familia ni moto wa kuotea mbali na kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kushiriki kikamilifu kadiri ya uwezo na nafasi zao.

Furaha ya Upendo ndani ya familia Katika Mwanga wa Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, Neno la Mungu ni “mwandani” wa familia hata kwa familia ambazo zinakabiliwa na “migogoro” kwa sababu linawaonesha dira na njia ya kufuata. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanaume na mwanamke wanapoungana pamoja katika kifungo chau pendo wanapendana na kuwa ni chemchemi ya uhai, mfano hai wa Mungu Mwenyezi ambaye ni Muumbaji na Mkombozi. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja katika upendo, tunu zinazopaswa kushuhudiwa ndani ya familia. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majadiliano unanopaswa kufahamika kuwa ni mwambatano wa kimwili na maisha ya ndani, unaowawezesha wanandoa kuwa kitu kimoja sanjari na kujisadaka katika upendo. Utu wema ni tunu muhimu sana katika mang’amuzi ya maisha ya ndoa na familia ya Kikristo, ingawa tunu hii mara nyingi inasahaulika na wengi nyakati hizi za mahusiano ya haraka haraka na yasiokuwa na mizizi.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa malezi na majiundo makini ya watoto, mawe hai ndani ya familia, zawadi ya Mungu na wala si mali ya mtu binafsi. Anagusia tatizo la ukosefu wa fursa za ajira ndani ya familia; mateso na mahangaiko ya familia za wakimbizi na wahamiaji wanaokataliwa na kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, wanaishi katika mazingira magumu na wasi wasi mkubwa!

Furaha ya Upendo ndani ya familia: Ukweli na changamoto za familia katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mafao ya familia ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ulimwengu na Kanisa kwa siku za usoni, kumbe, unapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Hapa Baba Mtakatifu anaorodhesha litania ya matatizo yaliyobainishwa na Mababa wa Sinodi mintarafu familia katika ulimwengu mamboleo: Ubinafsi unaotishia dhana ya uhuru na haki kwa kuzing’oa kutoka katika ukweli, tunu msingi na kanuni za maisha kiasi cha kutoa mwelekeo kwamba, kila jambo linaruhusiwa. Ubinafsi, utamaduni usiojali kwa kudhalilisha upendo ambao unageuzwa na kuonekana kuwa ni jambo la mitandao ya kijami; upendo unaoweza kuunganishwa, kutatizwa au kusubilishwa kadiri ya matakwa ya mlaji! Kwa njia hii Baba Mtakatifu anasikitika kusema, watu wanageuza familia kuwa ni jambo la mpito; mahali pa kukutana pale mtu anapojisikia.

Hapa ndipo mahali muafaka ambapo mchango wa Wakristo unapaswa kujionesha kwa kuambata ndoa na kwenda kinyume cha mtazamo na mawazo ya watu wa nyakati hizi kwamba, ndoa ni kama ”mtindo” au kwa kujisikia wanyonge katika ngazi ya ubinadamu na maadili. Mwelekeo huu wa Kikristo haupaswi kuwa tu kama kigezo cha kupambana na mwelekeo potofu wa dhana ya ndoa na familia kwa kujilinda; kwa kwenda kinyume cha ari na ugunduzi wa kimissionari au kwa kujikita katika sheria.

Baba Mtakatifu anasema, mwelekeo wa Kikristo unapaswa kuwa ni kielelezo cha uwajibikaji unaojikita katika ukarimu; kwa kushuhudia sababu msingi na malengo ya maisha ya ndoa na familia. Hapa kuna haja ya kuonesha ukomavu unaojikita katika ukweli na uhalisia wa maisha na kwamba, Wakristo wengi wamejikuta wakishuhudia maisha ya ndoa inayojikita kimsingi katika kazi ya uumbaji au katika masuala ”mafundisho tanzu ya Kanisa” maadili na kanuni maadili viumbe; mambo ambayo yamewafanya wanandoa wengi kuishi katika ombwe bila kugusa uhalisia wa mambo! Wengi wameona ndoa kuwa ni mzigo ambao wanapaswa kuubeba katika maisha yao, badala ya kuwa ni safari katika ukuaji na utimilifu wa mtu.

Baba Mtakatifu anaitaka mihimili ya Uinjilishaji kujikita kwa namna ya pekee katika majiundo makini ya dhamiri nyofu bila kujidai kwamba inataka kubadili mwelekeo. Hapa kuna haja ya kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zenye mwelekeo chanya na ukarimu; zinazoweza kutoa dira na mwelekeo barabara na sahihi wa kupata furaha ya kweli; kwa kuonesha ukaribu wa upendo kwa wanyonge. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua changamoto ambazo wanafamilia wanapaswa kukabiliana nazo katika ulimwengu mamboleo mintarafu mchango wa Mababa wa Sinodi za Maaskofu zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na mwaka 2015.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapinga kwa nguvu zote sera na mikakati inayofumbata utamaduni wa kifo kwa kuruhusu: vizuia mimba; kuwafanya watu kuwa tasa au utoaji wa mimba. Baba Mtakatifu anawaambia wanandoa kwamba, kwa kuwa na dhamiri nyofu na wanapoona kuwa kweli katika safari ya maisha yao wamekuwa wakarimu katika kuendeleza zawadi ya maisha, wanaweza kuamua kuwa na mwelekeo wa kuratibu idadi ya watoto wanaotaka kupata kutokana na sababu msingi!

Baba Mtakatifu anasema, kati ya umaskini mkubwa ambao jamii nyingi zinakabiliana nao kwa nyakati hizi ni kupungua kwa imani na matendo ya ibada, hali inayowatumbukiza watu wengi katika upweke, dalili za kutokuwepo kwa Mungu katika maisha ya watu. Familia na nyumba ni chanda na pete na kwamba, haki ya familia si haki ya mtu binafsi kwani familia ni kito cha thamani ambacho kinapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa na jamii kwa kuwa na sera makini ya familia. Baba Mtakatifu anagusia pia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinazofanywa kwenye familia, shule, jumuiya na taasisi ambazo zimepewa dhamana ya kuwalinda! Hii kashfa isiyovumilika kabisa!

Baba Mtakatifu anasema kuna familia za Kikristo zinazoteseka kwa kudhulumiwa na kunyanyaswa; kuna familia zenye walemavu, wazee na mbaya zaidi ni umaskini wa hali na kipato. Kwa familia zinaosambaratika umaskini unakuwa ni mzigo mkubwa kwani hapa wanawake ndio wanaobeba dhamana kubwa ya malezi na matunzo ya watoto wao. Watu wa jinsia moja wanaoishi pamoja, si ndoa kwani haya ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa na mpango wa Mungu kwa binadamu mintarafu kazi ya uumbaji.

Ndoa za namna hii zinahatarisha na kudhoofisha tunu msingi za Injili ya familia. Utu wema na kanuni maadili ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na wote. Dhuluma na nyanyaso kwa wanawake ni kudhalilisha utu na heshima yao! Hakuna sababu msingi za kuwabagua wanawake, bali haki na wajibu wao vinapaswa kulindwa na kudumishwa! Lakini Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kuna misimamo mikali ya kutetea wanawake ambayo haiwezi kukubalika hata kidogo.

Suala la usawa wa kijinsia ni jambo ambalo ni hatari kwa malezi na makuzi ya watoto; tofauti za kijinsia zinaweza kubainishwa lakini haziwezi kutenganishwa; changamoto ni kuheshimu kazi ya Uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, maisha ni zawadi inayopaswa kupokelewa kwa heshima na taadhima; kwa kulindwa na kudumishwa kadiri ya mpango wa Mungu.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

28 July 2018, 09:07