Kumbu kumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, 26 Julai 2018 Kumbu kumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, 26 Julai 2018 

Papa Francis: Dhamana na wajibu wa jamii kuwalinda na kuwaenzi wazee!

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, anasifu heshima inayotolewa na familia ya Mungu Barani Afrika kwa wazee wao, kwani wao ni utajiri, hawatengwi wala kudharauliwa bali wanabaki kama miamba na walezi wakuu wa mila, desturi na tamaduni njema katika jamii. Huu ni mfano bora unaopaswa kuigwa na walimwengu badala ya kuwatelekeza wazee kama "magari mabovu"!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Siku kuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai, katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwathamini wazee, kwani wao ni amana na utajiri wa familia. Wahudumiwe kikamilifu, wapendwe na kupatiwa nafasi ya kuzungumza na kucheza na wajukuu wao.

Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, Vatican News inapenda kurejea tena katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuhusu nafasi ya wazee katika jamii pamoja na kurejea tena kwenye Waraka wa Kitume wa Papa Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” Sura ya tatu: Mwelekeo kwa Yesu: Wito wa familia. Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee, wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na utume wao ndani ya Familia. Watambue kwamba, wao ni wadau wa kwanza wanaoshirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji, malezi na makuzi ya watoto wao kwa sasa na kwa siku za usoni.

Wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani, wazazi wawasaidie watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” anaanza kwa kubainisha ukweli kwamba, wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbali mbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku za usoni.

 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, anasifu heshima inayotolewa na familia ya Mungu Barani Afrika kwa wazee wao, kwani wao ni utajiri, hawatengwi wala kudharauliwa bali wanabaki kama miamba na walezi wakuu wa mila, desturi na tamaduni njema katika jamii. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunza namna ya kuheshimu na kuwathamini wazee kutoka Afrika. Umaskini na magonjwa visiwe ni sababu ya kuwatenga na kuwakosea heshima wazee katika jamii. Ameichangamotisha jamii kwa ujumla kutambua kuwa wazee ni msingi wa uhai na maendeleo endelevu na fungamani.

Kanisa Barani Afrika linatakiwa kuwapa nafasi wazee katika kutatua migogoro ya kijamii, ili kuharakisha msamaha, haki na amani. Hii inatokana na ukweli kwamba, amani na utulivu Barani Afrika kwa mda mrefu imejengwa katika Mabaraza ya usuluhishi ambamo wazee ndio waamuzi. Amethibitisha kuwa Kanisa linawaheshimu, linawasikiliza na kuwatumia wazee. Amewataka Wazee kuupokea wajibu huo na kamwe wasijisikie kama ni watu wasiokuwa na nafasi na wala kwamba, wamepitwa na wakati. Wazee wametakiwa kutumia uzoefu na karama zao katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili

Akizingatia wajibu na nafasi muhimu waliyo nayo wanaume katika familia na jamii, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amewataka Wanaume Wakatoliki katika familia zao kuleta mchango mkubwa katika malezi ya Kikristo na kiutu kwa watoto wao. Wawe mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wawajibike kisawa sawa katika malezi na makuzi ya watoto wao sanjari na kuwathamini wenzi wao wa ndoa.  Hata hivyo, analitaka Kanisa Barani Afrika kuweka bayana na kupigania haki za wanawake na kuwahusisha moja kwa moja katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina. Amezitaka taasisi za Kanisa na wakatoliki kwa ujumla, kuwa mfano wa kumthamini na kumwendeleza mwanamke kwa kumpa fursa sawa na hadhi anayostahili katika jamii.

Wanawake wajiheshimu na kutambua nafasi waliyo nayo katika kuleta maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kama ishara ya upendo na mshikamano miongoni mwa wanafamilia. Anawachangamotisha kuendeleza utamaduni uliowekwa na wanawake katika Injili ambao daima waliandamana na Yesu na Mitume. Wanawake wajikite katika kulilea Kanisa na jamii kwa nguvu na upendo wao wote bila kujibakiza. Wanawake wajione kuwa kama uti wa mgongo wa familia ya Mungu Barani Afrika. Idadi yao na karama zao ni chachu tosha katika mchakato wa kuleta masamaha, haki na amani Barani Afrika.

Waraka wa Kitume: Furaha ya Injili katika Familia Sura ya III: Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anatoa muhtasari wa mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia. Hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na ina mwelekeo wa kudumu ambayo ni zawadi. Ndoa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya upendo wa kweli wa wanandoa na wito mahususi wa kuishi kama bwana na bibi. Ndoa ni Sakramenti na zawadi inayowawezesha wanandoa kujikita katika mchakato wa utakatifu na wokovu wa wanandoa wenyewe. Kwa mwelekeo huu tendo la ndoa ndani ya familia, lililotakatifuzwa kwa Sakramenti ni njia ya kukua na kukomaa katika neema na Fumbo la maisha ya ndoa, mwaliko kwa wanandoa kumwomba Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuibariki Ndoa yao.

Kanisa halina budi kuwasaidia wanandoa wanaoishi “uchumba sugu” wale waliofunga ndoa ya Serikali; wanandoa wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha ya ndoa kwa baada ya kuoa au kuolewa na kuachika na baadaye kuamua kuoa au kuolewa tena. Viongozi wanapaswa kuwashughulikia watu hawa kwa kuongozwa na ukweli wa upendo; wawafafanulie kwa kina na mapana mafundisho ya Kanisa na kwamba, hakuna majibu ya mkato, bali kila kesi inapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Viongozi wawe na hekima ya kutambua unyeti wa masuala wanayoshughulikia. Kwa wanandoa ambao hawakubahatika kupata watoto kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanahamasishwa kuridhika kwa kujikita katika utu wema na Ukristo, kwani watoto kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa mara nyingine tena tunu msingi ya maisha ya binadamu na haki ya mtu kuishi tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo cha kawaida kinapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu!

Wafanyakazi katika sekta ya afya wanayo dhamana ya kimaadili kwa kukuza dhamiri nyofu ili kuendeleza zawadi ya uhai kwa kutojiingiza kwenye vitendo vya kifo laini au tiba za ghali sana. Kanisa linapinga adhabu ya kifo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, kuna mahusiano muhimu sana kati ya Familia na Kanisa, kwani ikiwa kama Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, Kanisa ni familia ya familia na kwamba, upendo unaomwilishwa kwenye familia ni nguvu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Siku kuu ya watakatifu
26 July 2018, 14:54