Papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana 29 Julai 2018 Papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana 29 Julai 2018 

Papa Francisko: Waamini jibuni kashfa ya baa la njaa kwa vitendo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wakristo, wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, mwaliko wa kujibu kwa umakini mkubwa kila aina ya kilio cha baa la njaa, kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kamwe waamini wasiwageuzie watu hao kisogo. Wajifunze: kuthamini, kuhifadhi na kugawana chakula na wahitaji zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Yesu pamoja na mitume wake, walikuwa na fedha kidogo kiasi kwamba, wasingeweza kutosheleza mahitaji ya chakula kwa umati mkubwa uliojitokeza kumsikiliza Kristo Yesu akiwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Lakini, wakagundua kwamba, kulikuwa na kijana aliyekuwa na mikate mitano na samaki mawili, Yesu akaamuru wakatishwe, akaichukua ile mikate, akashukuru, akaimega na kuwapatia mitume, ili waweze kuwaandalia watu, wote wakala, wakashiba na kusaza mabaki ya chakula yaliyokusanywa katika vikapu kumi na viwili.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 29 Julai 2018, amewataka waamini kuendelea kumpatia Kristo Yesu kipaumbele cha kwanza, kwani anataka kuwaonesha huruma na mapendo; anaguswa na mahitaji msingi ya waja wake. Kimsingi, watu wana njaa na Yesu kwa kushirikiana na mitume wake, anataka kuwashibisha watu hawa. Katika maisha na utume wake, Kristo Yesu amewalisha watu chakula cha Neno la Mungu, akawafariji na kuwapatia wokovu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Yesu aliwaonea huruma waja wake, akawalisha pia kwa chakula cha kimwili na kuwaponya magonjwa yao. Kumbe, wafuasi wa Kristo, kamwe hawawezi kujidai kwamba, hawaoni mahitaji msingi ya jirani zao, kiasi hata cha kujibidisha ili kuweza kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio hiki. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa kijana yule aliyekuwa na mikate mitano na samaki wawili, lakini hakusita kugawana na umati ule! Vijana wajengewe uwezo wa kujisadaka kwa ajili ya mahitaji msingi ya jirani zao. Waamini kwa kuwapatia jirani zao mambo msingi katika maisha, wanaweza kuwa tayari kusikiliza na kufahamu mambo makubwa zaidi, yatakapokuwa yanatangazwa na kushuhudiwa mbele yao.

Yesu anapenda kuwafunulia watu wenye njaa, uhuru, haki na amani, upendo na neema ya Mungu katika maisha yao. Kristo Yesu anaendelea hata leo hii kuonesha uwepo wake endelevu kati pamoja na watu kwa njia ya Wakristo, wanaopaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kujibu kwa umakini mkubwa kila aina ya kilio cha njaa, kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kamwe waamini wasiwageuzie watu hao kisogo.

Kristo Yesu ni mkate wa uzima wa milele ulioshuka kutoka mbinguni, changamoto na mwaliko kwa Wakristo ni kuonesha mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha. Huduma ya upendo kwa maskini ni kielelezo makini cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu katika ngazi ya mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu katika tafakari yake, amekazia pia umuhimu wa kuhakikisha kwamba, chakula kinatumiwa vyema, mwaliko kwa familia ya binadamu kuhakikisha kwamba, inatumia vyema rasilimali za dunia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rasilimali hizi anakaza kusema Baba Mtakatifu si kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya jamii; wala kwa ajili ya mahangamizi ya binadamu mwenyewe, bali ni kwa ajili ya kuendeleza huduma fungamani inayojikita katika ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Watu wajifunze kuheshimu, kutunza na kugawana chakula na jirani zao kama kielelezo cha Injili ya ukarimu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria, awasaidie walimwengu kuibua mbinu mkakati utakaojikita zaidi katika maendeleo fungamani ya binadamu, uhakika wa usalama wa chakula na mshikamano kwa kuondokana na chuki, matumizi ya silaha na hatimaye, vita.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

29 July 2018, 10:14