Tafuta

Papa Francisko tarehe 31 Julai 2018 amekutana na kuzungumza na mahujaji wa Chama cha Watumishi wa Altareni Kimataifa. Papa Francisko tarehe 31 Julai 2018 amekutana na kuzungumza na mahujaji wa Chama cha Watumishi wa Altareni Kimataifa. 

Papa Francisko: Utakatifu ni wito wa wote kila mtu kadiri ya hali na maisha yake!

Baba Mtakatifu Francisko, jioni tarehe 31 Julai 2018 amekutana na mahujaji wa Chama cha Kimataifa cha Watumishi Altareni na kujibu maswali yao matano, akiwakumbusha kwamba, hata yeye ni hujaji katika imani na kwa kuungana na Kristo Yesu, chimbuko la amani, anapenda kuwatia shime katika mchakato wa kutafuta, kuambata na kushuhudia amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika malezi, makuzi na majiundo ya watoto na vijana, ambao kimsingi ni matumaini ya Kanisa na Jamii ya leo na kesho iliyo bora zaidi akiwataka wawe ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na mshikamano duniani. Kuanzia tarehe 30 Julai 2018 hadi tarehe 3 Agosti 2018, Mji wa Roma umefunikwa na watumishi wa Altareni zaidi ya sabini elfu, kutoka katika nchi 19 duniani walioitikia mwaliko wa “Associazione Internationalis Ministrantium, CIM, yaani “Chama cha Kimataifa cha Watumishi Altareni, kinachoongozwa na Askofu Ladislav Nemet.

Hija ya Watumishi wa Altareni kwa mwaka 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Utafute amani ukaifuatie. Hiki ni kilio, furaha na shukrani ya maskini mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa huruma, wema na upendo mkuu aliomtendea na kwamba, anaona wajibu wa kushirikishana furaha na jirani zake. Baba Mtakatifu Francisko, jioni tarehe 31 Julai 2018 amekutana na mahujaji hawa na kujibu maswali yao matano, akiwakumbusha kwamba, hata yeye ni hujaji katika imani na kwa kuungana na Kristo Yesu, chimbuko la amani, anapenda kuwatia shime katika mchakato wa kutafuta, kuambata na kushuhudia amani duniani.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali kuhusu tendo la amani ambalo waamini wanashirikishana kwenye Ibada ya Misa Takatifu, anasema ni mwaliko na changamoto ya waamini kwenda kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani na umoja unaoleta mabadiliko katika Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa, ili kupenda kama anavyopenda mwenyewe. Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu yanakamilika kwa waamini kupewa amani, ambayo wanapaswa kuipeleka kwa wengine kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo kwamba, kwa hakika, wao ni wafuasi wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwilisha amani hata katika matendo ya kawaida kabisa!

Watumishi wa Altareni wamemwambia Baba Mtakatifu kwamba, wanapokuwa wanatumikia Altareni wanapata pia nafasi ya kulitafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia hii, wanahamasishwa baada ya kusikiliza Neno la Mungu, kulimwilisha katika matendo, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu amewakumbusha watumishi wa Altareni kwamba, wao wanatekeleza kwa vitendo: Sala na Kazi, “Ora et Labora” kama ilivyokuwa kwa Maria na Martha. Huduma ya Liturujia ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, lakini pia wanapaswa kujenga utamaduni wa kusali na kukaa kimya, ili hatimaye, kung’amua karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha, tayari kuyatumia kwa ajili ya wengine pamoja na kujiweka mbele ya Mungu jinsi walivyo! Baba Mtakatifu anawatia shime vijana hawa kuwahudumia jirani zao na wawe wepesi kuomba ushauri kutoka kwa walezi na vijana wenzao jinsi ya kuweza kumtumikia Mungu na jirani kwa ufanisi zaidi.

Vijana hawa wanasikitika kuona kwamba, vijana wenye umri kama wao, wanashindwa kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu, kiasi kwamba, vijana hawana tena “mchechemko wa kwenda Kanisani” pengine kutokana na sababu mbali mbali katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka vijana hawa kuwa ni mitume na wamisionari miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwa kushuhudia kwamba, katika hija ya maisha yao, wamebahatika kukutana na Kristo Yesu na sasa wanamfahamu, changamoto inayowataka kuendelea kujipyaisha katika Neno la Mungu na Sala. Wawe washiriki wazuri wa Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wajenge ndani mwao, utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu katika hali ya ukimya unaomwilishwa katika matendo mema. Vijana wana kiu na hamu ya kuwa na marafiki wema na watakatifu, kwa njia ya ushuhuda wao wenye mvuto, wanaweza kuboresha maisha ya familia, jumuiya na Kanisa katika ujumla wake.

Watumishi wa Altareni wamemsimulia Baba Mtakatifu Francisko dalili za ukanimungu wanazokutana nazo katika hija ya maisha yao kwa baadhi ya watu kuonesha kwamba, hawana sababu ya uwepo wa Mungu katika maisha, wao wanajitosheleza au kwa maneno mengine “wako kamili gado”. Imani ya watu kama hawa imengia mchanga! Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani ni zawadi kubwa katika maisha ya mwanadamu na muhimu sana kama ilivyo hewa. Imani inawawezesha waamini kupata maana halisi ya maisha kwa kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu anayetaka kuanzisha mahusiano na mafungamano ya dhati, ili kuwa kweli ni watoto wake wapendwa. Watu wote wanahamasishwa kujenga familia ya Mungu, yaani Kanisa, Jumuiya ya waamini inayolishwa kwa Mkate wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Watumishi wa Altareni wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wanaipenda na kuithamini sana huduma yao Altareni na kwamba, wanataka kumtumikia Mungu na jirani, lakini kutenda mema, hapo panageuka kuwa ni patashika nguo kuchanika kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu kwani kwa hakika si wakamilifu wala watakatifu! Baba Mtakatifu amesema kwamba, utakatifu ni mchakato wa maisha unaojikita katika ushupavu na wala si kwa watu goigoi na kwamba, Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani ndiyo dira na mwongozo wa utakatifu wa maisha. Wajitahidi kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Hii ni dhamana inayoweza kutekelezwa na kila mwamini kadiri ya uwezo na nafasi yake. Kwa njia hii, anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa hakika watakuwa wakamilifu na watakatifu, kwani “utakatifu si lelemama wala maji kwa glasi; kweli yataka moyo”! Na kwa majibu haya, watumishi Altareni, walihitimisha hija yao ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

 

31 July 2018, 10:21