Cerca

Vatican News
Umaskini bado una nyanyasa utu na heshima ya binadamu. Umaskini bado una nyanyasa utu na heshima ya binadamu.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Madonda Matakatifu ya Yesu yanaendelea kuvuja damu duniani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema Madonda Matakatifu ya Yesu yanaendelea kujionesha kati ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, magonjwa na umaskini; wagonjwa, wazee na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau wafungwa wa kiroho na kimwili. Kumbe, bado kuna umuhimu wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu katika haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Miaka 50 ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake usiokuwa na mipaka. Ni muda wa kutafakari na kujiwekea malengo na mikakati ya kuboresha maisha na utume, daima kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa karama ya Jumuiya ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa na walimwengu katika ujumla wao. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Bwana Maurizio Lopez Oropeza, Rais wa Jumuiya ya Maisha ya Kikristo Duniani, Jumuiya hii inaposherehekea Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Mosi, Baba Mtakatifu anasema, kwa kutambua na kuthamini: zawadi, karama na neema ambazo wamekirimiwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita; wanapaswa kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mungu, ambaye amewaangalia na kuwapatia tunza yake inayovuka mipaka ya ubora na tunu zao kama binadamu. Hii ni dhamana inayowawajibisha kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, ili kukutana na jirani zao, tayari kuwalisha kwa Neno la Mungu na Mkate wa uzima, ulioshuka kutoka mbinguni, unaozima kiu ya udadisi wa kibinadamu, kwa kupambwa na huruma pamoja na upendo, unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii ni changamoto ya kujikita katika mambo msingi ya maisha ya kiroho na kiutu!

Pili, kwa kuzingatia kiini cha tasaufi ya Mtakatifu Ignasi wa Loyola, ambaye Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu yake, kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai, Baba Mtakatifu anampongeza Bwana Maurizio kwa jitihada zake za kutaka kuunganisha na kumwilisha tafakari katika matendo; sala na kazi kama mlango wa kumwendea Mwenyezi Mungu kwa njia ya Madonda Matakatifu ya Yesu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Madonda haya yanaendelea kujionesha kati ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, magonjwa na umaskini; wagonjwa, wazee na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau wafungwa wa kiroho na kimwili.

Tatu, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kwa kuongozwa na tunu msingi za maisha ya Kikristo, huku wakiendelea kujizatiti katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, wanapaswa kujisadaka mikononi mwa Kristo Yesu, ili aweze kuwafunda na kuwaunda kwa upendo wake, ili waweze kufanana yake. Waendelee kujiuliza ni mambo yepi ambayo wamemtendea na wataendelea kumtendea Kristo Yesu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anaishukuru Jumuiya ya Maisha ya Kikristo Duniani, inaposherehekea Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kama shuhuda wa huruma na upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anawatia moyo kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo kati pamoja na watu wake, kwa kushuhudia kwa vitendo maana ya utume wao. Hatimaye, anawaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

31 July 2018, 16:02