Cerca

Vatican News
Papa Francisko anawataka waamini kutubu na kumwongokea Mungu ili waweze kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Papa Francisko anawataka waamini kutubu na kumwongokea Mungu ili waweze kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. 

Papa Francisko awataka waamini kutubu na kumwongokea Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, yuko tayari kuwapokea na kuwarudia hadhi yao tena kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, ikiwa kama watakuwa tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao! Mungu atawasamehe na kuwaokoa kutoka katika utumwa wa dhambi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Mama Kanisa anafundisha kwamba, dhanbi ni kosa dhidi ya akili, ukweli na dhamiri sahihi. Ni kushindwa kuwa na mapendo kweli kwa Mungu na jirani, hivyo, uharibu mahusiano na mafungamano wa kibinadamu. Ndiyo maana Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi, ili aweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia ukweli. Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Baba Mtakatifu Franciko kwa ajili ya Chama cha Familia Kimataifa cha E’quipe Notre-Dame, (END), ambacho kimekuwa na mkutano wake wa XII wa Mwaka huko Fatima nchini Ureno, kuanzia tarehe 16-21 Julai 2018.

Hiki ni chama kilichoanzishwa na Henry Caffarel, miaka 70 iliyopita na leo hii, chama hiki kimeenea katika mabara matano, kwenye nchi 95, kikiwa na jumla ya wanachama 13, 500. Tafakari za siku zimekuwa zikitolewa na Askofu mkuu mteule Josè Tolentino Calacà de Mendonca, aliyeongoza mafungo ya Kwaresima ya mwaka 2018 kwa Sekretarieti kuu ya Vatican na sasa ameteuliwa kuwa Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki. Huu umekuwa ni muda wa sala, tafakari, maadhimisho ya Ibada mbali mbali za Kanisa pamoja na ushuhuda kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Katika maadhimisho haya, Ujumbe wa Baba Mtakatifu uliotumwa kwa Maria Berta na Josè Moura, viongozi wakuu wa Chama cha Familia Kimataifa cha E’quipe Notre Dame, (END) umesomwa kwa niaba yake na  Askofu mkuu Rino Passigato, Balozi wa Vatican nchini Ureno. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anakita mawazo yake kwa Injili ya Baba mwenye huruma, ili kufafanua kwa dhati “dhana ya kazi”. Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kujitambulisha na Mwana mpotevu, anayerejea nyumbani kwa Baba mwenye huruma na kupokelewa kwa shangwe kubwa, kiasi hata cha kumrejeshea tena utu na heshima yake, aliyoichezea kutokana na mahangaiko ya ujana.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa, kujiaminisha kwa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, kwa kujitambua kwamba, wao katika maisha yao, wamemkosea Mwenyezi Mungu na kufutika kabisa mbele ya macho yake yenye huruma na mapendo, lakini kwa ujasiri mkubwa, wako mbele yake tena ili kurejesha agano na Mwenyezi Mungu! Waamini watambue kwamba, wanahitaji uwepo wa Mungu katika maisha yao, kiasi cha kuwa na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu, huruma na upendo, ili aweze kuwapokea, kuwakaribisha na hatimaye, kuwakumbatia katika mikono yake inayookoa.

Kristo Yesu alipokuwa anaitupa mkono dunia, alinyoosha mikono yake pale juu Msabani, ili kuwapokea na kuwakumbatia wote wanaokimbilia huruma na msamaha wake, kwani hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na huruma na upendo wa Kristo katika maisha yake, kwa sababu huruma ndilo jina na haki yake. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, wote wameokolewa kwa njia ya Fumbo la Pasaka. Kristo Yesu anaendelea kulihamasisha Kanisa kutoka kifua mbele, ili kwenda kuwatafuta wale waliopotea! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kusema, kwa wale wanaomtafuta Kristo Yesu, hawana budi kufuata sheria na maagizo yake, ili kweli waweze kukutana mahali ambapo Kristo Yesu mwenyewe anataka na wala si kadiri ya mapenzi ya waamini wenyewe!

Neno la Mungu
21 July 2018, 16:44