Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ametoa ushauri kwa wakleri na majandokasisi kuhusu wito, maisha na utume wao ndani ya Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Francisko ametoa ushauri kwa wakleri na majandokasisi kuhusu wito, maisha na utume wao ndani ya Kanisa Katoliki.  (ANSA)

Papa Francisko atoa ushauri wa kina kwa wakleri na majandokasisi katika maisha na wito!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri na majandokasisi kutambua kwamba, wameitwa kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika maisha na wito wa kipadre, kumbe wanapaswa kuwa wafuasi waaminifu, daima wakiwa na mang'amuzi endelevu ya wito wao nyenzo msingi katika maboresho ya maisha na wito wao wa kipadre! Mapadre wa Majimbo Je?

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Hivi karibuni, tarehe 16 Marchi 2018, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa na mazungumzano na wanafunzi mapadri na waseminari walioko katika vyuo mbali mbali vya kikanisa Jijini Roma. Katika maswali yaliyoulizwa, Baba Mtakatifu amefafanua majibu yake kwa kujikita katika ufuasi wa Kristo, mang’amuzi endelevu ya wito, nyenzo msingi katika kuboresha malezi endelevu na karama ya mapadri wa jimbo.

Baba Mtakatifu anasema, mapadri wanaitwa kuwa wafuasi wa Kristo, wamisionari na ndugu kati yao. Mfuasi ni yule anayesikiliza maelekezo ya mwalimu wake, hivyo ni muhimu kujifunza kusikiliza sauti ya Mungu kila wakati. Iwapo kuhani anapata taabu kuielewa sauti ya Mungu katika utume na maisha yake, basi aige kutoka kwa mtoto Samueli (Rej., ISamueli 3), aende kwa kaka zake walio wakubwa na wenye uzoefu ili wapate kumsaidia namna ya kuisikiliza sauti ya Mungu na kuzungumza naye. Leo hii kuna tabia ya badhi kusikiliza yale wanayotaka kusikia wao na sio kile ambacho Mwenyezi Mungu anawaambia, halafu kuna wengine wanajifanya viziwi kwa kisingizio kwamba Neno la Bwana ni adimu kama nyakati za uovu wa watoto wa Eli (Rej., ISamueli 3:1). Lakini ukweli ni kwamba, mtu huyo anayejifanya kiziwi ndiye aliyejizimisha mwenyewe na kujitenga na Neno na ufunuo wa Mungu, kwani taa ya Mwenyezi Mungu inayoashiria sanduku la Agano ingali bado inawaka mpaka yatakapofika mapambazuko ya ukamilifu wa dahari (Rej., ISamueli 3:3).

Padri ni mmisionari na anatakiwa kuwa katika hija kila wakati. Mapadri wasichoke kuwapokea waamini na kuwahudumia katika mahitaji yao mbali mbali. Pamoja na umuhimu wa ratiba za shughuli za kichungaji, mapadri waepuke sana kuwafukuza waamini au kugoma kutoa huduma kwa sababu tu haiendani na ratiba, bali wachambue kwa utulivu uzito wa shida ya mwamini na mazingira yanayopelekea shida hiyo kuhitaji huduma kwa wakati fulani. Ni kwa namna hii siku za padri na za jumuiya nzima za wakristo zitakuwa katika hija, na pengine kutakuwa na surprise za kutosha tu, na huo ndio utamu wa kuwa mfuasi na mmisionari anayetenda utume wake kidugu pamoja na wenzake.

Padri hayuko peke yake sababu yeye sio kisiwa. Padri anatimiza utume wake na anaishi pamoja na mapadri wenzake, watawa na pamoja na waamini wote. Utume na maisha ya kidugu ni vya msingi sana katika kushirikishana changamoto mbali mbali na kutafuta suluhu za pamoja. Maisha ya udugu ni hija ya pamoja katika maisha ya kiroho ambapo mtu anakuwa pia na urafiki wa kiroho na urafiki wa kitume katika kushirikishana utume na maisha ya kila siku. Kutakuwa na nyakati za kushirikishana uchovu, changamoto, maumivu lakini pia furaha, vichekesho, mafanikio na kadhalika. Udugu huu sio wa mapadri wenza tu, bali pia udugu na urafiki na watawa wa kike na wa kiume pamoja na walei, jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anakuwekea jirani yako kadiri ya mapenzi yake.

Mang’amuzi endelevu ya wito ni jambo la msingi sana katika utume na maisha ya padre. Baba Mtakatifu anasema, kuna watu wanasemasema vimaneno kwamba Papa Francisko ameleta kimtindo cha mang’amuzi endelevu ya wito, kana kwamba ni ki fashion fulani cha enzi hizi. Kiuhalisia ni kwamba, mang’amuzi endelevu ya wito yanapatikana tayari katika Injili na katika histori nzima ya Kanisa. Kanisa katika maisha na utume wake limekuwa siku zote katika mang’amuzi endelevu. Hivyo maana ya kung’amua kama ambavyo Ratio fundamentalis, yaani mwongozo wa malezi ya kipadri unavyodadavua, ni ile hali ya kuchanganua na kutambua kwamba jambo fulani ni sahihi au la, kwamba jambo fulani linatoka kwa Mungu au ni mapenzi binafsi ya mtu ama ni ushawishi wa shetani. Katika uchambuzi na mang’amuzi ni lazima kubaini hayo yote na kufikia kufahamu kilicho cha kweli na cha haki.

Mang’amuzi endelevu ni lazima yafanyike katika sala, yaani mbele ya Mwenyezi Mungu ili kufahamu vema kile kinachoendelea ndani ya mtima wa mtu husika na katika roho yake, kisha mang’amuzi hayo lazima yalinganishwe kupitia mtu anayekusindikiza katika wito wako. Baba wa kiroho kwa kawaida hakuamulii mambo katika mang’amuzi, bali yupo kwa ajili ya kukuelekeza kwa umakini namna ya kutazama, namna ya kusikiliza na namna ya kufanya mang’amuzi, kisha mwishoni uamuzi unakuwa wa kwako binafsi. Katika mang’amauzi endelevu ya wito na maisha kwa ujumla, ni muhimu kuandika yale ambayo mtu anayaona, anayasikia, kuyachambua na kuyaamua katika mchakato wa mang’amuzi.

Kwa kawaida, pale ambapo mtu anakosa kufanya mang’amauzi endelevu ya kila siku, hatari zake ni kuwa baridi na mgumu ka chuma, anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mapadri wasiofanya mang’amauzi endelevu katika maisha na utume wao, huishia kurahisisha mambo kupita kiasi au kukata tamaa kwamba kitu fulani na fulani haviwezi kufanyika, na huwa wagumu na wazito katika kuendana na hali halisi ya maisha na kuhudumia watu, pengine hata ukali usio na maana. Hali za namna hii ni viashiria wazi kwamba padre mhusika hatoi nafasi kwa Roho Mtakatifu kutenda kazi ndani mwake.

Hivyo Baba Mtakatifu anawaalika mapadri kujifunza kutoka kwa mtume Petro na Filipo. Petro alipofika kwa jemedari Kornelio huko Kaisarea, aliona hata watu wa mataifa wamepokea Roho Mtakatifu, akafanya mang’amuzi ya haraka na kuamua kwamba hakuwa na sababu wasibatizwe kwa maji (Rej., Matendo 11: 44 – 48). Filipo aliruhusu Roho wa Bwana atende kazi ndani yake na kufuata maelekezo kuelekea njia panda ya Yerusalemu na Gaza, ndipo anakutana  na mkurugenzi wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia akisoma gombo la Isaya, na baada ya kumfafanulia akaomba kubatizwa na Filipo akafanya hivyo (Rej., Matendo 8: 26 – 40).

Kuna mapadri wengi wanaomtambua Mungu katika Utatu Matakatifu, na wanajitahidi kutenda utume wao kwa kiasi fulani, lakini wanajikuta matunda ya utume wao sio mengi na pengine hayadumu, au hata wanajikuta wanakwamisha mambo mengi au kuwakwaza wengi sababu hawaruhusu Roho Mtakatifu awaongoze, bali wanajitafutia mapito yao wenyewe na hivyo kujikuta wakipotea.

Mtu anayeishi ndani ya Roho wa Mungu hujikwamua kutoka utumwa wa kufanya utume kilelemama, kimayaimayai fulani, kutoka utumwa wa kukata tamaa na kukatisha wengine tamaa, kutoka utumwa wa ukali na kufukuza kondoo wanaohitaji kuhudumiwa katika kweli na haki kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwani Roho huyo atakayewaongoza ni Roho wa kweli. Kuna hatari ya mapadri wengi kuishi na kuwaongoza waamini kana kwamba Roho Mtakatifu hayupo kabisa na hajawahi kuwepo, kama anavyosimulia mtume Paulo alipofika Efeso anashangazwa walipata ubatizo gani sababu walimwambia kuhusu Roho Mtakatifu, hawajawahi hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu (Rej., Matendo 19: 1 – 7). Padri na waamini wote, hawataweza kukomaa kiroho iwapo hawataishi kuendana na Roho Mtakatifu anavyowavuvia katika utume na katika maisha ya kila siku, anasema Baba Mtakatifu.

Katika malezi fungamani ya majandokasisi na mapadri, pamoja na nyanja mbali mbali za kiroho, kielimu, kidugu, kisaikolojia, Baba Mtakatifu amesisitiza kwa namna ya pekee malezi ya kiutu ambayo inaonekana wengi kutotilia maanani na hivyo kushindwa kuzaa matunda bora na yenye kudumu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika mapadri wawe kweli mababa wenye uwezo wa kuzaa watoto kiroho na kiutu. Baba asiyeweza kuhusiana vizuri na watoto wake, au anayewanyanyasa, ama kutowatunza vema, ni bora aache kuwa Padri; kwani padri anaitwa kupenda, kuwa mwenye huruma, kufahamu kuhusiana vizuri, kucheka na anayecheka, kuhuzunika na anayehuzunika, kuwa karibu na anayeteseka, kufariji aliyekata tamaa, kucheza na watoto kwa heshima na kadhalika.

Mapadri wajitahidi pia kujipyaisha kadiri ya maendeleo ya sayansi, teknolojia, falsafa, taalimungu, Mafundisho ya Kanisa, utandawazi na mwenendo wa maisha kwa ujumla. Mapadri waepuke kuishi kwa mitindo ya kizamani wakati vitu vingi vinabadilika, lakini pia waepuke sana kushobokea mambo ya hovyo na kujikuta wanaharibu au hata kupotea wao wenyewe. Kila padre ajitambue udhaifu wake na akeshe kwa sala na maadili ili shetani asijekumnyuka mweleka na kuanza kumkejeli. Kila mmoja ni dhaifu, na iwapo mtu hautambui udhaifu wake, basi aombe wengine wamsaidie kuutambua na awe macho kila wakati katika hilo. Kila mtu atambue kwamba shetani yupo na kama simba anayezungukazunguka kutafuta mawindo (Rej., IPetro 5:8), akikukuta hujielewielewi anapita na wewe kiulaini ka kitoweo cha bure.

Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kusema kwamba, iwapo unaamini kuwa kuna Mungu katika Utatu Mtakatifu, malaika na watakatifu, basi ni muhimu kuamini pia kuna Ibilisi na jeshi lake ambao wana lengo la kuuvuruga ufalme wa Mungu, na wanatumia yeyote anayejisahau au kjiachia kihasara fulani katika mitindo ya maisha isiyofaa. Ingawa sio rahisi mapambano ya namna hii, mapadri wajitahidi na Mwenyezi Mungu atawasaidia kukwepa mishale ya yule mwovu.

Kuhusu karama ya mapadri wa jimbo, Baba Mtakatifu anasema kwamba, karama yao ni uzawa. Katika karama hiyo, mapadri wa jimbo watambue kwamba, kuna baba yaani Askofu jimbo, kuna watoto ambao wanakuwa ndugu kati yao, na watoto hao kwa nafasi yao wanazaa watoto ambao wanawatunza na kuwalea. Katika mahusiano kati ya baba na mwana, inawezekana baba akawa na tabia ngumu inayoogopesha watoto au hata wakati mwingine kutowasaidia sana. Hata hivyo ni muhimu kwa watoto kmheshimu baba yao na kujiweka karibu naye, sio kwa kujipendekeza au kupeleka umbea, bali kwa kumfanya Askofu jimbo ajitambue kuwa yeye ni baba na hivyo pole pole kuwa na matumaini ya kuishi na kutenda kwake kibaba. Hatari inayoweza kutokeasiku hizi, ni ile ya mtoto kutaka kumfuta baba yake katika maisha, jambo ambalo linamfanya mtoto kuonekana ndiye hafai kuliko hata baba yake.

Watoto wa karama ya uzawa, kwanza kabisa ni mapadri wenyewe, ambao wao wanakuwa ni ndugu kati yao. Kuwa ndugu maana yake ni kuishi kwa upendo, kusaidiana, kurekebishana kwa heshima pale mmoja anapokosea, na kisha kupanga na kutenda kwa pamoja. Mapadri waepuke kutendeana kwa husuda, waepuke kudharauliana, waepuke kutengana na kuishi kipweke, waepuke kusemana vibaya, waepuke kufurahia anguko la mwenzao, kwani kutenda kwa namna hii ni kuipoteza karama yao ya uzawa ndani ya jimbo.

Pili, ni watoto ambao wao mapadri wanawazaa kiroho na kiutu. Hawa ni waamini ambao wanakabidhiwa katika utume wao ili waishi nao kwa kujitambua kuwa wao ni mababa, na hivyo wawatunze na kuwalea vema, wakitambua wote ni watoto wapendwa wa Mwenyezi Mungu. Mapadri wawe karibu na watoto hao ili kila mwamini ajisikie kweli ni sehemu ya baba huyo, yaani mapadri wanaowahudumia. Hata hivyo wawe mapadri wanaotambua nafasi wanayopaswa kuiweka kati yao na watoto wao, wasiweke ukaribu utakaohatarisha mahusiano kati ya baba na watoto wake. Kwa mazungumzano na ushauri huo alioutoa Baba Mtakatifu kwa wanafunzi mapadri na waseminari waliopo Jijini Roma anasema, anaamini kabisa kwamba wakijitahidi kuishi kwa namna hiyo watakuwa watakatifu.

Ujumbe kwa Mapadre

 

19 July 2018, 08:47