Tafuta

Vatican News
Ajali ya moto nchini Ugiriki. Ajali ya moto nchini Ugiriki.  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na maafa ya moto nchini Ugiriki

Watu 79 kufariki dunia, wengine 550, wakiwemo watoto 23 kujeruhiwa vibaya na moto pamoja na magari zaidi ya 1, 000 kuteketezwa na moto mkali pamoja na makazi ya watu kuharibiwa vibaya, Jumatatu, tarehe 24 Julai 2018. Serikali ya Ugiriki imetangaza siku tatu za maombolezo. baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambi rambi kwa wote walioguswa na maafa haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amesikitishwa sana na taarifa za janga la moto lililotokea kwenye mji wa Mati, karibu na Athens nchini Ugiriki na kusababisha zaidi ya watu 79 kufariki dunia, wengine 550, wakiwemo watoto 23 kujeruhiwa vibaya na moto pamoja na magari zaidi ya 1, 000 kuteketezwa na moto mkali pamoja na makazi ya watu kuharibiwa vibaya, Jumatatu, tarehe 24 Julai 2018. Serikali ya Ugiriki imetangaza siku tatu za maombolezo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo, anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wale wote walioguswa na maafa haya makubwa, kwa uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwapokea mbele ya uso wake, wale wote waliofariki dunia kutokana na moto huu. Anaendelea kuwatia shime, majeruhi, ili waweze kupata nafuu na hatimaye, kurejea tena kwenye shughuli zao za kila siku.

Anapenda kutumia fursa hii pia kuvitia moyo vikosi vya uokoaji vinavyoendelea na shughuli zake, ili kuhakikisha kwamba, amani na usalama vinarejea tena katika eneo hili ambalo limeteketea kwa moto na kuwaacha wale waliosalimika wakiwa katika simanzi na majonzi makubwa. Anawaombea neema na baraka za kuweza kuvumilia yote na kuanza upya kwa ari na moyo mkuu. Taarifa zinaonesha kwamba, kwa kawaida, huu ni mji wa kitalii wenye wakazi 700, lakini wakati wa kiangazi, mji hufurika kwa uwepo wa watalii kutoka ndani na nje ya Ulaya.

Wananchi waliosalimika ni wale waliokimbilia baharini na kujitumbukiza humo, ili kukwepa kiwango cha joto kilichokuwa kinaongezeka maradufu kutokana na moto kusambaa kwa kasi sehemu mbali mbali za mji huo. Jumuiya ya Kimataifa imeonesha umoja na mshikamano kwa kutuma vifaa na wataalam wa vikosi vya zima moto kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watu kutoka Marekani, Israeli, Canada na Uturuki.

Wakati huo huo, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika salam zake za rambi rambi kwa wananchi wa Ugiriki anasema, inasikitisha kuona maafa makubwa yaliyosababishwa na moto huu, si tu kwa kusababisha vifo bali pia kuharibu mazingira, nyumba ya wote. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anapenda kuungana na viongozi wengine wa dini na serikali kuwafariji wale wote waliofikwa na maafa haya makubwa. Athari zake ni kubwa katika maisha na ekolojia katika ujumla wake.

Hiki ni kipindi cha kuonesha moyo wa umoja, upendo na mshikamano kwa familia ya Mungu nchini Ugiriki, ambayo kwa sasa inakabiliwa na hali tete sana! Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Ugiriki ilikumbwa na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa, kiasi hata cha kuacha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Ugiriki

Kwa upande wake, Askofu mkuu Sebastianos Rossolatos, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ugiriki, kwa niaba ya Kanisa Katoliki nchini humo, anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa msiba huu mkubwa uliowakumba wananchi kutoka ndani na nje ya Ugiriki. Idadi ya watu wanaoendelea kufariki dunia inaongezeka. Kanisa linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa wote walioathirika kwa maafa haya kwa kuwasaidia kwa hali na mali.

Majanga asilia yanayosababishwa na shughuli za binadamu ni nafasi nyingine tena ya kutafakari kwa kina umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwani athari zake ni kubwa katika ekolojia nzima. Watu wajifunze kuheshimu sheria, kanuni na utunzaji bora wa mazingira.

Ajali ya moto

 

25 July 2018, 14:35