Tafuta

Vatican News
ETHIOPIA-ERITREA-POLITICS-PEACE-TALKS ETHIOPIA-ERITREA-POLITICS-PEACE-TALKS  (AFP or licensors)

Papa Francisko apongeza majadiliano ya amani Pembe ya Afrika

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili Mosi, Julai 2018 ameyaelekeza mawazo na sala zake kwa familia ya Mungu nchini Nicaragua ili demokrasia iweze kushika mkondo wake; Siria ili kuwapunguzia mateso na kwamba, kuna matumaini ya amani huko Pembe ya Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe Mosi Julai 2018, aliyaelekeza mawazo yake nchini Nicaragua, Siria na Pwani ya Pembe ambako cheche za majadiliano ya amani zimeanza kuonekana! Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika mchakato wa majadiliano ya umoja wa kitaifa, ili kuweza kuondokana na machafuko ya kisiasa nchini humo, ili hatimaye, demokrasia ya kweli iweze kushika mkondo wake.

Hali ya Kisiasa nchini Nicaragua: Jumanne, tarehe 3 Julai 2018, majadiliano katika ukweli na uwazi yanafanyika huko nchini Nicaragua kwa ushiriki mkamilifu wa Tume ya Kimataifa ya Haki Msingi za Binadamu. Hadi sasa Rais Daniel Ortega wa Nicaragua hajaridhia ombi la Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua la kufanya mapema uchaguzi mkuu, ifikapo mwezi Machi 2019. Maaskofu pia wamependekeza wateuliwe viongozi wapya wa Tume ya Uchaguzi na Mahakama kuu! Maaskofu wanakaza kusema, kiongozi wa kweli, hana budi kusikiliza na kujibu kilio cha watu wake kwa hekima na busara! Umoja wa Mataifa unapenda kushiriki kikamilifu katika kudhibiti ghasia, fujo na vurugu zinazoendelea nchini Nicaragua kiasi cha kutishia amani na usalama wa raia na mali zao.

Siria hali bado ni tete sana hasa Jimbo la Dar’aa ambako kuna idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha kutokana na mashambulizi ambayo yameharibu hata shule, hospitali na kusababisha idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji kutafuta: usalama na hifadhi ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaendelea kusali kwa ajili ya watu hawa wanaoteseka na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha mashambulizi dhidi ya watu hawa ambao kwa hakika wamejaribiwa sana kwa miaka ya hivi karibuni!

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anasema, hali kwa sasa inatisha na kwamba, kuna haja ya kuweka ulinzi zaidi kwa ajili ya raia na mali zao! Msaada wa dharura upelekwe moja kwa moja nchini Siria ambako watu wanateseka zaidi!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, licha ya machafuko ya kisiasa nchini Nicaragua na mashambulizi huko Siria, lakini, bado kuna habari njema na cheche za matumaini ambazo zimeibuka hivi karibuni huko kwenye Pembe ya Afrika, baada ya kipindi cha miaka 20 ya “ubaridi wa kisiasa”, Serikali ya Ethiopia na Eritrea zimerejesha tena mchakato wa majadiliano ya amani kati ya nchi hizi mbili, tukio ambalo linawasha cheche za matumaini kwa Nchi za Pembe ya Afrika na Bara la Afrika katika ujumla wake!

Hizi ni juhudi ambazo zimefanywa kati ya Rais Isaias Afeworki wa Eritrea pamoja na Waziri mkuu mpya wa Ethiopia Bwana Ahmed Abiy, ili kuanzisha mchakato wa upatanisho na msamaha kati ya mataifa haya mawili. Ethiopia inapenda sasa kutekeleza Mkataba wa Amani uliotiwa mkwaju kunako mwaka 2000 ili kuokoa maisha ya watu kutokana na misigano na malumbano yasiokuwa na tija wala mashiko. Itakumbukwa kwamba, kati ya Mwaka 1998 hadi mwaka 2000, zaidi ya watu 80, 000 walipoteza maisha kutokana na vita kati ya nchi hizi mbili. Kumbe, majadiliano ya haki, amani na maridhiano kati ya nchi hizi mbili ni hatua kubwa kuelekea katika ujenzi wa amani kati ya Ethiopia na Eritrea.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya Sala kwa familia ya Mungu nchini Thailand, ambayo imeingiwa nahofu kubwa baada ya wachezaji 12 pamoja na kocha wao kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa takribani majuma mawili sasa, huko Mae Sai Chiang Rais, Kaskazini mwa Thailand.

 

01 July 2018, 08:12