Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akisalimiana na mahujaji wa Chama cha Watumishi wa Altareni, 31 Julai 2018. Papa Francisko akisalimiana na mahujaji wa Chama cha Watumishi wa Altareni, 31 Julai 2018.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu na wokovu wa binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, jioni, tarehe 31 Julai 2018 amekutana na watumishi wa Altareni na kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu. Umekuwa ni muda wa sala na tafakari mbali mbali kuhusu Injili ya amani duniani, ili kweli vijana hawa waweze kuwa ni: vyombo na mashuhuda wa upendo, msamaha, ukweli, umoja na mshikamamo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Watumishi wa Altareni kwa mwaka 2018 mjini Roma inaongozwa na kauli mbiu “Utafute amani ukaifuatie. Hii ni changamoto kwa vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya amani duniani kwa kuondokana na woga pamoja na maamuzi mbele yasiyokuwa na mvuto wala mashiko! Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, jioni, tarehe 31 Julai 2018 amekutana na watumishi wa Altareni na kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu. Umekuwa ni muda wa sala na tafakari mbali mbali kuhusu Injili ya amani duniani, ili kweli vijana hawa waweze kuwa ni: vyombo na mashuhuda wa upendo, msamaha, ukweli, umoja na mshikamamo.

Vijana wanataka kuwa kweli ni vyombo vya matumaini, mwanga na furaha ya maisha, daima wakiendelea kujibidisha katika njia ya utakatifu wa maisha! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, amewataka vijana hawa kufanya yote kwa utukufu wa Mungu, huu ni muhtasari wa urafiki wa dhati na Kristo Yesu, ili kutenda kwa haki; kwa kusikiliza na kumtambua Mwenyezi Mungu anayezungumza kutoka katika undani wa dhamiri ya mtu, ili hatimaye, kung’amua mapenzi yake. Utukufu wa Mungu ni msingi wa dhamiri nyofu.

Watu wote watambue kwamba, wao ni watoto wa Mungu, kumbe wanapaswa kujitahidi kuwapendeza wote katika mambo yote, ili wapate faida ya kuokoka. Vijana wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanawasha mwanga wa matumaini na furaha katika maisha, kama njia ya kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu na furaha ya imani inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo. Kwa njia ya jitihada hizi, watu wengi wataweza kumtambua Kristo Yesu kuwa ni Mkombozi wa dunia na tumaini la walimwengu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana wanaweza kutekeleza dhamana na wajibu huu kwa kumuiga Kristo Yesu, kama alivyofanya Mtakatifu Paulo mwalimu na mtume wa mataifa pamoja na watakatifu wengine wote. Kwa njia ya maisha na utume wao, wamekuwa kweli ni mashuhuda wa Injili hai, wakijitahidi kuhakikisha kwamba, wanamwilisha tunu msingi za Kiinjili katika vipaumbele vya maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, ambaye anakumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai. Mtakatifu Inyasi katika maisha na utume wake, daima alifanya yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kweli akawa ni kiini na maana ya maisha yake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawataka watumishi wa Altareni kuiga mifano ya watakatifu kwa kutenda yote kwa utukufu wa Mungu na wokovu wa binadamu!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

 

31 July 2018, 09:57