Tarehe 25 Julai 2018 Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI achapishe waraka wa Kitume "Humanae vitae" yaani "Maisha ya Mwanadamu". Tarehe 25 Julai 2018 Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI achapishe waraka wa Kitume "Humanae vitae" yaani "Maisha ya Mwanadamu". 

Waraka wa Kitume: "Humanae vitae" yaani "Maisha ya Binadamu" Miaka 50 tangu uchapishwe

Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka huu wa kitume, alipembua kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Akakazia: wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Mwenyeheri Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968, miaka 50 iliyopita, alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”. Ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Mwenyeheri Paulo VI anayetarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018. Anakita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha! Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, zinazotaka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, sadaka na majitoleo binafsi. Monsinyo Gilfredo Marengo, Rais wa Taasisi ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Ndoa na Familia anasema, Mwenyeheri Paulo VI alikuwa mwamba wa Injili ya familia na kamwe hakutikisika katika maamuzi na mafundisho yake ya kina!

Nchi zilizoendelea ziliona kwamba, ongezeko la watu duniani, lilikuwa ni tishio kwa ustawi na maendeleo yao. Kutokana na mantiki hii, wachumi wakawatangazia watu raha, starehe na anasa kwa kufumbata utamaduni wa kifo na matokeo yake, leo hii kuna nchi ambazo zinalia na kuomboleza kutokana na kuwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa kila mwaka pamoja na kuendelea na kuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa.

Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka huu wa kitume, alipembua kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Akakazia kwa namna ya pekee, wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha, kwa kuheshimu mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa mwelekeo huu, wanandoa wanaweza kuwa kweli waaminifu katika tendo la ndoa na mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kukataa kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo, unaofumbatwa katika vitendo vya utoaji na uzuiaji mimba, vinavyowekwa mbele ya macho ya watu wengi kama njia muafaka ya kufurahia maisha na kusahau kwamba, majuto ni mjukuu na baada ya kisa ni mkasa! Ekolojia ya binadamu inapaswa kulindwa na kudumishwa kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu!

Kanisa linakazia umuhimu wa waamini kuambata kanuni maadili na utu wema; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa linapenda kuwaona waamini wake wakiwa makini kushuhudia Injili Familia inayoambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waraka  wa “Maisha ya binadamu” unapaswa sasa kusomwa pia kwa mwanga wa “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Injili ndani ya familia” ambao umechapishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko anayekazia umuhimu wa: Injili ya Familia, Injili ya Uhai, Utu na heshima ya binadamu. Papa Francisko anapembua kuhusu wito wa familia; umuhimu wa upendo ndani ya familia; upendo unaozaa upendo kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; kwa kuenzi na kudumisha udugu na mshikamano. Anakazia umuhimu wa malezi na majiundo makini kwa watoto, bila kusahau changamoto zinazowakabili wanandoa.

Mwenyeheri Paulo VI aliona changamoto hizi, akazivalia njuga kiasi cha kubaki peke yake akikabiliwa na kinzani kutoka ndani na nje ya Kanisa. Aliwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kuheshimu Injili ya Uhai kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Huu ni mwaliko wa kukata katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo unaojielekeza hata wakati mwingine wa kutaka kupata watoto kwa gharama yoyote ile. Matokeo yake ni baadhi ya wanawake kugeuzwa kuwa ni maabara ya kuzalisha watoto kwa njia ya chupa! Hapa kuna hatari ya watoto kugeuzwa kama bidhaa inayoweza kupatikana sokoni ikiwa kama mtu ana jeuri ya “vijisenti” vyake, au “vijisenti vya mboga”.

Lakini ikumbukwe kwamba, mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi katika kifungo cha ndoa, kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. Upendo katika maisha ya ndoa na familia unajikita katika uhuru, wajibu na utashi kamili. Hapa si mambo ya mtu kujisikia tu! Waraka huu haukupokelewa kwa mikono miwili, hali ambayo hata Mwenyeheri Paulo VI alitambua fika kwamba, angekumbana nayo, lakini akasimama kidete na kwa moyo mkuu kutangaza Injili ya Uhai inayojikita katika utu na heshima ya binadamu kadiri ya mpango wa Mungu.

Papa Paulo VI alionesha dhamana na wajibu wa Kanisa katika kulinda, kutetea sanjari na kuendeleza maisha ya mwanadamu bila kuogopa. Binadamu anapaswa kupewa heshima na kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo ya binadamu na kamwe asigeuzwe kuwa ni kichokoo cha tamaa za kibinadamu. Ndoa iwe ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa mwanadamu unaowajibisha na unaopania kuendeleza kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu!

Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” unapaswa kusomwa pia katika mwanga wa Waraka wa Mtakatifu Yohane Paulo II: Injili ya uhai sanjari na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Injili ndani ya familia”. Hizi ni nyaraka zinazoshibana na kukamilishana katika kutangaza Injili ya uhai inayofumbatwa katika tunu msingi za Injili ya familia, kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu kushiriki kikamilifu katika mpango wa kazi ya uumbaji!

Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, lilifanya maandamano makubwa yaliyowahusisha waamini na watu mbali mbali kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Waraka huu wa Kitume, unaotoa mafundisho tanzu kuhusu: mpango wa Mungu katika maisha ya ndoa na familia; upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na dhamana na malezi na makuzi kwa watoto wao. Kauli mbiu ya maandamano haya ilikuwa Familia ni kitovu cha upendo na urithishaji wa maisha.

Maandamano haya yalilenga kupinga: nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kazi za suluba, utumwa mamboleo, ndoa za utotoni na mauaji ya watoto ambao pengine wanatolewa kafara. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwapokea, kuwalinda, kuwatunza na kuwaendeleza watoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watoto wana haki ya kupata malezi bora na makini ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi dhidi ya jamii inayoogelea katika rushwa, ufisadi,  udini na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi!

Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuzingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Ili kufanikisha azma hii, wazazi wanapaswa kuwajibika barabara katika maisha ya ndoa na familia; kwa kuishi tunu msingi za Kikristo pamoja na kuhakikisha kwamba, familia zao zinakuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa sala na utakatifu wa maisha. Vijana wanapaswa kufundwa vyema jinsi ya kuheshimu miili yao kwani ni Mahekalu ya Roho Mtakatifu. Vijana watambue, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia, ili waweze kuwa tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Injili ya uhai

 

 

25 July 2018, 14:01