Tafuta

Papa Francisko atoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Yemen walioko Korea ya Kusini. Papa Francisko atoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Yemen walioko Korea ya Kusini. 

Mshikamano wa Papa Francisko kwa wakimbizi toka Yemeni

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia mambo msingi na kutaka kuonesha umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, kwenye Kisiwa cha Jeju (Cheju), huko Korea ya Kusini, ametoa kiasi cha Euro 10, 000 kama mchango wa Kanisa kwa ajili ya kuwahudumia wahamiaji 500 kutoka Yemeni ambao wamekwama kisiwani hapo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa anakazia mambo makuu yafuatayo: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. “Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kutumia njia za halali za uhamiaji na wala si kuwasukumizia watu hawa katika maeneo ambamo wanaweza kukabiliana na dhuluma na vita kwa kuweka uwiano mzuri kati ya usalama wa taifa na umuhimu wa kulinda haki msingi za binadamu. “Kuwalinda” ni dhamana ya kutambua haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa wakimbizi na wahamiaji wote wanaokimbia hatari za maisha kwa kutafuta hifadhi ya kisiasa, usalama na kuhakikisha kwamba, hawanyonywi.

Baba Mtakatifu anasema, “Kuwaendeleza” ni dhana inayojikita katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu ya wakimbizi na wahamiaji: Biblia inafundisha kwamba “Mungu anampenda mgeni, anamvisha na kumpatia chakula” kumbe, “wapendeni wageni kwani hata ninyi mlikuwa wageni nchini Misri”. “Kuwahusisha” maana yake ni kuwawezesha wakimbizi na wahamiaji kushiriki kikamilifu katika maisha ya jamii inayowakirimia kama sehemu ya mchakato wa kutajirishana na ushirikiano unaodumisha maendeleo endelevu na fungamani kwa Jumuiya mahalia.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia mambo haya msingi na kwa kutaka kuonesha umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, kwenye Kisiwa cha Jeju (Cheju), huko Korea ya Kusini, ametoa kiasi cha Euro 10, 000 kama sehemu ya mchango wa Kanisa kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji 500 kutoka Yemeni ambao wamekwama kisiwani hapo. Kiasi hiki cha fedha kimepokelewa na Askofu mkuu Alfred Xuereb, Balozi wa Vatican nchini Korea, aliyewatembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama ushuhuda wa mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa uapande wake, Askofu Peter Kang wa Jimbo Katoliki Jeju (Cheju) ameitaka familia ya Mungu Jimboni mwake kuonesha moyo wa upendo, amani na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji, hawa kutoka Yemen wanakokimbia: vita, njaa, umaskini na magonjwa yanayoendelea kupukutisha maisha ya watu kila kukicha. Kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Yemeni, kumekuwepo na idadi kubwa ya wananchi wa Korea ya Kusini ambao hawana tena fursa za ajira, kwani sehemu kubwa ya kazi zinafanywa na wakimbizi pamoja na wahamiaji kutoka Yemeni ambao hawachagui wala kubagua kazi, bali apate haki zake msingi.

Wachunguzi wa mambo wanasema, wananchi wengi wa Korea ya Kusini wameonesha moyo na ari ya upendo na mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji kutoka Yemeni. Hawa ni watu wanaokumbuka historia ya maisha yao, kwani hata wao, wamewahi kuonja huruma na upendo kutoka kwa watu sehemu mbali mbali za dunia.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umezindua kampeni ya amani nchini Yemeni ili kusaidia mchakato wa kusitisha vita ya wenyewe kwa wenyewe, ambayo kwa sasa imedumu kwa takribani miaka minne. Umoja wa Mataifa umeombwa kupeleka watunza amani, ili kuwahakikisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao. UNICEF inasema, kuna uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji, jambo linalotishia uwepo wa magonjwa ya milipuko hasa miongoni mwa watoto wadogo. Uharibifu wa miundo mbinu ya maji na majengo ya huduma msingi za binadamu ni kinyume kabisa cha sheria na haki za kimataifa. Inasikitisha kuona kwamba, hata watoto wadogo bado wanachukuliwa na kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita, jambo ambalo linakiuka haki msingi za watoto, ambao mara nyingine wanatekwa kutoka kwenye familia zao.

Sikiliza kwa raha zake mwenyewe!

 

31 July 2018, 15:16